Baadhi ya mifuko ya sukari iliyokamatwa ikiwa imehifadhiwa katika ghala la Polisi kituo cha Polisi Himo Mkoani Kilimanjaro.

01.  Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mh Lazaro Nyalandu( Kulia), Mbunge wa Vunjo Mh Augustine Mrema ( Katikati) na Mkuu wa Wilaya ya Moshi Mussa Samisi wakizungumza na vyombo vya Habari mara baada ya kutazama sukari iliyokamatwa katika maeneo ya mipakani  Mkoani Kilimanjaro.

 01.  Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mh Lazaro Nyalandu( Kushoto), akijibu hoja mbali mbali za Mbunge wa Vunjo Mh Augustino Mrema (Kulia) alipokuwa katika ziara yake ya kutembelea Masoko na vituo vya biashara mipakani kastika Mkoa wa Kilimanjaro. Wanaoshuhudia ni viongozi na watendaji wa Mamlaka mbali mbali katika Mji Mdogo wa Himo.

01.  Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mh Lazaro Nyalandu akitoa maagizo kwa watendaji wa mamlaka mbali  za serikali katika Mji mdogo wa Himo mara baada ya kukamilisha ziara yake ya kutembelea na kukagua masoko na vituo vya Biashara mipakani katika Mkoa wa Kilimanjaro.

Kufuatia operesheni kabambe  ya nchi nzima  kukamata sukari inayosafirishwa nje ya nchi, Jeshi la polisi Mkoa wa Kilimanjaro kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato nchini TRA, wamefanikiwa kukamata mifuko 2100 ya sukari iliyokuwa ikivushwa mpaka kupelekwa nchi  jirani ya Kenya.

Kiasi hicho kikubwa cha sukari kimekamatwa katika maeneo mbali mbali ya mpaka wa Tanzania na Kenya na kuhifadhiwa katika ghala la polisi kituo cha Himo, ikiwa ni mwendelezo utekelezaji wa agizo la  Waziri Mkuu Mh  Mizengo Pinda aliezitaka Mamlaka zote za ulinzi na Usalama nchini kuhakikisha kuwa, bidhaa hiyo haivuki mipaka ya ili kukabiliana na uhaba mkubwa wa bidhaa hiyo hapa nchini.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mh Lazaro Nyalandu akiwa katika ziara ya kutembelea masoko na vituo vya biashara mipakani, amefika katika eneo la Himo na kushuhudia kiasi hicho kikubwa cha sukari  huku Mbunge wa Jimbo la Vunjo Mh Augustino Lyatonga Mrema akiiomba serikali kutoa agizo la kuzitaka Mamlaka husika kuwauzia wananchi bidhaa hiyo mara moja bila kusubiri taratibu zinazotumia muda mrefu huku wananchi wakiendelea kuteseka kwa kukosa bidhaa hiyo muhimu.

Ziara ya ghafla ya Viongozi hao ilivutia umati mkubwa wa wananchi na wafanyabiashara wa maeneo ya Himo na Holili hali iliyolawalazimu viongozi hao kuzungumza na wananchi. Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mh Lazaro Nyalandu, akalipongeza Jeshi la Polisi na Mamlaka za Usalama katika Miji ya Mpakani ya Himo na Holili kwa jitihada kubwa ya kupambana na biashara za magendo katika eneo hilo.

“Kazi mnayofanya hapa ni nzuri sana na ya kupigiwa mfano katika maeneo mengine  nchini. Wananchi wanateseka kwa kukosa sukari, agizo halali la serikali lililopiga marufuku biashara hii linakiukwa kwa makusudi, hatuwezi kuvumilia tabia hii iendelee, watu wachache wasio na utu waendelee kuneemeka huku wananchi walio wengi wakitaabika. Pamoja na uchache wa askari na uhaba wa vitendea kazi, ninaomba msilale, shirikianeni na wananchi, nendeni kila kona, zuieni njia zote haramu zinazotumika kupitisha magendo.”

Kwa upande wake Mbunge wa Vunjo Mh Augustino Mrema amesema, uhaba wa sukari nchini unatokana na bei nzuri ya bidhaa hiyo katika nchi za jirani hali inayowavutia wafanyabiashara wenye tamaa kupeleka bidhaa hiyo katika nchi za Kenya na Uganda.

“ Sukari ya Tanzania inauzwa nchini Kenya kwa bei mara mbili zaidi ya hapa nchini. Miji yetu ya mipakani ina njia za panya lukuki huku vyombo vyetu vya ulinzi na usala vikiwa na watendaji wachachache na vitendea kazi duni. Ninaiomba serikali kuzipa uwezo mamlaka zake ili ziweze kufanya kazi kwa ufanisi, ninaomba pia sukari ilioyokamatwa iuzwe mara moja kwa wananchi na askari au raia walifanikisha kukamatwa kwa bidhaa hizi wapewe motisha ya asilimia kumi ya kile walichokamata. Tukifanya hivi, biashara zote za magendo mipakani zitakoma.”

Naye Mkuu wa Wilaya ya Moshi Mussa Samizi aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, ameahidi kuongeza nguvu katika operesheni hiyo na kuwaomba wananchi kuvisaidia vyombo vya dola katika zoezi hilo kwa kutoa taarifa sahihi mara wanapoona vitendo hivyo vya kuvusha sukari na bidhaa nyingine hasa kastika njia za panya ambazo haziwezi kufikiwa na vyombo vya dola kwa urahisi.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mh Lazaro Nyalandu, amewata Watanzania kushindana kikamilifu na majirani zetu katika kutumia vyema fursa za kibiashara zilizoko katika maeneo ya mipaka ya nchi yetu na nchi jirani.
Akizungumza na Viongozi na watendaji mbali mbali wa serikali wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mh Nyalandu amesema hadi sasa, ni watanzania wachache sana wanaofanya biashara zenye tija katika masoko na vituo vya biashara mipakani.

“Masoko yetu yamejaa bidhaa za wageni kwa zaidi ya asilimia 70 huku sisi tukiambulia asilimia 30 na bidhaa zetu tunazowauzia nyingi ni bidhaa ghafi, baada ya muda mfupi wenzetu wanaziongeza thamani na kutuuzia tena kwa bei ya juu. Lazima tuchukue hatua, tufanye kama wao, tuwapelekee bidhaa mpaka nchini mwao, tujenge masoko na mifumo thabiti itakayowavutia kuja nchini na kufanya biashara ki halali, nchi ipate kodi, wao wafaidike na sisi tufaidike pia.”

Ziara ya Mh Nyalandu kutembelea masoko na vituo vya biashara mipakani ilianzia katika Mpaka wa Tanzania na Kenya katika Mji wa Namanga ikiwa na lengo la kutembelea maeneo hayo kote nchini. Baada ya kutembelea vituo vya Himo na Holili, msafara wa Naibu Waziri utatembelea kituo cha Horohoro Mkoani Tanga kabla ya kuhamia kanda ya Ziwa.
Imetolewa na
Kitengo cha Habari na Mawasiliano,
Wizara ya Viwanda na Biashara.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...