NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE YA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA, BALOZI SEIF IDDI, AKIZUNGUMZA WAKATI WA MKUTANO WA BARAZA KUU LA 65 LA UMOJA WA MATAIFA ULIOFANYIKA MWISHONI MWA WIKI, MKUTANO HUO ULIPOKEA NA KUJADILI TAARIFA ZA MAHAKAMA ZA KIMATAIFA ZA MAUAJI YA KIMBARI YA RWANDA(ICTR) NA MAUAJI YA HALAIKI YA ILIYOKUWA YUGOSLAVIA YA ZAMANI (ICTY). KATIKA MKUTANO HUO PAMOJA NA MAMBO MENGINE NAIBU WAZIRI ALISISITIZA NIA NA UTAYARI WA TANZANIA WA KUHIFADHI NYARAKA NA KUMBUKMBUKU MUHIMU ZA MAHAKAMA HIYO BAADA YA KUMALIZA KAZI ZAKE.


NA MWANDISHI MAALUM

NEW YORK-Wakati Marais wa Mahakama za Kimataifa za Mauaji ya Kimbari nchini Rwanda(ICTR) na ile ya mauaji ya halaiki ya iliyokuwa Yugoslavia ya zamani (ICTY0, wakilalalamikia uhaba wa fedha na wataalamu. Tanzania imeiambia tena Umoja wa Mataifa kwamba inayo nia na uwezo wa kuhifadhi nyaraka na kumbumbuku za Mahakama ya kimataifa ya Rwanda.

“Kama tulijitolea kuikaribisha mahakama hiyo katika ardhi yetu, kama tulitoa ushirikiano wa hali na mali kwa mahakama hiyo, kama tulitimiza wajibu wetu wa kimataifa na kitaifa katika kufanikisha utendaji kazi wa mahakama hiyo, hapana shaka kwamba hata uwezo na raslimali za kuzihifadhi kumbukumbu hizo tunao”.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Seif Iddi, katika mkutano wa Baraza Kuu la 65 la Umoja wa Mataifa, lilipokutana mwishoni mwa wiki, kupokea na kujadili taarifa kuhusu utendaji kazi wa mahakama hizo mbili.

Naibu Waziri Seif Iddi, akaueleza mkutano huo, kwamba, wakati utendaji kazi wa mahakama ya kimataifa ya mauaji ya kimbari ya Rwanda, ikikaribia ukingoni mwa kukamilisha kazi zake, Tanzania imekuwa ikifuatilia kwa karibu sana maamuzi ya kikao cha kazi cha Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, kuhusu uhifadhi wa nyaraka na kumbukumbu muhimu za makahama hiyo.

“Na kwa sababu hiyo serikali ya Tanzania inaamini kuwa nyaraka nyeti zinazoihusu mahakama hiyo, lazima zitunzwe mahali salama, penye amani na mazingira ambayo yataruhusu na kutoa fursa kwa UN, mamlaka au mtu atakayeruhusiwa kuzipata nayaraka hizo bila ya vikwazo au pingamizi, wasi wasi wa usalama au tatizo la kisiasa” akasisitiza Naibu Waziri

Akaongeza “ Tanzania iko tayari kuendelea kuzihifadhi nyaraka hizo na kumbukumbu zote kwa moyo mmoja kama ambavyo tumekuwa katika kipindi chote tangu kuanza kazi kwa mahakama hiyo. Tunaamini kwa nguvu zote kwamba miundombinu imara ya kutunzia nyaraka na kumbumbu hizo muhimu kwa vizazi vijavyo tayari ipo”.

Akizungumzia utendaji kazi wa Mahakama hizo mbili, Naibu Waziri, amesema hapana shaka kwamba mahakama hizo zimefanya kazi nzuri na iliyotukuka nakwamba zinapaswa kupongezwa na kila mtu.

“ Ningepeda kutoa shukrani zangu kwa mahakama hizo kwa kuweza kuwafikisha mbele ya mkono wa sheria watuhumiwa wote. Lakini ninapenda kuunga mkono ombi lililotolewa na marais wa Mahakama hizo la kutaka nchi wanachama waendelee kutoa ushirikiano wa kuwafikisha mbele ya mkono wa sheria watuhumiwa walioko bado mafichoni”. akasema Balozi Seif Iddi

Na kuongeza “ Nikiizungumzia Tanzania, ninapenda niwahakikishie, waheshimiwa marais, kwamba serikali yangu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano siyo tu kwa ICTR bali hata kwa mahakama ya iliyokuwa Yugoslavia ya zamani (ICTY)pale itakapo bidi.

Akatumia fursa hiyo kuzitaka nchi nyingine kutoa ushirikiano kwa mahakama hizo na kuhakikisha kwamba watuhumiwa ambao wanasadikiwa kuwa wamo ndani ya nchi zao wanafikishwa kwenye mkono wa sheria.

Awali Marais wa Mahakama hizo wakiwasilisha taarifa zao wameliambia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba licha ya kazi kubwa na nzuri ambayo mahakama zao zimekuwa zikitekeleza hadi sasa, ukwasi wa fedha na wafanyakazi wenye uzoefu unarudisha nyuma utendaji kazi wa Mahakam hizo.

Jaji Dennis Byron, Rais wa Mahakama ya Rwanda akiwasilisha taarifa yake, amesema kuwa Mahakama hiyo imeendelea kupoteza wafanyakazi wenye uwezo na uzoefu mzuri ambao wamekuwa wakiondoa na kwenda kutafuta kazi zenye maslahi mazuri zaidi.

Akasema hadi sasa ICTR imekwisha kupotea wafanyakazi 167 kati ya Julai 2009 na Juni 2010. Na kuongeza kuwa licha cha changamoto zote hizo, mahakama hiyo iliyopo jijini Arusha Tanzania inaendelea na mchakato wa kukamilisha kesi zinazotakiwa kumalizika kabla ya mwaka 2011.

Kwa upande wake Jaji Patrick Robinson, Rais wa Mahakama ya Yugoslavia wa Zamani ( ICTY) naye amesema kuwa tatizo la kuondoka kwa wafanyakazi wenye uzoefu limeathiri pia mahakama yake. Na akauomba Umoja wa Mataifa kuzisaidia Mahakama hizo ili ziweze kukamilisha kazi zake.

Mahakama ya Kimataifa ya mauaji ya Kimbari ya Rwanda ( ICTR) ilianzishwa mwaka 1994 wakati ile ya Yugoslavia iliyoko The Hauge Uholanzi,ilianzishwa katika miaka ya 1990 baada vita vya Balkan.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Bongo msitake kutuletea aibu duniani.Tulizoshapata zinatosha.Mnajua kabisa kuwa jengo litakalohifadhi hizo nyaraka litachomwa moto.Tumeshaona majengo kibao yameunguzwa kuficha ubadhirifu.Nasaco,kitega uchumi,Bot ni mifano halisi.Hakuna uchunguzi uliofanywa zaidi ya maneno ya kila siku "Polisi wanachunguza chanzo cha moto" lakini hatupati matokeo au kusikia watu wakifikishwa mahakamani kisha gerezani.Sasa mnataka kujitwisha kazi nyingine.Najua Tz watapata mshiko kwa kuhifadhi nyaraka.Lakini kama tunavyojua bongo hakuna siri jengo litakalohifadhi hizo nyaraka litajulikana na kila mtu awe mkulima au mbwia unga.Naomba achieni wengine wale hizo pesa za ICC.
    *MICHUZI USIBANIE NI UKWELI MTUPU HUU.

    ReplyDelete
  2. Hata mimi nina wasi wasi maana kuna huyu mtu moja anaitwa Dr Slaa huyu yeye ana mashushushu kila sehemu sasa hayo mafaili ya watu itakuwa siri kweli? Si atayapata halafu aanze kusema mambo ya kesi za watu mitaani kwenye mikutano ya hadhara kisha tupate aibu? Afadhali hata yakiungua moto aibu yake sio kubwa kama yazagae mitaani kwenye magazeti.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...