NA RAMADHANI ALI- MAELEZO ZANZIBAR 
Wizara ya Afya ya Zanzibar imetiliana saini mkataba wa makubaliano wa kuanzishwa kwa majaribio kutolewa huduma za maradhi ya afya ya akili katika Hospitali ya Makunduchi iliyoko Mkoa wa kusini Unguja. Uwamuzi wa kuifanya Hospitali ya Makunduchi kuanzisha huduma hiyo inatokana na mapendekezo ya Wizara ya Afya ya mwaka 2008 na taarifa ya Afya ya akili Zanzibar ya Jumuia ya Ulaya. 
Wadau watatu wanashirikiana katika mpango huo ambao ni Hospitali ya Chuo Kikuu cha Haukeland cha Norway, Hospitali ya Afya ya akili ya Kidongochekundu na Mradi wa kuimarisha Afya Zanzibar. Katika sherehe za utiaji saini zilizofanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja, Wizara iliwakilishwa na Katibu Mkuu Dk. Mohammed Jiddawi, Chuo Kikuu cha Haukeland kiliwakilishwa na Dk. Ingavr Bjelland, Dk. Peter McGovern alitia saini kwa upande wa Mradi wa kuimarisha Afya kijiji cha Makunduchi na Dk. Khamis Othman alitia saini kwa upande Hospitali ya Kidongo Chekundu. 
Wadau hao watatu watashirikiana katika kuimarisha kujenga uwezo huduma za maradhi ya Afya ya akili kwa visiwa vya Unguja na Pemba, kuanzisha mtaala wa kufundisha masomo ya afya ya akili wafanyakazi wa Hospitali ya Makunduchi kwa mujibu wa Shirika la Afya duniani (WHO) na kuunga mkono maendeleo ya mafunzo yanayotolewa kwa wauguzi wa Hospitali ya Makunduchi na Hospitali ya Kidongo chekundu. 
Katika hatua za awali zitakazoanzia mwaka huu, kliniki ya afya ya magonjwa ya akili ya Hospitali ya Mkunduchi itasimamiwa kwa kiasi kikubwa na Hospitali ya Kidongo chekundu na mafunzo yatatolewa katika mwaka wa kwanza wa kuanzishwa huduma katika Hospitali hiyo. Hatua ya pili ya mpango huo itakayoanza mwezi Januari mwakani ambapo kliniki hiyo itakuwa imeimarika na Hospitali mama ya Kidongo chekundu kuridhika na hatua iliyofikia, Hospitali hiyo itaruhusiwa kujiendesha yenyewe katika masuala mbali mbali ya uongozi na tiba. 
Kwa mujibu wa makubaliano hayo Hospitali ya Chuo Kikuu cha Haukeland itasimamia na kuimarisha mitaala ya elimu ya magonjwa ya Afya ya akili kwa wafanyakazi wa Hospitali ya Makunduchi ikiwemo kusimamia mafunzo hayo. 
Wadau wote kwa pamoja wamekubaliana kuendeleza na kuimarisha huduma za magonjwa ya afya ya akili katika kliniki ya Makunduchi kwa mujibu wa misingi ya Shirika la Afya Duniani. Hospitali ya Makunduchi itakuwa ni ya pili kutoa huduma za magonjwa ya Afya ya akili kwa kisiwa cha Unguja na kwa Kisiwa cha Pemba huduma hiyo bado inaendelea kutolewa katika Hospitali ya Chake Chake tu.
  Dk. Ingvar  Bjelland kutoka Hospitali ya Chuo Kikuu cha Haukeland  nchini Norway akitoa maelezo jinsi  Hospitali hiyo itakavyotoa huduma ya magonjwa ya Afya ya akili Zanzibar katika sherehe za kutiliana saini zilizofanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.
 Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dk. Mohammed Jiddawi  na Dk. Peter McGovern  wakitia saini makubaliano ya kuanzisha huduma za Aya ya magonjwa ya akili katika Hospitali ya Makunduchi. Katikati ni Naibu Waziri wa Afya Dk. Sira Ubwa Mamboya akishuhudia utiaji saini  katika sherehe zilizofanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.
Dk. Ingvar  Bjelland kutoka Hospitali ya Chuo Kikuu cha Haukeland  nchini Norway na Daktari bingwa wa magonjwa ya akili wa Hospitali ya Kidongo chekundu wakitia saini makubaliano ya kuanzishwa huduma za magonjwa ya Afya ya akili katika Hospitali ya Makunduchi Kusini Unguja.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...