Moja ya barabara za mitaa kata ya Iwawa Makete mjini zikiwa zimelundikwa vifusi kwa zaidi ya miezi mitatu sasa huku kukiwa na kibao kikionesha barabara imefungwa ilihali magari yanapita hivyohivyo licha ya maelekezo ya kibao hicho(Habari/picha na Edwin Moshi)
Vifusi vikiwa vimelundikwa barabara ya kuelekea hospitali ya wilaya ya Makete 
Hapa inalazimu magari kupita kwenye mifereji
 Vifusi vingine hadi vimeyeyuka kutokana na kukaa muda mrefu
Wananchi wa kata ya Iwawa wilayani Makete ambao ni watumiaji wakubwa wa barabara za mitaa katika kata hiyo, wameiomba halmashauri ya wilaya ya Makete kusambaza vifusi vilivyopo katika barabara hizo ambavyo vimewekwa zaidi ya miezi mitatu sasa

Wananchi hao wametoa ombi hilo kufuatia adha wanayoipata hasa wanapotumia magari kwa kuwa barabara hizo zimekuwa nyembamba hivyo kuleta usumbufu kwa watumiaji hasa wakati wa magari kupishana


Mmoja wa mwananchi aliyezungumza na ripota wetu Bw. Sipati Mbwilo amesema wanashangaa vifusi hivyo kukaa muda mrefu barabarani bila kusambazwa, jambo linalosababisha usumbufu kwa watumiaji na wakati mwingine kulazimika kuzunguka kupita kwenye barabara nyingine ili kufuata huduma hata kama huduma hiyo ipo jirani

“Unajua braza unaweza kukuta umepata kazi ya kupeleka kuni ama kwenda kuchukua kuni kwa gari, lakini inakulazimu uzunguke umbali mrefu ili kukwepa hivi vifusi ambavyo hatujui vitasambazwa lini, ni bora wangeviweka pindi watakapokuwa tayari kuvisambaza leo mwezi wa tatu vifusi vipo barabarani mambo gani haya” alisema Mbwilo

Naye dereva wa lori aliyejitaja kwa jina la Kisauti amesema vifusi hivyo vinawapa tabu wanaoendesha magari makubwa kutokana na wembamba wa barabara na wakati mwingine kulazimika kukataa baadhi ya kazi wanazozipata kutokana na magari yao kushindwa kupita kwenye barabara hizo

Ripota wetu amezungumza na mhandisi wa ujenzi wilaya ya Makete Mhandisi Samwel Ndoveni ambaye amekiri kuwepo hali hiyo lakini amesema kero hiyo itaondolewa hivi karibuni kwa kuwa msimu wa mvua uliokuwa ukikwamisha utekelezaji wa zoezi hilo unamalizika na mkandarasi ataanza kazi mara moja

Amesema kwa mwaka huu mvua zilinyesha kwa wingi na ndiyo maana zoezi hilo lilishindwa kutekelezeka kwa wakati kama ofisi yake ilivyokuwa imepanga

“Ni heri lawama za kutokusambaza vifusi zitupate kuliko tungesambaza vifusi wakati mvua inanyesha, matokeo yake tungetengeneza tope jingi na barabara zisingepitika huo ungekuwa ni uharibifu wa fedha za serikali” alisema Mhandisi Ndoveni

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. AnonymousMay 12, 2013

    Tego la uchaguzi hilo, vuteni subira kidogo wananchi vitasambazwa tu muda ukikaribia.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...