Aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumisha na Utawala wa BOT, Amatus Liyumba akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo huku akikabiliwa na shitaka jipya la kukutwa na  simu ya mkononi akiwa gerezani. (Picha na Francis Dande).
 Aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumisha na Utawala wa BOT, Amatus Liyumba akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo.
Liumba akirudishwa Rumande.

Na Ripota Wetu.

ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu akikabiliwa na kosa la kukutwa na simu ya mkononi gerezani.

Liyumba (63) anatumikia kifungo cha miaka miwili katika gereza la Ukonga, baada ya kupatikana na hatia ya kosa la matumizi mabaya ya ofisi ya Umma.

Akisomewa shitaka hilo jana mahakamani hapo na Wakili wa Serikali Elizabeth Kaganda, mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Stuart Sanga, alidai kuwa Julai 27, mwaka huu katika gereza la Ukonga, mtuhumiwa alikutwa na simu aina ya Nokia 1280, ya rangi nyeusi yenye namba 0653004662 kinyume cha sheria ya wafungwa namba 86.

Baada ya kusomewa shitaka hilo yalizuka mabishano ya kisheria baina ya upande wa mashitaka na upande wa utetezi, ambapo upande wa utetezi ukiwakilishwa na Majura Magafu alidai kuwa katika hati ya mashitaka sheria namba 86 ya sheria ya wafungwa kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, haionyeshi kwamba upande wa mashitaka unamshitaki mshitakiwa kwa kifungu gani.

“Ili mshitakiwa aweze kujibu kama ana kosa au la inapaswa makosa yawe yanaeleweka kwamba anatuhumiwa chini ya kifungu gani, tunaomba upande wa mashitaka kufanya marekebisho ambayo yanaweza kurekebishwa hata kwa mkono kwamba wanamshitaki katika kifungu gani cha sheria hiyo,” alidai Magafu.

Akipangua hoja hiyo Wakili Kaganda aliiomba Mahakama itambue kuwa mshitakiwa anashitakiwa kwa kosa la kukutwa na kitu kisichoruhusiwa gerezani.

Wakili Magafu alidai kuwa mashitaka hayo yana dosari hivyo upande wa utetezi hauwezi kumruhusu mteja wao kusema ndio au hapana kwa makosa aliyosomewa, hivyo aliiomba Mahakama kuifuta ili upande wa mashitaka ukaifanyie marekebisho hati hiyo.

“Kifungu cha 86 kina sehemu tatu, ya kwanza inatambulisha kukutwa na kitu kinachokatazwa na Magereza lakini haisemi kosa, ya pili na ya tatu inakataza tu lakini pia inatoa kwa Ofisa wa Magereza kuweza kuiharibu hiyo mali,” alidai Magafu.

Akitoa uamuzi wa Mahakama, Hakimu Sanga alikubaliana na upande wa utetezi ambapo aliutaka upande wa mashitaka kuifanyia marekebisho hati hiyo ya mashitaka na kuahirisha shauri hilo kwa muda ili kutoa nafasi kwa upande wa mashitaka kufanya marekebisho.

Baada ya kufanya marekebisho Mahakama ilirudi tena ambapo Wakili Kaganda alidai kuwa kwa mujibu wa amri ya Mahakama ya kuifanyia marekebisho hati ya mashitaka, upande wa mashitaka umefanya hivyo kwa kutumia sheria ya mwenendo wa makosa ya jina namba 234 ( 1) na (2) na kumsomea upya mshitakiwa shitaka lake ambalo alilikana, na kuiomba Mahakama kuwapangia tarehe nyingine ya kutajwa kwa shauri hilo kwa kuwa upelelezi haujakamilika.

Wakili Magafu kwamba kwa kuwa mshitakiwa anatumikia adhabu ya kifungo ambacho anamaliza Septemba 28, mwaka huu, aliiomba Mahakama kumpatia dhamana, ikitokea kwamba ametoka jela aendelee kuwa chini ya dhamana katika kesi hii.

Hakimu Sanga alisema sheria hairuhusu mtu anayetumikia kifungo kupata dhamana, lakini kwa kuwa kesi hii ni mpya Mahakama inaweza kutoa dhamana.

“kwa minajili ya kesi hii, dhamana iko wazi kwa mshitakiwa kwa kusaini hati ya dhamana ya Sh 50,000 na mdhamini mmoja ambaye anafanya kazi katika sehemu inayotambulika,” alisema Hakimu Sanga.

Mshitakiwa alipata dhamana jana hiyo hiyo na kesi iliahirishwa mpaka Septemba 29, mwaka huu itakapotajwa tena.

Mei 24, mwaka 2010 Liyumba alihukumiwa kwenda jela miaka miwili na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, na Mei 28 kupitia ya mawakili Majura Magafu na Hudson Ndusyepo, Liyumba alikata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam akitoa sababu 12 za kupinga hukumu hiyo pamoja na adhabu.

Hata hivyo, Desemba 21, 2010, Mahakama Kuu ilitupilia mbali rufaa yake na kukubaliana na hukumu iliyotolewa Mahakama ya Kisutu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 9 mpaka sasa

  1. Huyu Baba anaweza kufa kwa presha ya mlolongo wa matatizo anayopewa akiwa kama MBUZI WA KAFARA kuwalinda wazito waliohusika kuhujumu mabilioni ya pase za walalahoi... Bongo kweli Tambalale!

    ReplyDelete
  2. huyu si mfungwa jamani,mbona hana sare za wafungwa

    ReplyDelete
  3. Jamani Hii Nchi, haki ipo wapi? Kama mtu umekamatwa na kitu kisichokubaliwa Gerezani na hususan simu ambayo inahitaji kuchajiwa kila siku; kwa nini Mkuu wa Gereza asiwajibishwe? Au ndio nchi ya KISASI? Watu wana mambo/chuki zao binafsi wanabambikiana makesi. Je! Huyo aliyepigiwa simu mpaka akamwekea Mtego wa Maafisa Usalama anaweza akatuambia Jamaa alizungumza naye kitu gani? mpaka akakasirika na kumwekea mtego? Katika hili, tunajenga Taifa ama tunatafuta Chuki kutoka kwa Jamaa wa huyo Liumba? Maana ukweli siku moja utakuja kudhihirika na tukashindwa pa kuficha sura zetu.

    Mdau.

    ReplyDelete
  4. Ndugu Michuzi mi naomba kueleweshwa juu ya nguo au mavazi ya ndugu Liumba.Ninavofahamu mimi Liumba anatumikia kifungo cha miaka 2 kwa sasa!! Na je mtu anapokuwa anatumikia kifungo akipatikana na kesi na akatakiwa kupelekwa mahakamani anavaa nguo za kiraia???? Au siku hizi wafungwa hawavai uniform kama zamani??? Naomba jibu wadau maana sijaelewa!!! AU HIZI PICHA ZINAZOTOLEWA NI ZA WAKATI ULIOPITA???

    Mdau , Norway.

    ReplyDelete
  5. Sasa kama alifungwa kuanzia tarehe 24 May 2010 mpaka tarehe 28 Sept 2011 miaka miwili itakuwa imeisha? au ndiyo kuhesabia siku mchana na usiku?

    ReplyDelete
  6. kuwa na simu siyo big issue kama inavyodhaniwa, hii yote ni kudhalilisha tu mtu wa watu. mugeweza kumnyang'anya tu na mambo yakaisha.

    ReplyDelete
  7. Mbona hatujasikia wale wanauza bangi gerezani wakiletwa kisutu? Je, waliokuwa wakimuuzia vocha wako wapi? Hapo Ukonga wafungwa wenyewe simu ni Liyumba pekee au?

    ReplyDelete
  8. mafisadi wapo weeengi na wapo huru ni huyu tu ndiye mmemsweka ndani ni bora naye abaki huru tujue moja hata hainogi.

    ReplyDelete
  9. makosa kama hayo yanayotokea ndani ya magereza kwanini wasiyamalize kwa kutumia kamati za nidhamu ndani ya hayo magereza kuliko kuja mahakamani kutupotezea muda wakati mahakama na mahakimu wenyewe ni wachache...mambo mengine jinsi wanavyoamua utajua tuu hata wakuu wenyewe wa magereza ni wababishaji tuu na sheria zao hazisaidii yeyote zaidi ya kupoteza mudatuu nna resources za maana,kwa mtoni hapo unaitwa mbele ya kamati ya nidhamu unapewa onyo ukirudia unaongezewa mwezi mzima au unakuwa isolated na kunyimwa privilledged fulani wanazopata wafungwa wenzako

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...