HATIMAYE uongozi wa mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Tanzania bara Yanga leo imempa mkataba wa miaka miwili kiungo wake mchezeshaji Haruna Niyonzima huku kukiwa na taarifa kuwa kiungo huyo amemwaga wino kwa dau la dola 70,000 sawa na Shilingi 111,654,000 milioni sambamba na mshahara wa dola 3,000 ingawa Yanga wenyewe wamegoma kuweka wazi kiasi hicho cha fedha.

Mshahara huo wa Niyonzima umepanda baada ya awali kupokea dola 1500 na kusajiliwa kwake, kumezikata ngebe klabu ambazo zilikuwa zikimnyemelea wakiwemo wapinzani wao Simba sambamba na Azam ikiwa ni pamoja na klabu moja ya nchini Tunisia.

Akizungumza Makao Mkuu ya klabu hiyo Niyonzima ambaye pia aliangusha chozi baada ya kukumbushwa baba yake mzazi aliyefariki miaka mingi alisema "Watu walitaka kujua mimi nitaenda wapi, ninachotaka kusema kwa sasa nimeamua kusaini Yanga na nitaitumikia kwa nguvu zangu zote kwa miaka miwili, na kwa sasa akili yangu naelekeza Kombe la Kagame.

"Kama wachezaji tumekuwa na matatizo mengi, ni kweli timu nyingi zilinifuata lakini niliamua kutuliza kichwa kwanza kabla sijaamua kufanya chochote, naheshimu kazi yangu, na ningependa Mungu anijalie hata nikimaliza mkataba huu mpya niendelee kuichezea Yanga."alisema Mnyarwanda huyo ambaye msimu uliopita alipata ulaji kwenda kuichezea timu ya El Merreikh ya Sudan na klabu hiyo ya Jangwani ilimzuia.

Hata hivyo habari ambazo zilizipatikana jana zinasema kuwa katika kikao kilichofanyika juzi jioni makao makuu ya klabu hiyo kulikuwa na mvutano mkubwa wa viongozi ambao wengine walitaka waachane na kiungo huyo ambaye alikuwa akiwadengulia kumwaga wino akitaka donge nono zaidi, wakifananisha na Sunday Manara 'Computer' ambaye alishawai kuitosa timu hiyo na kwenda Pan Afrika wakati akiwa ni mchezaji tegemeo.

Lakini jana Katibu mkuu wa klabu hiyo Laurance Mwalusako alisema wameamua kumuongezea mkataba Niyonzia kufuatia klabu hiyo kuhitaji mchango wake hasa katika michuano yao ya kimataifa kwani katika kipindi cha miaka miwili ameonyesha kiwango cha hali ya juu.

"Yamekuwa yakiongelewa mengi juu ya mchezaji wetu Niyonzima, ukweli leo umedhihirika kwamba Niyonzima ni mchezaji wa Yanga na ataendelea kuitumikia kwa miaka miwili.

Haruna Niyonzima alijiunga na Yanga kwa mara ya kwanza Julai 2011 akitokea katika timu ya APR nchini Rwanda ambapo katika miaka yake miwili aliyoichezea timu ya Yanga amefanikiwa kuisadia kupata makombe mawili ya ubingwa wa Ligi Kuu 2012-2013 na Kombe la Kagame 2011-2012.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...