Jumuiya ya Wanataaluma Waislamu Tanzania (TAMPRO) imetoa msaada wa vifaa tiba kwa Hospitali ya Taifa Muhimbili vinavyokadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 100 katika maeneo ya upasuaji, vifaa vya nusu kaputi, vifaa vya matibabu ya pua, koo na masikio, vifaa vya watoto pamoja na vifaa kwa ajili ya chumba maalumu cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU).
 Akikabidhi vifaa hivyo, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Mh. Dkt. Hussein Mwinyi alisema msaada huo umekuja wakati muafaka kusaidia juhudi za Serikali katika kutoa huduma kwa wananchii. “Ni dhahiri kuwa vifaa hivi vina gharama kubwa na hivyo mmeipunguzia Hospitali gharama hiyo, tunawashukuru sana. Kwa ujumla haya ni baadhi tu ya maeneo muhimu katika Hospitali ambayo kwa kiwango kikubwa yana mahitaji makubwa ya vifaa vya tiba”.
 Sera ya ushirikiano baina ya sekta ya umma na sekta binafsi inaelezea ushirikiano wa karibu katika ya mashirika binafsi na Hospitali za serikali katika kutoa huduma za afya. Serikali peke yake ina changamoto kubwa kutimiza mahitaji yote ya vifaa tiba na vifaa kwa Hospitali ya Taifa Muhimbili. Hivyo wanapojitokeza wadau mbalimbali kusaidia utoaji bora wa huduma za afya kwa kuchangia vifaa basi inakuwa ni faraja kubwa sana kwetu, alisema Dkt. Mwinyi.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanataaluma wa Kiislamu Tanzania Bw. Mussa Mziya alisema kuwa Serikali inajitahidi vilivyo katika kupeleka huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi wake, haswa huduma za lazima kama afya na elimu pamoja na uwezo mdogo wa kugharamia huduma hizi kwa mamilioni ya Watanzania, hivyo kuwa vigumu kutoa huduma hizi muhimu kwa wananchi wote. Aidha alisema  mara kwa mara viongozi wetu wamekuwa wakihimiza wananchi wenye uwezo na taasisi za kijamii na kidini kusaidia juhudi hizi za Serikali kutoa huduma za jamii kwa wananchi na ndiyo maana kwa kulifahamu hili na kutambua wajibu wetu katika kuisaidia jamii, TAMPRO imekuwa ikijitahidi kila inapoweza na kwa kusaidiana na taasisi rafiki za ndani na nje ya nchi kutoa misaada mbalimbali ya kijamii kwa wananchi.
 Taasisi  ya Wanataaluma Waislamu Tanzania (TAMPRO) ni taasisi isiyo ya Kiserikali iliyosajiliwa na Serikali mnamo mwaka 1997, ambayo ilianzishwa na Wanataaluma hawa kwa lengo mahsusi la kuisaidia jamii nzima ya Watanzania katika maeneo mbalimbali ya huduma za kijamii kama vile – Elimu, Afya, Ushauri na Utafiti. Aidha TAMPRO pamoja na kuwa si jumuiya ya kutafuta faida (non-profit organization) ina miradi kadhaa ya mfano katika shughuli zake za kuwahudumia wananchi: ikiwemo vituo vya afya na zahanati jijini Mwanza na Mkuranga mkoani Pwani, Shule ya Sekondari Sotele Mkuranga,  Kituo cha Maendeleo ya Ufundi (Skills Development Centre – Temeke Tungi) ambacho kinaendesha mafunzo mbalimbali ya ushonaji na kompyuta, Kwa kushirikiana na (Helping Hand), mradi wa ng’ombe wa maziwa, mbuzi wa maziwa na kuku wa kienyeji kwa kushirikiana na  Shirika la HEIFER INTERNATIONAL la Marekani, katika wilaya ya Kisarawe ambapo zaidi ya wananchi 150 watanufaika na  mradi huu  ambao unathamani ya jumla ya pesa za kitanzania (Tsh 100 mil).
DSC05550.JPG
Aliyesimama ni Kaimu MKurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Sr. Agnes Mtawa akimkaribisha Mh. Waziri
wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hussein Mwinyi (MB). Mwenye tai nyekundu ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanataaluma Waislam Tanzania Bw. Mussa Mziya.
DSC05555.JPG
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanataaluma Waislam Tanzania Bw. Mussa Mziya akitoa taarifa ya TAMPRO
DSC05561.JPG
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanataaluma Waislam Tanzania Bw. Mussa Mziya akimkabidhi Mh. Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii sehemu ya msaada huo.
DSC05572.JPG
Baadhi ya wanachama wa Jumuiya ya Wanataaluma Waislam Tanzania katika picha ya pamoja na Mh. Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii baada ya kukabidhi msaada kwa Muhimbili
DSC05576.JPG
Wakiketa jambo na Mh. Waziri kutoa kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Sr. Agnes Mtawa, akifuatiwa na Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Donald Mbando na Mwenyekiti wa TAMPRO Bw. Mussa Mziya


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...