WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali haitataifisha shule, zahanati, hospitali wala Vyuo Vikuu vinavyoendeshwa na taasisi za kidini na amewahimiza wajenge zaidi na zaidi ili kuisaidia jamii kubwa ya Watanzania.

Ametoa wito huo wakati akizungumza na walimu, wazazi na wahitimu wa kidato cha nne wa shule ya sekondari Magnificat iliyoko Sanya Juu, wilayani Siha mkoani Kilimanjaro.

Waziri Mkuu ambaye aliwasili Sanya Juu jana asubuhi (Jumamosi, Septemba 20, 2014) akitokea Dodoma, alisema huko nyuma Serikali ilitaifisha shule na vyuo lakini kwa kiasi fulani ilishindwa kuviendesha ikaamua kuvirudisha kwa wamiliki wake ambao ni taasisi za kidini.

“Ni kweli huko nyuma tulikuwa navyo, lakini tumevirudisha kwenu tunataka na ninyi ni washirika katika kuleta maendeleo kwa wananchi walio wengi,” alisema Waziri Mkuu.

“Nilishawahi kusema huko nyuma na leo nasisitiza tena kwamba hatutaifisha shule, zahanati, hospitali wala Chuo Kikuu chochote cha taasisi ya kidini. Ninawasihi mjenge zaidi na zaidi,” aliongeza.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa shule hiyo iliyoanzishwa Januari 15, 2011, aliwakabidhi vyeti wanafunzi 42 wa kidato cha nne wanaotarajia kufanya mtihani wa kidato cha nne Novemba, mwaka huu ikiwa ni mara ya kwanza kwa shule ya sekondari ya Magnificat kufanya mtihani huo.

Waziri Mkuu aliwapongeza wanafunzi hao kwa kushika nafasi ya kwanzawilayani Siha kwenye mitihani ya utamirifu (yaani mock) katika kidato cha nne. “Vilevile, shule hii imekuwa ya 12 kati ya shule 316 za Mkoa wa Kilimanjaro na ya 16 kati ya shule 564 kwa Kanda ya Kaskazini Mashariki zilizofanya mtihani huo. Mimi napata imani kuwa watafanya vizuri kwenye mtihani wao wa kidato cha nne Novemba 2014,” aliongeza.

Mapema,Mkuu wa Shirika la Masista la Kazi ya Roho Mtakatifu na Meneja wa Shule hiyo, Sista Inviolata Kessy alisema shule hiuo ilianzishwa kwa lengo la kutoa elimu bora na kuwashawishi watoto wa kike wa Kimasai waone umuhimu wa elimu na hivyo kuwaepusha na ndoa za utotoni. Vile vile, kuwapa msingi mzuri wa elimu kama sehemu ya maandalizi yao ya kupata elimu ya juu.

Alisema shule hiyo ambayo ni ya mchanganyiko na ya mchepuo wa sayansi na biashara, imefanikiwa kujenga maabara tatu za kemia, fizikia na baiolojia pamoja na chumba cha kompyuta.

Akisomarisalakwa niaba ya wahitimu, Anastazia Kimaro alisema shule hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo ukosefu wa jengo la utawala pamoja na basi la shule la kuwapeleka wananfunzi kwenye ziara za mafunzo.

Aliomba pia wawe wanapelekewa magazeti ya kila siku na kila wiki ili wanafunzi wa shule waweze kupata taarifa mbalimbali za mambo yanayojiri nchini na duniani.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...