Salamu bwana Michuzi, mkuu wa libeneke,
Leo nina beti hizi, nakuomba uziweke,
Japo mimi si mjuzi, beti zina ladha yake,
Enyi watu wa Takwimu, dini nayo iwekeni!

Naongelea hesabu, za watu pia makazi,
Dini kwetu si aibu, wala si Jinamizi!
Hivi ipi ni sababu, dini hatuweki wazi?
Enyi watu wa Takwimu, dini nayo iwekeni!

Watu mwawahamasisha, ‘mhesabiwe jamani’,
Dini wakiwakumbusha, hiyo ‘noma nyamazeni’,
Acheni kunichekesha, hayo mambo ya zamani,
Enyi watu wa Takwimu, dini nayo iwekeni!

Dini jambo la dhahiri, kamwe haijawa siri,
Msianze kukariri, eti hili ni hatari,
Kwetu ndio utajiri, hata ziwe utitiri,
Enyi watu wa Takwimu, dini nayo iwekeni!

Mnapo apa bungeni, nyote mwahusisha dini,
Mwavishika mikononi, vitabu vyenu vya dini,
Hivi hamuoni soni, takwimu kuwa kapuni?
Enyi watu wa Takwimu, dini nayo iwekeni!

‘Steti dipatimenti’, ya watu wa Marekani,
Imeandaa tovuti, dini zetu zimo ndani,
Hapa picha siipati, sisi ni ‘mahayawani’?
Enyi watu wa Takwimu, dini nayo iwekeni!

Wazawa hatujijui, tuko wangapi kidini,
Ukihoji ni jinai, waweza nyea debeni,
Takwimu hamtufai, data ziko Marekani?!,
Enyi watu wa Takwimu, dini nayo iwekeni!

Nchi yetu kweli noma, data za dini hatuna!,
Lakini bwana Obama, kazianika bayana,
Hii sasa ni hujuma, wapi zimepatikana?,
Enyi watu wa Takwimu, dini nayo iwekeni!

‘Dini yavunja amani’, asema bwana Wasira,
Mimi hii siamini, huyu babu hana sera,
Pengine hajiamini, au kaleta hasira,
Enyi watu wa Takwimu, dini nayo iwekeni!

Takwimu za kitaifa, zina hadhi ugenini,
Ziwe sahihi kisifa, tuzijue hadharani,
Vinginevyo ni kashifa, takwimu hazilingani,
Enyi watu wa Takwimu, dini nayo iwekeni
Serikali naisihi, jukumu kutolikacha,
Kutoa ‘figa’ sahihi, bora kuliko kuacha,
Sio kutoa kebehi, mtamuudhi Kundecha,
Enyi watu wa Takwimu, dini nayo iwekeni!

Kama dini mwaipinga, muundae waraka,
Kuzikataza runinga, tovuti na vibaraka,
Visianzishe ushenga, kutangaza matabaka
Enyi watu wa Takwimu, dini nayo iwekeni!

Mashekhe na maimamu, nanyi ninawashauri,
Msigomee takwimu, hata walete jeuri,
Shirikini kwa nidhamu, pengine kwenu ni kheri,
Enyi watu wa Takwimu, dini nayo iwekeni!

Wagomaji ni wachache, wengine watashiriki,
Hapo mtapanda mche, wa chuki na unafiki,
Kumbe hawa ni wachache, hata robo hawafiki?!
Enyi watu wa Takwimu, dini nayo iwekeni!

Shairi namalizia, msije mkasinzia,
Amani naitakia, nchi yangu Tanzania,
Pinda wito itikia, sema watakusikia!
Enyi watu wa Takwimu, dini nayo iwekeni!
  
Mwamgongo,
Mwenyeji wa Tanga.
16 Juni 2012 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 12 mpaka sasa

  1. AnonymousJune 18, 2012

    Shairi hili ni zuri na ujumbe umefika
    Mtungaji ni mahiri wala hakukurupuka
    Ni vyema kutafakari haya aliotamka
    Hivyo nami nashauri dini nayo kuiweka

    ReplyDelete
  2. Japo siujuwi mwanzo, hili suala yakini,
    Mepitia maelezo, loyanena hadharani,
    Mazuri yako mawazo, DINI tiwa hesabuni,
    Hata wasokuwa nazo, Takwimu yao wekeni.

    Ni mtu uhuru wake, chaguwa cha kuamini,
    Tena kwa ridhaa yake, huwa ya mtu imani,
    Ziweka Takwimu zake, ubaya wake sioni,
    Nojuwa athari zake, basi bayana semeni.

    Kama hilo mwalikwepa, na bungeni lifuteni,
    Kwa "Misakhafu" noapa, "Biblia" mikononi,
    Hilo katu liogopa, noahidi hatuoni,
    Kama MOLA mwaogopa, kitabuche heshimuni!

    ReplyDelete
  3. AnonymousJune 18, 2012

    Mshairi wetu,
    Suala la nini kiwekwe kwenye sensa siyo la watu wa Takwimu bali ni sera ya serikali. Kuwapigia kelele hawa ni sawa na kumpigia kelele dereva kwa tatizo la uundwaji wa gari. Mueleze Rais wa nchi na serikali yake ili Baraza la Mawaziri lijadili na kupitisha ama kukataa.

    Salamu zao.

    ReplyDelete
  4. AnonymousJune 18, 2012

    Kaka/dada mwamgongo labda mimi nikuulize kwanini hasa ww unataka takwimu za dini ziwekwe ?ni kweli unataka tu kujua idadi ya waislam na wakristu au kuna lengine?unajua kunamsemo unasema "never try to win an argument" kwasaabu hakuna furaha ndani ya ushindi wa mabishano ikionekana leo labda waislam ni wengi ndugu wakristu hawatafurahi na ikionekana pia wakristu ni wengi waislam hawatofurai kadhalika sasa sijui kwa kweli watu wanatafuta nini katika hili

    ReplyDelete
  5. AnonymousJune 18, 2012

    Ewe mshairi,
    hoja yako naikubali,
    si kwa nia mbaya,
    bali kwa minajili,
    ya kumaliza ubishi.

    ReplyDelete
  6. AnonymousJune 18, 2012

    Nimefurahishwa kwa ujumbe uliosheheni shairi lako bwana Mwamgongo,nadhani ni wakati mwafaka kwa maono kama yako kwa kupitia tungo zako.

    ReplyDelete
  7. AnonymousJune 18, 2012

    Shairi zuri lakini halijasema madhara ya kuacha sensa au uzuri wa sensa ya dini.

    limehimiza tuu.

    ReplyDelete
  8. AnonymousJune 18, 2012

    Safi sana Bwana Mwamgongo,siku hizi kupata vionjo kama hivi nadra sana.

    ReplyDelete
  9. AnonymousJune 18, 2012

    Du Ndugu Mwamgongo..! Nikupongeze kwa utunzi mahiri wa shairi. Mimi ni mpenzi sana wa Fasihi yakiwemo na mashairi pia.
    Nina mawazo taofauti na wewe katika ujumbe uliomo ndani ya tungo zako. Mimi sidhani kama kuna umuhimu woowte kwa watu wa Takwimu kutuhesabu Watanzania kwa dini zetu.Ili itusaidie nini? Kwa mfano tukishajua wapagani ni 12 % itakuwa na mahusiano yapi katika kupanga bajeti ya nchi au kuleta maendeleo nchini?
    Katiba ya sasa ya nchi hii inaoneshakuwa Tanzania ni nchi isiyokuwa ya kidini, kila mtu ana uhuru wa kuabudu dini au dhehebu atakalo ili mradi tu asiwe anavunja sheria. Kwa hivyo katiba kutoa uhuru huo mimi nadhani ilikuwa na lengo la kutambua na kuheshimu dini mbalimbali zilizopo, ila kutoziweka katika muundo wa serikali wala ni kwa sababu haikuwa ana dini, japo watu wake wana dini zao.
    Ujenzi wa Tanzania unategemea misingi ya umoja wa watu wake bila kujali dini zao. We unafikili tukijua takwimu za dini zitatusaidia nini? Sisi si wamarekani..! wao wanasababu zao za kutafuta muundo wa jamii fulani kwa dini zao. Sisi tunataka kujua takwimu za dini zetu ili iweje.
    Si tunajuana kuwa nani anakwenda msikitini, nani kanisani na nani haendi popote! Kwani hili nalo lazima tuliweke kwenye takwimu. Mi nadhani hii ni kazi ya makasisi na mashehe kujua waumimi wao wako wangapi. Ila ni kazi ya serikali kujua Watanzania wako wangapi.
    Mwisho nikushukuru na kukupongeza kwa utunzi mzuri wa shairi, japo siafiki hoja yako.
    Naitwa Msuke Mtoka

    ReplyDelete
  10. Che GuevaraJune 18, 2012

    pelekeni UDINI wenu huko ndio maana hamuendelei kila kukicha majungu tu na migogogro isiyo na kichwa wala miguu

    ReplyDelete
  11. AnonymousJune 18, 2012

    Kama nchi hii haina dini kinachotaka watu kuapa bungeni ni nini? au kuapa kwa kutumia vitabu vya dini maana yake nini? Kwa nini wasiape kwa katiba tu au wasiape kabisa, kinachotaka kila kitu tuombe tunamuomba nani.
    Kwa nini walemavu wahesabiwe.......na takwimu zao ziwepo kwani wao sio watanzania, kwani wao si binadamu? Na watu wanakazana kusema kuhesabiwa kwa misingi ya dini ni udini, udini maana yake ni nini? Kubaguliwa kwa sababu ya dini kupo, na inajulikana hii sio siri hatutaki tu kukubali lakini ipo.
    Ikanushwe hadharani kuwa waislam si asilimia 35 tu kwa vile takwimu ni za kizushi hizo zilizopo kwenye mitandao, tena cha kushangaza zimetolewa na taasis za dini ya kikristo, vinginevyo basi tuhesabiwe, ukweli ujulikane.
    Na sababu zipo, upendeleo unatolewa kwa shughuli mbali mbali za makanisa ikiwa pamoja na makubaliano baina ya makanisa na serikali, kisingizio ilikuwa hizo takwimu zakizushi, kuwa wao ni wengi, kwani tatizo likowapi si kuandika tu. Nauliza tena mbona kwenye CV wanandika dini yao na makanisa wanayo sali...........kipingele hichi basi kifutwe kila mahali na mtu akikiandika pahala popote iwe kosa la jinai.....na kupiga nyimbo za dini yoyote mitaani, maofisini, iwe ya serikali au binafsi iwe marufuku kwa vile inaendeleza udini, vile vile wakati wa chrimas marufuku kuweka marembo yao kila mahali........mbona wakati wa Nyerere havikuepo hivii......ina maana alikuwa haheshimu ukristo.......sasa kilicho zidi hapa nini? Tusiwe ndumilakuwili, wewe Che Guevara kama unataka kuwa mpagani hiari yako, haya ya udini tuachie sisi wenye dini zetu.

    ReplyDelete
  12. AnonymousJune 18, 2012

    We Che Guevara kama wewe mkomunisti sisi tuna dini zetu, na mdini ni mtu mwenye dini, kama ulivyo wewe mchaga mtu uliotoka uchagani.
    Kama nchi hii haina dini kinachotaka watu kuapa bungeni ni nini? au kuapa kwa kutumia vitabu vya dini maana yake nini? Kwa nini wasiape kwa katiba tu au wasiape kabisa, kinachotaka kila kitu tuombe tunamuomba nani.
    Kwa nini walemavu wahesabiwe.......na takwimu zao ziwepo kwani wao sio watanzania, kwani wao si binadamu? Na watu wanakazana kusema kuhesabiwa kwa misingi ya dini ni udini, udini maana yake ni nini? Kubaguliwa kwa sababu ya dini kupo, na inajulikana hii sio siri hatutaki tu kukubali lakini ipo.
    Ikanushwe hadharani kuwa waislam si asilimia 35 tu kwa vile takwimu ni za kizushi hizo zilizopo kwenye mitandao, tena cha kushangaza zimetolewa na taasis za dini ya kikristo, vinginevyo basi tuhesabiwe, ukweli ujulikane.
    Na sababu zipo, upendeleo unatolewa kwa shughuli mbali mbali za makanisa ikiwa pamoja na makubaliano baina ya makanisa na serikali, kisingizio ilikuwa hizo takwimu zakizushi, kuwa wao ni wengi, kwani tatizo likowapi si kuandika tu. Nauliza tena mbona kwenye CV wanandika dini yao na makanisa wanayo sali...........kipingele hichi basi kifutwe kila mahali na mtu akikiandika pahala popote iwe kosa la jinai.....na kupiga nyimbo za dini yoyote mitaani, maofisini, iwe ya serikali au binafsi iwe marufuku kwa vile inaendeleza udini, vile vile wakati wa chrimas marufuku kuweka marembo yao kila mahali........mbona wakati wa Nyerere havikuepo hivii......ina maana alikuwa haheshimu ukristo.......sasa kilicho zidi hapa nini? Tusiwe ndumilakuwili, wewe Che Guevara kama unataka kuwa mpagani hiari yako haya ya udini tuachie sisi wenye dini zetu.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...