Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Mh. Hawa Ghasia akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya uzinduzi wa Kituo cha Mtandao cha Kenya uliofanyika hivi karibuni Dar. Kushoto ni Balozo wa Kenya nchini, Boaz Mbaya, na Katikati ni Mkurugenzi wa Tanzania Global Development Learning Centre (TGDLC) Charles Senkondo.


Mfumo mpya wa ajira serikalini
Na Pascal Mayalla


Serikali haitaajiri watumishi wa umma wa kuanzia ngazi za maofisa waandamizi, bali sasa nafasi za kazi katika ngazi hizo, zitakuwa ni za uteuzi na zitagawiwa kwa watu wenye sifa walio ndani ya utumishi wa umma kinyume na ule utaratibu wa kuzitangaza kwa ushindani wa uwazi kwa kila mtanzania mwenye sifa kuwa na haki ya kuomba.
Uamuzi huo, umetangawa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bibi Hawa Ghasia, katika hafla ya kumuaga Mwenyekiti mstaafu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji msataafu, Lameck Mfalila, makamishina wa tume hiyo na wafanyakazi waliostaafu, iliyofanyika mwishoni mwa wiki katika viwanja viwanja vya Leaders Club, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Waziri Ghasia emesema, uamuzi huo wa serikali, unafuatia mabadiliko ya Sheria ya Utumishi Namba 7 ya Mwaka 2002, yaliyofanywa na Bunge hivi katika kipengele cha ajira katika utumishi wa umma kwa ngazi za maofisa waandamizi sasa sio za ushindani wa wazi.
Waziri Ghasia amesema, lengo la mabadiliko hayo ni kuipunguzia serikali mzigo wa kuendesha mafunzo ya mara kwa mara kwa maofisa wanaoajiriwa toka nje ya serikali, na kusisitiza kuwapandisha vyeo maofisa wa serikali wenye sifa na utendaji wao unajulikana kutaleta tija zaidi kuliko kuajiri watanzania wenye sifa ambao utendaji wao haujulikani.
Hata hivyo Waziri Ghasia amesema uamuzi huo hauna maana kuwa watanzania wenye sifa walio nje ya serikali sasa hawana nafasi tena katika uongozi wa utumishi wa umma, ila bado watanzania wenye sifa wataendelea kuajira katika utumishi wa umma pale ambapo hakutakuwa na watumishi wa umma wenye sifa zinazotakiwa.
Naye Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bibi Thecla Shangali, amewasisitizia watumishi wa umma kuzingatia taratibu sheria na kanuni katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ili utendaji wa serikali upate mafanikio yaliyokusudiwa na kuleta tija kwa maendeleo ya taifa.
Mwenyekiti mstaafu wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu, Lameck Mfalila, amesema anajivunia sifa ya kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa tume hiyo iliyoundwa mwaka 2002 na mafanikio makubwa ya tume hiyo iliyoyapata katika kipindi kifupi ambapo ni pamoja na kubadilisha sura na mitazamo ya watumishi wa umma toka utumishi wa zamani ambao ni utumishii tuu mpaka sasa kwenye utumishi wa umma unazingatia matokeo huku ukifanya kazi kibiashara kwa kufuata kanuni za mikataba ya huduma kwa wateja.
Jumla ya makamishna watano wa tume hiyo ewamestaafu na mwenyekiti wao sambamba na wafanyakazi 3 wa tume hiyo akiwemo, Naibu Katibu wa tume hiyo, Bibi Prisilla Ole Kambainei.


Upanuzi wa TGDLC
Kituo cha Tanzania cha Taaluma ya Maendeleo kwa njia ya Mtandao cha Tanzania Global Development Learning Centre (TGDLC), kinakabiliwa na changamoto kubwa ya kusambaza huduma zake zifike mikoani ili Watanzania wengi zaidi waweze kufaidika na huduma zinazotelewa na kituo hicho kuliko hali ilivyo sasa ambapo huduma za kituo hicho ziko jijini Dar es Salaam pekee.
Changamoto hiyo imetangazwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kituo hicho, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. George Yambesi wakati wa hafla fupi ya kumuaga Mwenyekiti Mstaafu wa Bodi ya Kituo hicho Bibi Mollel, ambaye sasa ni Katibu Mkuu ofisi ya Makamo wa Rais.
Bw. Yambesi amesema, tangu kuanishwa kwa kituo hicho mwaka 2000, tayari kimeishapata mafanikio makubwa kwa kuendesha kozi na mijadala mablimbali ya kimataifa kwa njia ya mtandao wa video hali iliyopelekea kuokoa mabilioni pya fedha za kigeni ambazo zingetumika kuwapeleka maofisa hao nje ya nchi.
Amesema kufuatia mafanikio hayo katika medani za kimataifa, kituo hicho kinakabiliwa na changamoto ya kusambaza huduma zake mikoani ili kuwafikia Watanzania walio wengi zaidi na kuzidi kuokoa fedha zinatakozotumika katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Msataafu, Bibi Mollel, amesema anajisikia faraja sana kuwa sehemu ya mafanikio makubwa ya kituo hicho katika kipindi cha uongozi wake, na kusisitiza ana imani kubwa na uongozi wa kituo hicho chini ya Bw. George Yambesi kwa sababu anamfahamu vizuri, amefanya nae kazi kwa karibu hivyo mafanikio ya kituo hicho yatapanda kwa kasi zaidi.
Bibi Mollel aliipogeza menejimenti na wafanyakazi wa kituo kwa moyo wa dhati wa kujituma katika kazi, kuwa na ushirikiano wa hali ya juu miongoni mwao na katika kuhudumia wateja wao na kueleza kuwa ndiyo siri kubwa ya mafanikio ya kituo hicho.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo hicho, Bw. Charles Senkondo, amesema kituo chake kimeipokea changamoto iliyoko mbele yake kwa moyo mmoja na kuanza kuifanyia kazi mara moja na kusisitiza kuwa kituo chake tayari kimeishafanya mipango mkakati wa kusambaza huduma zake mikoani kwa kuanzia na mikoa ya Arusha, Dodoma, Mwanza, Tanga, Mbeya na Morogoro.
Bw Yambesi amechukua nafasi ya mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa kituo hicho toka kwa Bibi Mollel kwa mujibu wa sheria ya kituo hicho ambapo mwenyekiti wake wa bodi, ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Mwisho.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 16 mpaka sasa

  1. HUYO JK WENU HUKO NAONA KAMA SIO MUISLAM HUPATI CHEO HUKO. mWE!

    mwislamu mkereketwa..FINLAND

    ReplyDelete
  2. sasa hapo ndio serikali ya bongo inapochemsha baada ya kwenda mbele inarudi nyuma, ndio yale yale ya kurithishana madaraka, ukiharibu hapa unahamishiwa kule nako ukaharibu halafu mnatuimbia nyimbo za maisha bora kwa kila mdanganyika. upuuzi mtupu...serikali zenye kutaka maendeleo ya haraka lazima waingize nguvu mpya zenye mawazo mapya ambazo zitaleta mabadiliko katika mifumo ya uendeshaji serikali na sio uzoefu maana kama uzoefu CCM na serikali yake ina miaka zaidi ya arobaini kwenye uongozi na nchi imezama bado kwenye dimbwi la umasikini.

    ReplyDelete
  3. Salaam... Duh kweli sasa tunapoenda nana ndipo penyewe manake unaambiwa ili uwe ofisa (kuanzia ngazi ya ofisa mwandamizi) serikalini wewe lazima uwe upo ndani hakuna tena mambo ya "competitive selection" kama zamani, sheria mpya hiyo ya 2002.... Hapo ina maana kama wizara imeoza, wacha tuendelee na uozo wetu hatutaki damu na mawazo mapya. Kweli watu wanajua kulinda nafasi/chakula chao manake wanajua mtama ukiwekwa nje kuna majamaa yametoka kubeba maboksi kama sisi yanajua mambo kwelikweli hivyo inabidi tuwa "boksi out" kwenye vinyang'anyiro vya ulaji... Makubwa haya.... kulikuwa na ile Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi mpya; sasa sio mbaya manake kila kitu kipya kasoro watendaji. Kaazi kwelikweli hii...

    Mungu Ibariki Tanzania na Watu Wake!!

    ReplyDelete
  4. Kwa nijuavyo mimi Mheshimiwa Waziri umechemsha kwani hiyo sasa unakaribisha Rushwa,unalinda maslahi ya waliondani ya Wizara,Hupanui ajira,Lakini chamsingi ni kwamba ndiyo katika mtindo ule ule kwamba mtakula mpaka kufa bila kuajiri wengine.Huu ni "U KINGUNGE".TOOOBA!

    ReplyDelete
  5. Wewe uliyetoa comment ya kwanza hapo juu ya kuhusu uislamu hebu tutolee udini hapa, watu kama nyinyi ndiyo mnaotuletea vita katika nchi zetu za Afika. Mimi binafsi naona hapa serikali imechemsha...yaani kweli huu ni ubinafsi wa hali ya juu, mwe!!!

    ReplyDelete
  6. serikali hii inatia aibu pengine kuliko zote zilizotangulia. Yaani watu wameshika madaraka ya juu lakini hawajiamini kabisa. No wonder nchi inanuka kwa umasikini.

    ReplyDelete
  7. siku nyengine michuz summarise mijiujumbe kama hii, ni mirefu sana, inashosha kusoma, ni kama umechapisha gazeti zima. please summarise it up!!!!!

    ReplyDelete
  8. Anon wa kwanza umekosa la kuongea naona au ulikuwa umetoka usingizini nini? Hapo kilichoandikwa ni kuwa hawatatoa nafasi za kazi za uandamizi kwa watu wa nje ila watapeana wenyewe humo kwa mumo katika idara husika za serikali, sasa hapo JK ameingiaje? Na Uislamu umeingiaje? Mmeanza kama wakati ule Mwinyi alivyokuwa raisi, kwani mbona JK hakuchaguliwa na waislamu peke yake. Msitake kuleta vitu ambavyo havipo katika mada.

    Nikirudi kwenye mada kweli hili ni pigo takatifu hasa sie tunaobukua na kubeba maboksi huku nje naona wameamua kuweka kauzibe. Lakini tutabanana hapo hapo, hivyo vizee kuna siku vitaishia tu watake wasitake. Watu wengine bwana kung'anga'nia madaraka! Watangaze watu wa apply kwa ujuzi na qualification zao na hao waliomo ndani waapply pia tushindane kwenye ujuzi, uzoefu na kwalifikesheni sio tu kwa uzoefu peke yake. Dah hii kali ndoto yangu yote imezimika.

    KUDADADEK!!!

    ReplyDelete
  9. Mfumo huu mpya wa ajira :-
    1. Ni wa kibaguzi maana hautoi fursa sawa kwa Watanzania wote na hivyo ni kinyume kabisa na Katiba yetu ya JMT

    2. Ni ilioridhika kuwa watumishi bora viongozi ni tu ambao tayari wamo ndani ya Serikali. Hapa kuna harufu ya mtindio wa maana halisi ya 'civil society'ambapo kila mtu ana thaminiwa mchango wake na kupewa fursa sawa kwa sifa zake.

    3. Ni unaopingana na sera za ILO na hata msisitizo wa ilani ya uchaguzi wa CCM juu ya soko huria hata la ajira na kuongeza ushindani hata katika kuwasaka watumishi viongozi bora ndani ya nchi.

    Ni aibu ktk karne ya 21 mtaalamu wa maendeleo ya rasilimali Wanadamu na mtetezi wa haki za binadamu kutetea mfumo feki ambao haujawahi kuwepo ulimwenguni isipokuwa kwa madikteta wanao hofu kupanua wigo wa ushindani na wanaoogopa kupata changamoto kutoka binadamu wengine wenye uzoefu na elimu ktk nyanja mbalimbali toka nje ya mfumo wa serikali.

    Aidha ili kukamilisha sera hii feki basi na mtindo huo huo uendelee hata tusione mtu anapewa uwaziri mpaka awe aliwahi kuwa naibu waziri na mtu kamwe asithubutu kuomba uraisi mpaka awe aliwahi kuwa makamu wa rais. Kimsingi hata tusione Mwanajeshi fulani anateuliwa kuwa DC au RC maana hapo hakuna justification ya kupandisha mtu wadhifa katika uzoefu wake. Nafasi hizo hasilani zibaki ni kwa ma RAO & DAS tuone!!
    Sera hii iendelezwe pia na NGO's, tusione mstaafu wa serikali anapewa nafasi kubwa popote katika NGO au CBO yeyote wala katika Mashirika ya dini. Na mtu ambaye hakuwa mfanya biashara asikubalike kuwa mfanya biashara mkubwa ni lazima aanze na kabiashara kadogo ka kuuza nyaya za mafungu sokoni.
    Na mtu asipelekwe kushiriki ktk Olympic mpaka tuwe tumemwona kuwa ameshashiriki Olympic siku zote za nyuma hata kama kabisa tunaona kuwa kiwango chake ni kile kinachokubalika!!

    Mimi huwa sipendi kabisa kesi lakini katika hili hata niko tayari kuipelleka serikali mahakamani chini ya movement ya ÇHAMA CHA WAAJIRIWA' kufuta sera hii maana inapingana na sheria yake mama (Katiba) na pia itahatarisha umoja wa Watanzania na zaidi ya yote inapingana na kanuni ya uendelezaji wa maboresho ktk menejiment ya umma.

    This very policy sounds like that of mass production and traditional brand protectionism! Maana ingekuwa pote ni hivi, Je, Asha Rose angepewa dhamana na ofisi aliyo nayo sasa UN???????

    SHULE:
    Sera ya ajira ijali sifa na uzoefu wa utelelezaji wa majukumu yaliyo ndani ya nafasi iliyo wazi. Na MTANZANIA yeyote mwenye sifa zaidi kuliko wengine walioomba au wanaoonekana kufaa (bila kujali mwajiri wake wa awali)achaguliwe au ateuliwe au aajiriwe.


    Nyakatakule Unyilisya Echalo

    ReplyDelete
  10. Sioni tatizo la utaratibu wa kuwapandisha waliopo kuwa maafisa waandamizi na kuendelea. Mtu hapandishwi bila utendaji kazi wake kuwa mzuri na hawa wanaopandishwa wanaingia kwenye civil service kama maofisa wa kawaida wanapofanya vizuri sioni tatizo la kuwareward kwa kuwapandisha. Wakipandishwa wanacreate vacuum chini na wanaotaka kujoin waombe waanze kama walivyoanza wengine. Sioni kuzibwa kwa ajira hapa...labda ndio utamaduni wetu mpya wa kulalamikia kila jambo la serikali

    ReplyDelete
  11. MTINDO WA AWALI HAUKUWA MZURI KWANI ULISABABISHA WATOTO, WAKE , WAKWE, MASHEMEJI NA NYUMBA NDOGO KUKOSA NAFASI NZURI PIA BAADHI NYA NAFASI ZILICHUKULIWA NA WATU AMBAO WANATOA SIRI ZA MIKATABA KWA WAPINZANI WETU HII NI HATARI KWA CHAMA CHETU KITUKUFU NA TAIFA KWA UJUMLA.

    ReplyDelete
  12. Kila mtu atabeba mzigo wake jamani, maana yake kila mtu atalea familia yake.

    Hebu tuamshe majadiliano ya kimabadiliko ya sera za nchi. huu undugunization na ujamaanization pamoja na urafikinization vitatufikisha pabaya.

    ReplyDelete
  13. Anon wa dec3,5:59 anasema

    "Sioni tatizo la utaratibu wa kuwapandisha waliopo kuwa maafisa waandamizi na kuendelea. MTU hapandishwi bila utendaji kazi wake kuwa mzuri"

    Mgogoro wa kauli yako unakuja katika kueleza maana ya hilo neno ulilolitumia bila kufikiri kwa undani lijulikanalo kama 'MTU'; maana kwa mjibu wa sera hiyo unayoitetea 'MTU' SASA NI YULE TU ALIYE MFANYAKAZI SERIKALINI!

    Hakuna anayepinga kupandishwa vyeo watumishi wazuri walioko Serikalini; TUTACHOSEMA, NAFASI INAPOKUWA WAZI ITANGAZWE NA YEYOTE (WA NDANI AU NJE ) AOMBE na sifa za mtu ndo zimpe kazi hiyo siyo nawe kuendeleza kautamaduni ka kutetea jambo tu eti kwa vile limeletwa na serikali, Serikali ndio sisi sasa tunaotoa maoni.

    AFISA UTUMISHI MWANDAMIZI - ARUSHA

    ReplyDelete
  14. Michuzi sheria iliyofanyiwa marekebisho ni sheria NO.8 ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002 na sio sheria NO.7 ya 2002.

    ReplyDelete
  15. Afisa utumishi mwandamizi, ukitaka kuleta mdahalo na mimi huniwezi. Ukitaka kuchambua uandishi hapa utakuwa unakosea. Hapa kwa michuzi hatuandiki kama tunaandika thesis hivyo usahihi ni relative na mimi sioni tatizo maana nilipotumia neno mtu kweli nilimaanisha mtu kwa maana ya civil servant lakini sikuondoka maana ya mtu kwa any human being.

    Afisa utumishi nadhani hujaelewa haya mabadiliko. Kwanza nataka kukuambia japo yapo kwenye eneo lako kuita mabadiliko haya ni sera ni makosa. Haya ni mbadiliko ya sheria ya mwaka 2002 ya utumishi wa umma na sio sera ya utumishi.

    Nataka nitoe tatizo moja dogo lilokuwepo kwenye mfumo wa zamani kwa kutumia mfano wa bw. Michuzi. Chukulia Daily news wanataka mhariri mkuu wa picha. Michuzi mchukulie ni mhariri mkuu msaidizi. Nyie maafisa utumishi kwa vile kazi zenu haziinvolve kusafiri kama michuzi anaetakiwa kusafiri kucover matukio mnakuwa na hasira nae mnamnyima information ya kazi mpya. Mnaitangaza lakini yeye hammwambii ili asiombe kwa vile mna grudges nae za kiuchumi. Matokeo yake watu wengine wanaomba kazi bila bwana michuzi kujua na kuomba. Mnainterview na kupata mtu toka nje ambaye hajui kazi za daily news zinavyofanywa. Huyu jamaa analetwa pale na Michuzi ndie anamfundisha kazi. Unadhani utendaji wa Bw. Michuzi utakuwaje? Bw Michuzi sio kwamba hana uwezo alinyimwa information.

    Mimi sioni tatizo kabila la mabadiliko haya. Waziri kasema kama waliopo hawana sifa za kazi, kazi zitatangazwa na wa nje wataomba. Nadhani hivyo ndio ilivyokuwa before 2002 na utaratibu ulikuwa unafanya kazi vizuri tu..sasa hapa tatizo liko wapi.

    ReplyDelete
  16. Ndg. Anon wa Dec 4. 10:48
    Hapa si suala la mdaharo wala mashindano na mtu wala uandishi wa Tasnifu bali hoja za msingi ndio zitasimama.
    Nashukuru kwa kujaribu kunisahihisha kuwa si mabadiliko ya sera bali sheria. Ingawa kwa hakika Sheria hiyo namba 8 ya utumishi wa umma ya 2002 lazima itabadili sehemu ya sera, kanuni na hata taratibu za ajira (policy,regulations & procedures) kwa watumishi umma kwa ngazi ya Maafisa Waandamizi kutoka ilivyokuwa (ushindani wa wazi) kuwa ya ushindani wa ndani (usiowazi).
    Aidha mfano ulioutoa wa Michuzi na Daily News hakika hilo ni TATIZO MOJA DOGO kama wewe mwenyewe ulivyosema na wala kwa hilo kamwe sheria isingeweza kubadilishwa maana tayari sera, sheria, kanuni na taratibu za ajira zinasisitiza uwazi na haki. Hivyo wewe unajaribu kututolea hapa mfano wa ufisadi, uzembe na hata unyanyaswaji katika ofisi kitu ambacho hakihitaji mabadiliko ya sheria bali msisitizo wa watu kuajibika ipaswavyo na hatua kuchukuliwa kwa wakiukaji!
    Ebu fikiri tena ulipoongea habari za Mhabarishaji Mwandamizi kukosa kujua habari za tangazo la kazi sehemu yake ya kazi! Sihitaji kukufundisha maana nadhani unaelewa kuwa kama kweli kuna uajibikaji unaopaswa, tangazo la kazi hutolewa si tu katika notice board ya Daily News wakati Michuzi amesafiri. Tangazo linapaswa kuwa sehemu mbalimbali na katika vyombo vya habari mbalimbali hivyo anaweza kuliona katika mbao za matangazo katika ofisi zingine za umma popote alipo, katika gazeti la Serikali, magazeti mengine nchini na hata katika television n.k. Pili kuna muda wa kutosha ili kuwapa watu fursa sawa ya kuliona tangazo na kutuma maombi. Ni ufedhuli na ubinywaji wa haki kwa walio mbali na Dar matangazo yanapotolewa halafu imebaki wiki au wakati mwingine hata siku mbili kabla ya mstari mfu!
    Hitimisho:
    Endapo haki na fursa sawa itatolewa kwa MTU YEYOTE MTANZANIA na TARATIBU ZA AJIRA ZIKAFUATA VIGEZO VYA MWENYE SIFA ZAIDI, hatuna haja ya kukumbatia mabadiliko hayo ya sheria ambayo yanaleta ubaguzi usio na msingi!

    AFISA UTUMISHI MWANDAMIZI- ARUSHA

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...