Wizara ya Maliasili na Utalii imewataka wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya Ardhioevu ambayo ni makazi na mapito ya ndege wahamao kushirikiana na Serikali katika kuwalinda ndege hao na kuhifadhi mapito na makazi yao. Wananchi pia wanakumbushwa kuwa maeneo ya ardhioevu ndio vyanzo vya maji ambayo yanafaa kwa matumizi ya kila siku ya binadamu, wanyama na ndege, hivyo maeneo hayo yalindwe.
Taarifa hii imetolewa na Wizara wakati huu wa maadhimisho ya Siku ya Ndege Wahamao Duniani ambayo huadhimishwa kimataifa tarehe 11 na 12 Mei kila mwaka.
Aina za ndege hao ni kama vile Heroe mkubwa na mdogo (flamingos) ambao wanahama kila mwaka kutoka sehemu moja ya dunia kwenda nyingine kutafuta malisho, maji, kukwepa hali mbaya ya hewa na kupata sehemu salama ya kuzaliana.
Tanzania ni nchi mojawapo yenye sehemu nyingi ambazo ni salama kwa mazalia ya ndege. Kwa mfano, Ziwa Natron ni maarufu kwa mazalia ya ndeye aitwaye Heroe mdogo. Inakadiriwa kuwa asilimia 80 ya Heroe mdogo kote duniani huzalia katika Ziwa Natron liliko Kaskazi mwa Tanzania.   Ziwa hilo ni kivutio cha utalii kutokana na ndege hao.
Maadhimisho ya Siku ya Ndege Wahamao Duniani yalianza mwaka 2006 na kuendelea kusherehekewa kila mwaka mwishoni mwa wiki ya pili ya kila mwezi Mei.  Watu duniani kote huitumia fursa hii kutoa elimu na kufanya matembezi katika sehemu zenye Ndege hawa  kwa ajili ya kusherehekea siku hii.
Ujumbe wa mwaka huu wa Siku ya Ndege Wahamao ni: "Tuunganishe juhudi zetu katika kuwahifadhi ndege wahamao mapito na makazi yao (Networking for migratory birds), ". Tafsiri ya ujumbe huu ni kuwa nchi, mashirika na watu binafsi wanatakiwa kuunganisha maeneo ya ardhioevu kwa ajili ya uhifadhi endelevu wa ndege wahamao.
Utunzaji kwa ndenge wahamao ni sababu mojawapo iliyofanya Tanzania kusaini Mkataba wa Uhifadhi wa Ardhioevu (Ramsar) mwaka 2000. Ardhioevu, pamoja na maufaa mengine,  ni makazi ya ndege wahamao.
Kutokana na Mkataba huo Tanzania imetenga maeneo ya Ramsar ambayo ni muhimu katika kuhifadhi bioanuwai. Maeneo ya ardhioevu yaliyotengwa ni pamoja na Ardhioevu zenye umuhimu wa kimataifa kama vile:- Malagarasi-Muyovozi ambayo ni muhimu kwa uhifadhi wa ndege aina ya Korongo domokiatu (Shoebill stork), na eneo la Ramsar la Ziwa Natron ambalo ni muhimu katika kuhifadhi  ndege aina ya Heroe mdogo (lesser flamingo) .
Serikali imekuwa ikiwajengea wananchi uwezo wa kuhifadhi na kutumia rasilimali za ardhioevu nchini kwa kutoa elimu ya uhifadhi katika maeneo yanayozunguka maeneo ya Ramsa. Maeneo hayo ambayo ni makazi muhimu ya ndege wahamao yanasimamiwa na Sheria ya Kuhifadhi Mazingira ya mwaka 2004 na ya Kuhifadhi Wanyamapori ya Mwaka 2009. 

George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
11 Mei 2013

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. AnonymousMay 11, 2013

    Asante Bwana Matiko, tumesikia na tumejifunza kitu.

    Sikuwa najua kama kuna siku maalumu inaitwa hivyo.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...