Na Pascal Mayalla

Wakazi wa Eneo la Mbezi Juu, barabara ya Goba, kuanzia eneo la Samaki Wabichi, jijini Dar es Salaam, wameitaka serikali kuwa wazi, kuwashirikisha wananchi, na kuzingatia sheria, taratibu na kanuni, katika utekelezaji wake wa mipango mbalimbnali ya maendeleo, vinginevyo, watajenga chuki kwa wanachi kuichukia serikali yao na viongozi wake.

Wito huo umetolewa jana, katika mkutano wa hadhara wa wakazi hao, waliokutana kujadili tishio la kukumbwa na bomoa bomoa ya upanuzi wa Barabara ya Goba kwa kiwango cha lami, kuunganisha barabara ya Bagamoyo kuanzia eneo la Samaki Wabichi na kuunganishwa na Barabara ya Morogoro, eneo la Mbezi Mwisho.

Huku wakiongozewa na Mwenyekiti wa kikao hicho, Dr. Winfred Milinga, amesema wakazi hao, wanaishi kwa wasiwasi na roho juu, kufuatia tishio hilo la bomoa bomoa ambayo serikali kupitia wakala wa barabara, Tanroad, inaliendesha kinyemela kwa kuiarifu Serikali ya Mtaa kama taarifa bila ushirikishwaji wowote wa wananchi ambao ndio waathirika.

Dr. Milinga amesema tishio hilo limeanzia kwa Barua ya Tanroad yenye kumb. No. RM/TRD/DSM/R.90.1/Vol.II/23 ya tarehe 25/02/2010, toka kwa meneja wa TANROAD wa Mkoa, kwenda kwa Serikali ya Mtaa ukielezea mipaka mipya ya barabara hiyo ni Mita 22.5 toka katikati ya barabara, toka mita 5 zilizopo sasa, hali itakayopelekea bomoa bomoa kuzikumba nyumba zote zilizoko kando kando ya barabara hiyo.

Sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Bw. Nyabakari, imeeeleza nioa ya serikali kuifanyia matengenezo barabara hiyo ya Goba toka Mbezi Mwisho hadi Samaki Wabichi pamoja na kuweka mipaka kuonyesha mwisho wa hifadhi ya barabara ya mita 22.5 toka katikati ya barabara. “Lengo ni kutambua hifadhi ya barabara na kuwatahadharisha wananchi kutokujenga ndani ya hifadhi hiyo”. Ilisema sehemu ya barua hiyo.

Barua hiyo, ilifuatiwa na uvamizi wa maofisa wa Tanroad kuingia kimabavu kwenye nyumba za kando kando ya barabara na kusimika mawe (beacons) mapya umbali wa mita 22.5 toka katikati ya barabara, bila taarifa wala mashauriano yoyote na wakazi hao.

Dr. Milinga amefafanua zaidi kuwa kufuatia hali hiyo, amefanya mawasiliano na ofisa huyo wa Tanroad ambaye alikubali kuja kuwafafanulia wakazi hao, kitu kinachoendelea na walikubaliana afike siku ya Jumamosi, 19/03/111 Saa 4 asubuhi, hivyo wananchi wakakusanyika ili kupata ufafanuzi huo, lakini ofisa huyo hakutokea na wala hakutoa udhuru wowote.

Mkazi wa eneo hilo, Balozi Mstaafu, Fanuel Kuzilwa, (Mninukulu wa Ikulu Mstaafu), amesema kitendo cha serikali kuwaweka wananchi wake katika wasiwasi wa maisha yao, kunajenga chuki kwa wananchi hao kuichukia serikali yao na viongozi wake hivyo kutishia amani na utulivu wa taifa kwa ujumla.

Mkazi Mwingine, Balozi Mstaafu, Herman Martin Mkwizu, iliishauri serikali kwa vile hiyo sio barabara kuu, isilazimishe ubomoaji usio wa lazima, badala yake ikubali uwepo wa barabara nyembamba kama miji mingine na kutolea mfano Barabara ya Samora, Mji mkongwe wa Zanzibar, na hata miji mikubwa ya kimataifa kama Roma, Venis, Vatican, ina barabara nyembamba na serikali zimeyakubali matokeo hayo.

Mjumbe wa eneo hilo, Mzee Ali selemani, huku akizungumza kwa jazba, ameitaka serikali kuwaheshimu wananchi wake kwa kusisitiza “serikali ni wananchi ndio walioichagua iwaongoze, bila wananchi, hakuna serikali, sasa iweje serikali yao walioichagua kwa kura zao, ije iwatendee visivyo?!!.

Amesema yeye ameishi eneo hilo tangu mwaka 1948, leo watu wa Tanroad wanakuja na kutishia kuivunja nyumba yake bila maelezo yoyote au ufafanuzi wa fidia, aliuza kwa umri wake wa miaka zaidi ya 70, ataanzia wapi?!.

Mzee Jackson Msokwa, amesema kama serikali, itafuata sheria, taratibu na kanuni, zinazotawala utwaaji wa maeneo ya watu kwa ajili ya shughuli za maendeo, hakutatokeo migogoro yoyote, na kusisitiza hatua ya kwanza kabisa ni ushirikishwaji wa wananchi ndipo utekelezaji unafuata, kitendo cha serikali kuanza na utekelezaji bila ushirikishwaji, ndicho chanzo kikuu cha migogoro.

Kikao hicho kimeteua kamati ya Watu saba, wakiongozwa na Dr. Milinga, kufuatilia suala hilo serikali. Wajumbe wengine wa kamati hiyo ni Bw. Jamuhuri Ngelime, Balozi Fanuel Kuzilwa, Jacson Musokwa, Baalozi, Mkwizu, Bibi Rehema Kayuni na Bibi Mary Hamisi ambaye pia ni katibu wa kamati hiyo.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 6 mpaka sasa

  1. WAKABOMOE NA SEHEMU ZA BEACH NYUMBA ZIMEJENGWA KARIBU NA BEACHA ISIVYOTAKIWA.

    ReplyDelete
  2. Hawa watu inaonyesha kuwa wanamatatizo ya kisheria,kwa kuwa kama wana uhalali na maeneo yao na yamepimwa kisheria na kuwekewa mawe,hawana sababu ya kuwa na wasiwasi na tanroads kwa kuwa tanroads imepanua maeneo yake na wao sasa wamo ndani ya tanroads ni kwa vyovyote tanroads itawasiliana nao kisheria maana yake kufidiwa,lakini kama wanamiliki hiyo ardhi kienyeji halafu wanategemea serikali iwaonee huruma,hiyo haikubaliki,sheria zipo na ni wajibu wa kila mtu kufuata sheria za ardhi bila kujali hiyo serikali uliichagua au hukuichagua.kwa kifupi kama serikali ina haki iendelee na mipango yake ya maendeleao kwa wananchi na nyie wananchi mnao lalamika kama mnaona mna haki basi muende mahakamani.Bila kufuata sheria tusitegemee maendeleo.

    ReplyDelete
  3. Wewe mtoa maoni wa 10:44 pm, sijui kama unelewa au kujua unachoongea. Ni bora ukakaa kimya na kusoma maoni ya watu wengine au uulize na ueleweshwe ndipo utoe maoni.
    Inasikitisha kuona kuwa serikali haiko wazi kwa wananchi na inataka kuwahujumu. Wananchi wamekuja kwa utaratibu mzuri na Tanroad haitaki kushirikiana nao kwa nini??? Hili tatizo liko muda mrefu na linaeleweka, tungeomba lifafanuliwe na wananchi waeleweshwe kabla na bila ya kutumia nguvu.

    ReplyDelete
  4. Mangufuli na TANROADS yake kwisha habari,miguu juu sa hizi naweza janga hata kwente round about ya pale Ubungo!Kidumu chama cha Mapinduzi kwa kutujali raia wake.

    ReplyDelete
  5. sasa kweli mmemwondolea wembe magufuli naaniii atasafisha barabara za walalahoiii, kweli magufuli wewe mziki mnene sasa acha kazi kapumzike jobag SA uangalie mabarabara 120kph ukienda slow utakamatwa mkeka hawakutaki magufuli usijigonge kapumzike tunakupenda tuko na wewe knehe. achana nao barabara za juu watazisikia mbaka waende mbinguni, mi ntajenga pale mbagala rangi tatu pananifaa sana panawateja wa maji.
    NATHANI KATIKA BOMOA BOMOA KUNA NYUMBA ZA MABEST WAO
    ILA KWANINI WAJENGE BARABARANI SHERIA SI IPOHATUTAKI MADINI TUNATAKA BARABARA, MZEE UNAHARIBU WATAKUSIFU KWA KUMRUHUSU BABU WA ROLIONDO USIPOANGALIA.

    ReplyDelete
  6. Mi nashangaa kweli tunalilia barabara na wakati maardhi yamejaa huko chanika, kisarawe, mlandizi. Hii yote ni kwa sababu kila mtu anataka kujenga kaframe mbele ya nyumba yake kwa hiyo barabarani wanaona dili.

    Tubadilike watz tupende maendeleo ya nchi yetu na mazingira pia., tuondoe ubinafsi. utakuta mtu kwenye daladala anakula muwa ganda anatupia barabarani ukimuuliza pale kuna jalala jibu hana. Change begin wit u.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...