Na Ripota wetu.
  
TUME ya kuchunguza chanzo cha kushuka kwa kiwango cha ufaulu wa mtihani wa kidato cha nne mwaka 2012, imesema Serikali inaandaa mkakati wa kuboresha matokeo unaojulikana kama Mkakati wa Kuboresha Matokeo (Better Results Now -BRN).

Mwenyekiti wa Tume hiyo Profesa Sifuni Mchome amesema lengo la mkakati huo ni kuleta maendeleo ya elimu nchini na tayari wataalamu wa ndani na nje ya nchi wanashiriki kikamilifu katika kufanikishwa zoezi hilo

Profesa Mchome amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizugumza na waandishi wa habari juu ya hatua iliyofikiwa mpaka sasa na Tume hiyo katika kutekeleza majukumu yake ya uchunguzi na kupata majibu kutoka kwa wadau wa elimu nchini.

Mwenyekiti huyo aliwaomba wananchi, taasisi mbalimbali na hata vyama vya siasa nchini bila kujali itikadi zao, kushiriki na kuhamasishana katika utoaji wa maoni kwa tume ili kufanikisha utatuzi wa changamoto zinazokwaza maendeleo ya elimu nchini.

“Pamoja na changamoto za muda mrefu zinazoikabili sekta ya elimu nchini, taifa bado linaendelea kupiga hatua na kujiwekea dhamira na mikakati ya kuleta maendeleo kupitia sekta mbalimbali” alisema Profesa Mchome.

Alifafanua kuwa changamoto hizo zinahitaji kuwekewa nguvu za pamoja na kutoa maoni endelevu ili kupata mustakabali wa jinsi ya kuinua elimu nchini katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu.

Profesa Mchome alisema hadi sasa wamefanya mahojiano na taasisi, mamlaka na wadau mbalimbali wa elimu nchini ambao wameainisha sababu za kushuka kwa kiwango cha ufaulu katika mtihani huo.

Alitaja baadhi ya taasisi na mamlaka hizo kuwa ni Chama cha Wamiliki wa Shule Binafsi nchini (TAMONGSCO),Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA) kanda ya Dar es Salaam, Chama cha Walimu Tanzania, viongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Taasisi ya Elimu Tanzania na Baraza la Mitihani Tanzania.

Wadau wengine waliohojiwa na tume hiyo ni Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala, Mameya, Maafisa Elimu wa miko ya Dar es Salaam na Tanga, Wakaguzi wa Elimu, Wajumbe na Wakuu wa shule mbalimbali za Dar es Salaam, wazazi wanafunzi na wananchi kwa ujumla.

“Mpaka sasa tumeshapokea ujumbe mfupi wa simu  zaidi ya 300, ujumbe kupitia tume tumepokea zaidi ya 200, baruapepe nyingi sana na watu tuliokutana nao ni zaidi ya 40, pia tumepokea simu nyingi sana ingawa changamoto ni mazungumzo” alisema Profesa Mchome na kuongeza kuwa:

“Maoni tuliyoyapata mpaka sasa ni shida ya walimu hawatoshi, uchache wa vitabu, hali ya majengo hairidhishi na umbali wa shule, na hizi shida zipo kwenye shule za Serikali na binafsi na kuna baadhi ya shule binafsi ni nzuri  lakini lina shida zaidi”

Kwa sasa wajumbe wa tume wako katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Tanga, Manyara, Arusha, Morogoro, Pwani, Simiyu, Shinyanga na Mbeya ambapo wanafanya mahojiano na wakuu wa mikoa na wilaya na shule, walimu, wanafunzi na wajumbe wa bodi za shuke za sekondari zilizoko kwenye mikoa hiyo.

Mwenyekiti huyo alisema baada ya wajumbe wa tume hiyo kumaliza kazi katika mikoa hiyo, watafanya safari za Zanzibar na Dodoma kuanzia Mchi 24 na kufanya mahojiano na vingoz wa serikali wa visiwa vya Unguja na Pemba na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Tume ya kuchunguza chanzo cha kushuka kwa kiwango cha ufaulu wa mtihani wa kidato cha nne mwaka 2012, iliundwa na Waziri Mkuu Machi 2 mwaka huu ili kutafua sababu zilizochangia matokeo yasiyoridhisha ya mtihani huo na inatarajiwa kukamilisha kazi yake baada ya majuma manne kuanzia sasa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 5 mpaka sasa

  1. Ni muhimu tuzingatie kila kitu, mimi proposal yangu ni hii katika hii Tanzanian Education Reform blog.

    http://www.leadergennis.blogspot.com/

    ReplyDelete
  2. Sawa Mdau wa kwanza, kwa nini usitume kama Full Proposal moja kwa moja kwenye Kamati na nakala ingine Serikalini?

    Nadhani peleka Printed Pack na uielekeze moja kwa moja ktk hiyo Kamati iliyoundwa na Waziri Mkuu.

    ReplyDelete
  3. Muache Siasa na mzingatie Sayansi, pia muwe mnakubali kukosolewa endapo panatokea Mkosoaji ktk suala la Mfumo wa Elimu!

    ReplyDelete
  4. Kamati hii itafaa zaidi itoe muelekeo wao huko Bungeni kwa waliotetea ya kuwa Mtaala ni mbovu wakati Mhe.Mbatia alipokosoa!

    ReplyDelete
  5. Ushirikiano na Uingereza Mkoloni wetu nadhani ungalipo kupitia Ubalozi wa Uingereza nchini licha ya kuwa tulikwisha pata Uhuru tokea mwaka 1961.

    Ya nini tuhangaike kuhusu suala la Elimu kuanguka nchini?

    Hata kama tunakuwa huru Kisiasa kwa nini tusimwachie Mkoloni wetu Mwingereza arudi kusimamia Elimu?

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...