Makadam na Prasad wakiwajibika
Wapenzi wakipigishwa mpumwende.

Baada ya ziara ya mafanikio ya mwezi mmoja mjini Addis Ababa, bendi ya Swahili Blues chini ya uongozi wa Leo Mkanyia imefanya ziara nyingine mjini Nairobi.

Bendi hiyo yenye maskani yake katika hoteli ya nyota tano ya Serena iliyo katikati ya mji wa Dar es Salaam ilianza ziara yake katika klabu maarufu inayojulikana kama Choices iliyopo katika barabara ya Baricho kwenye kitongoji cha Industrial Area. Shoo hiyo kabambe ilifanyika siku ya tarehe 23 April 2015 chini ya usimamizi wa kampuni maarufu ya Roots International katika mradi maalumu uliojulikana kama Thursday Nite Live @Choices kwa udhamini wa Tusker Malt Lager.
Shoo hii ilifana vilivyo na wapenzi lukuki waliohudhuria walikunwa kisawasawa na mirindimo kabambe toka kwa Swahili Blues Band. Wapenzi hao pamoja na kukunwa ipasavyo na umahiri wa Leo vilevile walifurahishwa sana na mwimbaji pamoja na mpiga ngoma Juma Setumbi. Kwa habari zaidi juu ya shoo hii tafadhali tembelea tovauti hiiwww.facebook.com/thursdaynitelive.

Siku ya tarehe 24 April, bendi ilifanya shoo yake ya pili katika ukumbi ujulikanao kama "At The Elephant" uliopo barabara ya Kanjata maeneo ya Lavington. Siku hiyo bendi ilipiga kabla ya mwanamuziki maarufu wa Kenya anayeitwa Dan 'Chizi' Aceda. Shoo hii nyingine kabambe iliandaliwa na mwanamuziki na mmiliki wa klabu hii aitwaye Eric Wainaina.Ilikuwa ni onyesho nyingine kabambe kweli kweli ambapo Leo, Henry Mkanyia na Felix Kijana walioonyesha umahiri mkubwa wa kusakata sindimba wakati walipo yaacha magitaa yao pembeni na kuanza kunengua ipasavyo. Mpumwende huu ulidhaminiwa na Nederburg pamoja na Culture Connect.

Siku ya Jumamosi ya tarehe 25 April bendi ilihamia katika ukumbi maarufu wa wasanii ujulikanao kama " The GoDown Arts Centre". Huo ulikuwa ni mpango maalumu wa kituo hicho kualika bendi mbalimbali kutoka Afrika Mashariki ambapo siku hiyo Nyota Ndogo na Kidum walibambisha sana tu. Ilikuwa ni jioni njema iliyojaa vionjo mbalimbali ambapo Kidum alipagawisha na miondoko yake iliyompatia umaarufu katika ukanda wote huu wa Afrika Mashariki. Nyota Ndogo naye akatupia nyimbo zake maarufu kama vile Nibebe na Watu na Viatu zenye miondoko ya pwani.

Hii ilikuwa ni fursa nyingine kwa Wakenya kupata mpumwende kutoka mirindimo ya makabila ya Kitanzania kama vile Wagogo, Wayao, Wamakonde na Wazaramo kupitia nyimbo kama Afrika, Che Maria, Shikandambwe, Mdundiko na Aichelelo. Hakika ilikuwa ni nafasi nyingine kwa utamaduni halisi wa Mtanzania kutangazwa bila ya aibu nje ya nchi yetu.

Shoo iliyofuata ilifanyika siku ya Ijumaa ya tarehe 1 May katika ukumbi mpya na wa kisasa ujulikanao kama Roof Top SunDowner uliopo maeneo yanayo karibiana na Ikulu hukoo Hullingham. Katika onyesho hili Leo alishirikiana vilivyo na wanamuziki maarufu wa Kenya wanaopiga vyombo kama vile Makadem ambayo anaimba na kupiga chombo cha asili kiitwacho Nyatiti. Vilevile alikuwepo mwanamuziki mkongwe Prasad ambaye anakung'uta ngoma za kiasili kutoka Bara Hindi zinazojulikana kama tabla. Ulikuwa ni mchanganyiko maalumu ambao wapenzi walifaidi kiingilio chao kikubwa walicho lipa ili kuona onyesha hilo kabambe na maalumu kabisa.

Katika mahojiano na Leo yaliyofanyika baada ya shoo hii, alieleza kuwa ziara hii imekuwa ni ya ya mafanikio ya hali ya juu sana na ameridhika na matokeo ya ziara hii.
"Matokeo ya ziara hii ni mazuri na makubwa sana. Mathalani, katika ziara hii nimeongeza wigo wa kufahamiana na wadau mbali mbali kutoka mataifa mengi zaidi. Faida nyingine ni kuweza kushirikiana na wanamuziki wengi zaidi wenye hadhi ya kimaitafa na nina shukuru kwa wao pia kupenda kazi yangu." alieleza Leo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...