Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akisaini moja ya leseni za uchimbaji madini kwa wamiliki waliokidhi vigezo vya kuapatiwa leseni. Anayeangalia ni Mwanasheria Wizara ya Nishati na MadinI Phines Sijaona.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akimsikiliza mmoja wa waombaji wa Leseni za uchimbaji madini, Mark Stanely mmiliki wa kampuni ya Bafex Tanzania Limited (Kanda ya Kusini Magharibi) wakati wa kikao cha kusaini leseni za uchimbaji madini zilizokidhi vigezo.
Kamishna Msaidizi anayeshuhgulia Leseni, Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi John Nayopa, akifafanua jambo wa wamiliki wa kampuni ya Gemini Exploration & Mining Service Limited mara baada ya Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo kumaliza kusaini leseni hizo.


Na Asteria Muhozya, Dar es Salaam

Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amewataka wamiliki na waombaji wa leseni za kuchimba madini kuhakikisha wanayaendeleza maeneo yao kwa kufanya kazi katika muda walioomba kulingana na leseni hizo la sivyo watafutiwa leseni zao kwa mujibu wa sheria ya madini.

Waziri Muhongo ameyasema hayo wakati akisaini leseni za Kampuni mbalimbali zilizokidhi vigezo vya kupatiwa leseni za uchimbaji madini katika maeneo mbalimbali nchini na kuongeza kuwa, kuanzia sasa Wizara haitaruhusu wamiliki wa leseni za madini kuuza maeneo yao kwa wamiliki wengine na kubadilisha majina ya kampuni kutoka kwa mmiliki mmoja kwenda mwingine badala yake itaruhusu endapo pande mbili zitaingia ubia.

“Hatutakubali wamiliki wa leseni kuuza maeneo yao na kubadili jina kutoka kwa mmliki mmoja kwenda mwingine badala ya kuyaendeleza, lakini kama wanaingia ubia hilo linakubalika” alisisitiza Muhongo.

Kauli ya Waziri imekuja baada ya kubaini kuwa, baadhi ya wamiliki wa leseni za uchimbaji madini kutokuyaendeleza maeneo yao kwa muda mrefu pindi wanapopewa leseni na badala yake kuyauza na kubadili majina ya kampuni jambo ambalo linachochea migogoro katika maeneo husika.

“Wananchi wanategemea mara baada ya kampuni kupewa leseni waombaji waendeleze maeneo yao lakini badala yake maeneo yanakaa bila kuendelezwa jambo ambalo linaibua migogoro”, aliongeza Muhongo.

Aidha, ameongeza kuwa, hatua hiyo inalenga kuwafanya waombaji na wamiliki kuwajibika na kufanya kazi kisasa badala ya kufanya kwa mazoea.

“Hatutaki waombaji wafanye kazi kizamani, hatutaki kupotezeana muda katika hili”, alisisitiza Waziri.

Kampuni zilizopata leseni za uchimbaji, ni pamoja na Bafex Tanzania Limited (Kanda ya Kusini Magharibi) Autrad Mining Company Limited, Nyang’wale Diamonds Limited (Kanda ya Kati Magharibi) na Paulo Sungura na Joyce Abinel Sekwao (Kanda ya Magharibi).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...