Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete , Jumamosi, Agosti 29, 2013, ameungana na mapadre na waumini wa Kabisa Katoliki na wananchi wa mji mdogo wa Lugoba, Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, kusherehekea miaka 50 ya utawa wa Sista Perpetua Mlamwaza. 
 Rais Kikwete aliwasili kwenye Ukumbi wa Mkulima, Lugoba kiasi cha saa saba unusu mchana kuungana na wananchi hao katika sherehe ambako pia alikuwa anapongezwa Sista Ponsiana wa Paroko hiyo hiyo ya Lugoba kwa kufikisha miaka 25 ya nadhiri ya usista. 
 Miongoni mwa waliohudhuria sherehe hiyo ni pamoja na baba mzazi wa Sista Perpetua, Mzee Ariseni, pamoja na dada yake mkubwa na wadogo zake. Masista hao wawili wanatoka Parokia ya Lugoba, eneo ambako shughuli za Kanisa Katoliki ziliingia kiasi cha miaka 100 iliyopita na Sista Perpetua alikuwa msichana wa kwanza wa Paroko ya Lugoba kujiunga na utawa wa Kanisa Katoliki alipoweka nadhiri ya kwanza mwaka 1965 kuwa Mtawa wa Shirika la Moyo Safi wa Maria Mgolole na kuweka nadhiri ya kudumu, miaka tisa baadaye, mwaka 1974. 
 Katika risala yao kwa Sr Perpetua, wananchi wa Lugoba wamempongeza Sista huyo kwa “safari ndefu ya maisha ya kumtumikia Mungu kwa kuwa sababu safari hiyo siyo ya mchezo…ina mabonde na milima, furaha na machungu na yote wewe Sr umeyashinda yote hayo katika miaka 50 iliyopita. Tunakupongeza sana kwa kututoa kimasomaso” 
 Sista Perpetua mwenye umri wa miaka 72, alizaliwa katika Kijiji cha Msoga, Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani baba yake akiwa Mzee Ariseni na mama yake akiitwa Maria Nyau (Mama wa Mungu) ambao kwa pamoja walimpa binti yao jina la Marystella. 
 Akizungumza katika sherehe hizo, Rais Kikwete amempongeza sana Sr. Perpetua kwa ujasiri wake wa kuingia katika utawa katika kipindi na nyakati ambako uelewa wa watu wa eneo hilo ulikuwa tofauti sana na sasa. 
“Wakati huo, uamuzi wa namna hiyo haukuwa uamuzi rahisi hata kidogo. Ulikuwa uamuzi mgumu lakini dada yangu Perpetua aliufanya uamuzi huo.” 
 Aidha Rais Kikwete ameongeza: “Nakupongeza pia kwa kuchagua maisha ya kujinyima na kuwatumikia watu. Ungeweza kabisa kuchagua maisha ya kubadili magauni kila siku na kwenda saloni, lakini hukuyataka maisha ya namna hiyo. Umetuletea heshima sana kwa uamuzi wako huu. Tunakushukuru na kukupongeza.”
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na Sista.Perpetua(kushoto) aliyekuwa anaadhimisha miaka 50 ya utawa na Sista Ponsiana(kulia) aliyekuwa anaadhimisha miaka 25 ya utawa .Maadhimisho hayo yalifanyika katika kanisa Katoliki Lugoba jana. 
Picha na Freddy Maro

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...