Kutokana na ongezeko la mvua zinazoendelea katika maeneo mengi nchini Mamlaka ya Hali ya Hewa inatoa taarifa ya mwelekeo wa mvua hizo katika kipindi cha siku kumi zijazo kuelekea mwaka mpya 2012.


Mifumo ya hali ya hewa inaonyesha kuimarika kwa hali ya joto la Bahari ya Hindi, sambamba na kuongezeka kwa msukumo wa hewa yenye unyevunyevu kutoka misitu ya Kongo na kusababisha makutano ya upepo katika eneo la mashariki na kusini magharibi mwa nchi. 



Hali hii inatarajiwa kuendelea kusababisha vipindi vya mvua kubwa katika maeneo ya Mikoa ya Pwani ya kasikazini (Morogoro, Pwani, Dar es Salaam, Tanga na kisiwa cha Unguja) hadi tarehe 22 Disemba 2011. Mvua hizo zinatarajiwa kurejea katika hali ya kawaida kuanzia tarehe 23 Disemba katika maeneo hayo.



Aidha maeneo ya mikoa ya nyanda za juu kusini magharibi( Mikoa ya Mbeya, Iringa na Sumbawanga), kanda ya kati (Mikoa ya Dodoma na Singida) na magharibi mwa nchi (Mikoa ya Kigoma na Tabora) yanatarajiwa kuendelea kuwa na mvua katika kiwango cha juu ya wastani pamoja na vipindi vya mvua kubwa. Hali hii inakwenda sambamba na utabiri wa mvua za Vuli na za Msimu ambapo maeneo mengi ya nchi yalitarajiwa kuwa na mvua juu ya wastani na vipindi vya mvua kubwa.



Kulingana na viwango vya mvua zilizonyesha katika kipindi kifupi ongezeko kidogo la mvua katika maeneo hayo linatarajiwa kuendelea kusababisha mafuriko na uharibifu wa miundombinu. Mamlaka inashauri tahadhari stahiki ziendelee kuzingatiwa.



Maeno mengine ya nchi yanatarajiwa kupata mvua za kawaida katika kipindi hicho. Aidha mwelekeo wa mvua katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari 2012 utatolewa mwishoni mwa mwezi huu.



Mamlaka ya Hali ya Hewa inaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya Hali ya hewa na athari zake na itaendelea kutoa taarifa na tahadhari kila inapobidi.



Dk. Agnes L. Kijazi
MKURUGENZI MKUU
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. Serikali inapaswa kuiwezesha idara hii ya hali ya hewa kwani vifaa vyake bado ni vya kizamani.Walitakiwa waione hali hii wiki kabla ya kutokea

    ReplyDelete
  2. walishasema kwa kina, tatizo huwa hatuthamini wataalam wetu, tunasubiri wageni waseme ndiyo tunachukua hatua.

    hapa wa kulaumiwa siyo TMA.njia nzuri ya kuuliza ingekuwa tumekosea wapi? siyo kutupa lawama moja kwa moja bila uhakika.

    ReplyDelete
  3. Inatubidi sasa watanzania tuwe na mazoea ya kuangalia vipindi vya utabili wa hari ya hewa tulio wengi huwa tunapuuzia.Ombi pia kwa vyombo vya habari msisubili mpaka saa mbili tena baada ya taarifa ya habari tuinge wezetu wanavyofanya kuiga sio zambi.Redio ndo hata amna kabisa vipindi vya utabili wa hali ya hewa.

    ReplyDelete
  4. Kuepuka na Gharama za baadae ni bora Serikali ikatoa nauli kwa wananchi wake waamie Kwenye maeneo ya miinuko.Haswa kwa wale wenye ndugu ama marafiki kuchukuwa hatuwa hiyo wenyewe mapemaa .
    Gharama za maombolezo ni nyingi kuliko za kutatuwa tatizo.
    Kingine ni Serikali kuchukuwa hatuwa za Haraka kuhusu ujenzi na uendelezaji wa mabonde yaliyopo Jijini Dar es salaam.
    Maeneo ya mambonde ya Dar es salaam ni kivutio kikubwa na yangeweza kuwezesha serikali kupata kipato cha utalii kama yangetengenezwa inavyotakiwa.
    Tupunguze hivyo vikao vya kuzungumzia jambo huku watu wanalipwa bure bila ya kutekeleza Majukumu ni syle ya kizamani sanaa.Kila mtu anajuwa maendeleo ya Tz yapo kwenye siasa sana bila ya kuchukuwa hatuwa ambazo ndiyo ukweli.
    Poleni sana na janga
    Mungu ametupa Akili na Utashi ,tutumie

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...