Muogelaji nyota wa zamani wa dunia na mshindi wa medali ya dhahabu ya michezo ya Olimpiki kwa upande wa wanawake, Penelope “Penny” Heyns wa Afrika Kusini ataendesha mafunzo ya siku mbili ya kuogelea kwa makocha wa klabu maarufu ya mchezo huo hapa nchini, Dar Swim Club. 

Penny ambaye ni bingwa wa kihistoria wa michezo ya Olimpiki kwa staili ya ‘Breastroke’ atawasili nchini Alhamis akitokea  Afrika Kusini tayari kuendesha mafunzo hayo kwa makocha watano wa klabu hiyo. 
Katibu Mkuu wa Dar Swim Club, Inviolata Itatiro alisema jana kuwa maandalizi yamekamilika na klabu yao itagharimia mafunzo hayo kwa lengo la kuboresha viwango vya wachezaji wao na makocha kwa ujumla. 
Inviolata alisema kuwa makocha wao watakaoshiriki katika kozi hiyo kuwa ni Michael Livingstone, Ferick Kalengela, Radhia Gereza, Kanisi Mabena, Adam Kitururu, Simon Ngoya na Salum Mapunda. Alisema kuwa makocha wao wanasifa za ngazi ya juu ya ufundishaji wa mchezo huo, kutokana na kukua kwa kasi kwa mchezo huo, wameona bora wapate mbinu za kisasa ili kwenda na wakati. 
“Makocha wetu wote watano ni bora katika ufundishaji, waliwahi kupata mafunzo Dubai, Marekani na nchi mbalimbali, lakini klabu imeona kuendelea kuwapa mbinu zaidi ili kufikia malengo yetu ya miaka 10,”
 “Tunataka kuona kila mtoto anacheza mchezo wa kuogelea, tulianza na watoto wadogo ambao kwa sasa ni mastaa katika mchezo huo na kuweza kushinda medali mbalimbali nje ya nchi,” alisema Inviolata. 
Alisema kuwa wao wameamua kupromoti mchezo wa kuogelea kwa vitendo ili kuona siku moja watanzania wanafuzu kushindana michezo ya Olimpiki, Jumuiya ya madola na mashindano ya dunia siyo kupata nafasi za upendeleo kama ilivyo sasa. 
Alifafanua kuwa Penny alitwaa medali za dhahabu katika mashindano ya Olimpiki yaliyofanyika mjini Atlanta 1996 kwa mita 100 na 200 na wanaamini kuwa ujio wake utapandisha morali wachezaji wao na makocha. 
Wakati huo huo; klabu hiyo imeendesha zoezi la ukusanyaji fedha kwa ajili ya kufanikisha semina hiyo na kufikia lengo lake. Inviolata alisema kuwa zoezi hilo limefanikiwa kutokana na msaada wa wadhamini mbalimbali ambao ni Best Western (Coral Beach Hotel), Euopcar, Butcher Shop Dar es Salaam, CapeTown Fish Market, Warere, Lemon Spa,Pyramid Consumers, Instyle Hair and beauty salon, Coca Cola, Zen Spa, Karambezi Cafe, The Water Front na Southern Sun Dar es Salaam. “Nawapongeza watu waliochangia na kufanikisha zoezi hili, makocha na waogeaji wetu watapata mafunzo bure na si kwa kuwabana wazazi au walezi wao kama ilivyokuwa awali,” alisema Inviolata.

 Penny mara baada ya kushinda medali katika mashindano ya Olimpiki
 Meneja wa hotel ya Coral Beach, Glynis Markus (katikati) akimpa zawadi maalum Katibu Mkuu wa klabu ya Dar Swim Club, Inviolata Itatiro (kulia) baada ya klabu hiyo kuwa mabingwa wa jumla wa mashindano ya Taliss 2016. Kushoto ni mratibu wa shighuli hiyo, Deidre De Wet.

Meneja wa hotel ya Coral Beach, Glynis Markus (kulia) akimpa zawadi maalum  kocha mkongwe wa mchezo wa mchezo wa kuogelea wa klabu ya Dar Swim Club, Ferick Kalengela wakati wa hafla ya kutunisha mfuko wa timu hiyo ili kuendesha semina ya makocha na wachezaji wao iliyopangwa kuanza Ijumaa ijayo. Wengine katika picha ni makocha na waogeaji wa timu hiyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...