Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Emanuel Humba akitoa maelezo ya utangulizi kwa Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya mjini Dodoma juzi.
Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti, Raphael Mwamoto akitoa mada ya utekelezaji wa shughuli za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya katika kikao kazi cha Wakuu wa Mikoa na Wilaya.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mwantumu Mahiza akichangia jambo katika kikao hicho.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Joseph Simbakalia akitoa mchango wake.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya akichangia mada katika kikao kazi hicho.
Washiriki wa kikao kazi hicho wakifuatilia mada ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya. 

 Na Mwandishi Wetu, Dodoma

SERIKALI imeshauriwa kubadili utaratibu wa matibabu kwa Maofisa Waandamizi ili kuwawezesha kunufaika na huduma za matibabu kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

Ushauri huo umetolewa na Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya mjini Dodoma katika kikao kazi cha siku tatu ambacho kiliongozwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.

Wamesema kuwa utaratibu wa sasa ambao unaonesha kuwa matibabu ni moja ya stahiki zao unawazuia Wakuu hao kunufaika na huduma za matibabu kupitia NHIF ambazo walisema zimeboreshwa sana kwa sasa na zina mtandao mkubwa unaowezesha kupata huduma mahali popote nchini.

Akichangia mada iliyowasilishwa na NHIF kwa wakuu hao, Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Moshi Chang’a alisema kuwa “Tunataka kuwa wanachama wa NHIF hata sasa ila kinachotubana ni hizo stahiki ambazo tumepewa ikiwemo ya matibabu kulipiwa na Serikali, ipo haja sasa ya Serikali kupeleka fedha NHIF ili sisi tutibiwe na Mfuko,” alisema Chang’a.

Alisema kuwa ni vyema wakajiunga na NHIF ambayo itawasaidia kunufaika na fao la wastaafu lakini pia itawapa hamasa kubwa katika uhamaishaji kutokana na ukweli kwamba watakuwa miongoni mwa watumiaji wa huduma hizo.

Akijibu hoja hiyo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema kuwa kwa sasa wakuu hao wanaweza wakajiunga wakati Serikali ikiliangalia suala hilo ili liwe kwenye utaratibu wanaoutaka.

Akitoa maelezo ya awali kwa viongozi hao, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Emanuel Humba alisema kuwa ili Mfuko ufanikiwe kuwafikia Watanzania wengi kama nchi zingine zilizofanikiwa katika suala hilo ni lazima viongozi wakawa wanachama au wanufaika wa huduma za Mfuko.

“Nchi zilizofanikiwa kuwaingiza wananchi wake kwenye utaraibu wa Bima ya Afya kama Ufilipino, Korea, Rwanda viongozi wake Wakuu ni wanachama wa Mifuko hiyo… hivyo nanyi wakuu wetu mkijiunga itakuwa ni kazi rahisi kufikia malengo yetu,” alisema Humba.

Aidha aliwaomba wakuu hao kuhakikisha wanafuatilia fedha zinazolipwa na NHIF katika Vituo vya Kutolea huduma kwenye maeneo yao ili zisaidie kuboresha huduma za matibabu ikiwemo ununuzi wa dawa na Vifaa tiba.

Katika suala hilo la Malipo, Waziri Mkuu aliutaka Mfuko kuweka utaratibu wa kuwapa taarifa za fedha viongozi wakiwemo Wakuu wa Mikoa, Wilaya, wabunge ili waweze kuzifuatilia katika matumizi yake.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...