Na Mwandishi Wetu

Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetoa ufafanuzi kuhusu malalamiko ya baadhi ya wananchi kuwa Tume hiyo imeweka ukomo wa idadi ya wananchi wanaotoa maoni katika mikutano yake inayoendelea katika mikoa minane na kuwaomba wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi katika mikutano inayoitishwa na Tume na kutoa maoni yao kwa uhuru na uwazi.

Katibu wa Tume hiyo Bw. Assaa Rashid amesema leo (Jumapili, Julai 8, 2012) kuwa Tume ingependa kupata maoni ya kila mwananchi na hivyo haiwezi kuweka ukomo kwa wananchi kutoa maoni katika mikutano inayoiitisha.

Ufafanuzi wa Tume hiyo unafuatia taarifa kupitia vyombo mbalimbali vya habari zikinukuu baadhi ya wananchi wakilalamika kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeweka kikomo cha idadi ya maswali na watu wanaotakiwa kutoa maoni yao katika mikutano ya kukusanya maoni ya wananchi.

Taarifa hizo ziliongeza kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba imekuwa ikitoa nafasi kumi tu kwa wananchi wanaopaswa kuuliza maswali yasiyozidi kumi katika mkutano mmoja na kwamba, katika baadhi ya Wilaya, ikiwemo Biharamulo yenye Kata 15, ni Kata sita tu ndizo zilizofikiwa na Tume.

“Katika baadhi ya Wilaya, kama Kusini Unguja na Bahi mkoni Dodoma, Tume imelazimika kuongeza muda wa kupokea maoni ya wananchi na wakati mwingine kuongeza idadi ya mikutano hadi kufikia mitatu badala ya miwili kwa siku. Hatua hizi zinalenga kutoa fursa zaidi kwa wananchi kutoa maoni yao,” amesema Bw. Assaa katika taarifa yake kwa vyombo habari.

Kuhusu mikutano iliyofanyika wilayani Biharamulo, Bw. Assaa amesema Tume ilipanga na imefanya mikutano sita kuanzia terehe 2 hadi 4 Julai, 2012 na jumla ya wananchi 267 walitoa maoni yao kwa mdomo na wananchi wengine 265 walitoa maoni yao kwa maandishi.

Kwa mujibu wa katibu huyo, vituo ambavyo mikutano hiyo ilifanyika ni Kelenge, Movata, Nyamigogo, Runazi, Nyakanazi na Biharamulo Mjini.

“Katika mikutano hiyo na mikutano mingine yote Tume haikuweka na haitaweka ukomo wa idadi ya wananchi wanaopaswa kutoa maoni,” amefafanua Bw. Assaa na kuongeza kuwa Tume inatambua kuwa wananchi wana shauku kubwa ya kutoa maoni yao kuhusu Katiba Mpya.

Hata hivyo, Katibu huyo alisema kuwa ingawa Tume ingependa kumfikia kila mmoja mahali alipo, jiografia ya nchi na muda ambao Tume imepewa, jambo hilo halitawezekana na kuwasihi wananchi kujitokeza kwa wingi katika maeneo ambayo Tume itafanya mikutano kama ratiba iliyotolewa inavyoelekeza.

Akifafanua kuhusu malalamiko kuwa baadhi ya Kata hazitafikiwa na Tume, Bw. Assaa amesema Tume haikupanga ratiba ya mikutano ya kukusanya maoni haikupangwa kwa kuzingatia Kata, bali imepangwa kwa kuzingatia eneo ambalo linaweza kujumuisha wananchi kutoka zaidi ya Kata moja.

Pamoja na kutoa maoni yao kupitia mikutano, Tume pia imewaomba wananchi kuendelea kutumia fursa nyingine kuwasilisha maoniyao kama tovuti ya Tume (www.katiba.go.tz), barua pepe (maoni@katiba.go.tz) au kwa njia ya posta kupitia Tume ya Mabadiliko ya Katiba, S.L.P. 1681, Dar es Salaam na S.L.P. 2775, Zanzibar.

Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilianza kufanya awamu ya kwanza ya mikutano ya kukusanya maoni ya wananchi katika mikoa minane tarehe 2 Julai mwaka huu na inatarajiwa kumalizika tarehe 30 mwezi huu. Mikoa hiyo ni Dodoma, Kagera, Kusini Pemba, Kusini Unguja, Manyara, Pwani, Shinyanga na Tanga.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 8 mpaka sasa

  1. AnonymousJuly 08, 2012

    kwa nini njia moja tu inatumika, sisi waghaibu itakuwa vipi.

    njia ya barua pia ingekuwepo.

    ReplyDelete
  2. AnonymousJuly 09, 2012

    Ipo njia ya barua Anonymous, huoni unaambiwa kwa njia ya posta S.L.P 1681 Dsm na 2775 Zanzibar.

    ReplyDelete
  3. AnonymousJuly 09, 2012

    njia ya barua ipo pia kuna address hapo chini S.L.P 1681 DSM au 2775 Zanzibar

    ReplyDelete
  4. AnonymousJuly 09, 2012

    Wewe wa "UGHAIBU" read between the lines, there are the addresses for Tanzanians.

    ReplyDelete
  5. AnonymousJuly 09, 2012

    wewe anony... hapo juu vipi au kuwa ughaibuni kumekufanya usijue kiswahili au ndio mvivu wa kusoma na kama mvivu wa kusoma utachangiaje katiba... soma maelezo ya katibu mpaka mwisho S.L.P zimeoneshwa hapo, barua pepe ipo, website imetajwa unataka nini tena... au ulikuwa huna cha ku 'comment', ukaona useme uko ughaibu??? hahaha pole ndugu ughaibu sio ishu siku hizi.. hahaha!

    ReplyDelete
  6. AnonymousJuly 09, 2012

    tusiwe wavivu wa kusoma... wewe anony... uliechangia mwanzo hebu soma kwa utulivu hiyo taarifa kwenye kwenye 'paragraph' inayoanza na "Pamoja na ......." kila nia imetajwa hapo , ya barua za kawaida, barua pepo na nyengine. au ulikuwa unataka kusema kuwa upo ughaibuni??

    ReplyDelete
  7. AnonymousJuly 09, 2012

    hebu soma hii taarifa hadi mwisho pls pls pls!

    ReplyDelete
  8. Mdau soma taarifa kwa ukamilifu kabla ya kutoa maoni mbona hapo umepewa email na website je hizo siyo njia mbadala? au mwenzetu unataka kutuma barua toka huko ughaibuni itafika lini? lakini nayo ni njia unaweza kutumia. Umeambiwa email ni maoni@katiba.go.tz na website ni www.katiba.go.tz. nimeona tu nikusaidie kusudi usiendelee kulalamika wakati taarifa ina majibu unayouliza.

    Ni vizuri kusoma taarifa kwa ukamilifu ndugu yangu.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...