Sekretarieti ya Mkoa wa Dodoma mwishoni mwa wiki ilifanya kikao cha pili cha baraza la wafanyakazi wake ambapo kwa mujibu wa katibu wa baraza hilo Ndugu Paul Masanja wajumbe wa baraza hilo ni pamoja na wawakilishi kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Ofisi zote za Wakuu wa Wilaya Mkoa wa Dodoma, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na Uongozi wa chama cha wafanyakazi wa serikali kuu na Afya TUGHE Mkoa.

Masuala muhimu katika kikao hiko cha baraza la wafanyakazi yalijumuisha Nafasi ya vyama vya wafanyakazi ndani ya baraza hilo, masuala ya mafao kwa watumishi wa Umma. Vilevile mapitio ya bajeti ya mwaka 2012/13, bajeti ijayo ya 2013/14 na kupitia mtiririko wa bajeti kwa kipindi cha kuanzia 2009/10 hadi 2013/14.
Mgeni rasmi katika kikao hiko alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dr. Rehema Nchimbi ambapo miongoni mwa masuala aliyoyapa msisitizo katika salamu zake za ufunguzi wa kikao hiko ni pamoja na yafuatayo:

·        Sera ya “Tenda kwa matokeo makubwa sasa” (Big Result Now). Dr. Nchimbi aliwataka watumishi wa umma kwa nafasi zao kwenye ofisi za serikali na shughuli mbalimbali lazima wajiwekee vipaumbele vya majukumu yao na kuweka mkakati mzuri wa utekelezaji utakaoleta ufanisi mkubwa na kasha kuweka utaratibu wa kupima matokeo ya utendaji.
Alifafanua kuwa lazima wafanyakazi waweke vipaumbele vinavyolenga kuleta mabadiliko makubwa katika kutatua kero na changamoto za wananchi mfano kwenye sekta ya utunzaji kumbukumbu/masijala, Afya na sekta zingine za huduma na uzalishaji.

·        Dr. Nchimbi aliwataka watumishi/wafanyakazi hususani wataalamu wa kilimo kujadili na kutafuta ufumbuzi wa pamoja wa tatizo la muda mrefu la upungufu wa uzalishaji wa chakula ndani ya mkoa unaoleta tatizo la upungufu wa chakula mara kwa mara mkoani Dodoma ukilinganisha na mahitaji ya chakula yaliyopo kwa hivi sasa.

·        Vilevile aligusia tatizo/changamoto ya Mkoa wa Dodoma kuwa na matokeo yasiyoridhisha katika sekta ya elimu hususani ngazi ya msingi na sekondari. Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa Dr. Nchimbi, wafanyakazi wanaujuzi na utaalamu katika nyanja mbalimbali kulingana na mahitaji hivyo hawana budi kutumia utaalamu na ujuzi wao wote kusaidia Mkoa wa Dodoma kuondokana na tatizo lao la kufanya vibaya kwenye sekta ya elimu.

·        Msisitizo mwingine uliwekwa kwenye suala la kuboresha hali ya makazi ya wananchi/ujenzi wa nyumba bora za makazi za wananchi na uondoshaji wa Tembe. Wataalamu wawasaidie wananchi kuboresha shughuli zao za uzalishaji na kujiwekea utaratibu wa kufanya mavuno kwenye shughuli zao hususani kuvuna mifugo na mazao na kuwekeza kwenye kuboresha makazi yao kuanzia ngazi za vijijini hadi mijini.
  
·        Dr. Nchimbi aliwatahadharisha watumishi wa Umma wenye tabia ya kuhujumu serikali wawe makini, aidha alikemea mahubiri hasa ya siasa yenye  viashiria vya uvunjifu wa amani, utulivu na mshikamano, vurugu na umwagaji damu; aliwaasa watumishi/wafanyakazi wasikubali kujihusisha na suala hili. Badala yake watumishi wa umma wanatakiwa kuzingatia maadili mema ya kazi zao, kuzingatia taratibu, kanuni na sheria ili kuboresha utoaji wa huduma katika sekta zote.

·        Vilevile Dr. Nchimbi aliwasisitiza wafanyakazi waone umuhimu wa kijiendeleza kielimu ili kuzidi kuboresha utoaji wa huduma zao na utendaji wao kwa ujumla. Aliwataka wafanyakazi watumie fursa zilizopo kama vile vyuo kujiendeleza. Aliwaagiza waajiri (Katibu Tawala Mkoa) kutoa kipaumbele cha ruhusa kwa ya kusoma kwa watumishi wa serikali wanaotaka kujiendeleza kielimu kupitia chuo kikuu huria cha Tanzania tawi la Dodoma kwa kuwa hawaaribu ratiba ya kazi kwani wanaweza kusoma huku wanafanya kazi kuitumikia serikali.

Alikemea tabia ya watumishi/wafanyakazi wasiopenda kujiendeleza kielimu kwa kubakia kwenye daraja moja la elimu kwa muda mrefu bila kujiendeleza na kusema kuwa inazorotesha utendaji na ufanisi.

Kwa upande wake mwenyekiti wa baraza hilo la wafanyakazi wa sekretarieti ya Mkao wa Dodoma  ambaye pia ni Katibu Tawala wa Mkoa Dodoma Ndugu Rehema Madenge alitoa Rai kwa wafanyakazi wa serikali wawe na desturi ya kubadilika kuanzia sasa na kusisitiza alichokieleza mkuu wa mkoa hususani sera ya Tenda kwa Matokeo Makubwa Sasa (Big Result Now).

Imetolewa na:
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma

Idara ya Habari

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...