Na
Teresia Mhagama, Mtera
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo ameeleza kuwa Mameneja wa Shirika la umeme nchini (TANESCO)
wanaosimamia Kanda mbalimbali nchini wataondolewa katika vyeo hivyo iwapo
hawatatimiza maagizo mbalimbali waliyopangiwa na Wizara ya Nishati na Madini
ifikapo Machi 1 mwaka huu.
Waziri wa
Nishati na Madini alisema hayo wakati wa kikao chake na watendaji wa Shirika la
Umeme nchini (TANESCO) na Taasisi nyingine zilizo chini ya Wizara ya Nishati na
Madini kilichofanyika katika Kituo cha kuzalishia umeme cha Mtera.
Profesa Muhongo alitaja maagizo hayo kuwa ni
kuunganisha umeme kwa wateja wengi, kuwa na makusanyo makubwa ya bili za umeme,
kupunguza manung’uniko ya wananchi katika huduma za umeme na uboreshaji wa
mawasiliano kati ya Shirika hilo na wananchi.
“Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, ifikapo Machi
Moja mwaka huu atatuthibitishia kama Mameneja hawa wataendelea na majukumu haya
wanayoyasimamia ama la na hii itatokana na ufanisi wa utendaji katika majukumu tuliyowapangia,”
alisema Profesa Muhongo.
Aidha, Waziri wa Nishati na Madini alisema kuwa
Kitengo cha Uwekezaji cha Tanesco kama hakitakuwa na miradi mipya ya umeme
ifikapo tarehe 2 Aprili mwaka huu, watendaji katika Ofisi hiyo wataondolewa katika nafasi hiyo kwa
kushindwa kutimiza majukumu yake ipasavyo.
“Hapa hatuna mzaha kwani mahitaji ya umeme ni
makubwa na tuna miradi mingi ya usambazaji umeme kwa wanannchi ikiwemo miradi
ya REA na wananchi wanahitaji umeme kwa matumizi ya majumbani na kuanzisha
viwanda vidogodogo, sasa bila miradi mipya ya umeme tutashindwa kusambaza umeme
kwa wananchi hawa kwa kuwa kiasi cha
umeme tulichokuwa nacho sasa bado
hakitoshi,” alisema Profesa Muhongo.
Profesa Muhongo pia aliwaasa Mameneja wa TANESCO
wa Kanda kuwakaribisha wawekezaji mbalimbali wa umeme ikiwemo miradi midogo ya
uzalishaji umeme wa maji ili nchi iwe na umeme wa kutosha na sio kuwakatisha
tamaa wawekezaji hao.
Vilevile Profesa Muhongo alisema kuwa watumishi watakaoleta urasimu katika
kujadili masuala ya uwekezaji wa nishati wataachia ngazi kwani ndio
wanaokwamisha juhudi za serikali katika kuongeza kiasi cha umeme nchini.
“TANESCO na
EWURA kwa sasa pale anapojitokeza mwekezaji wa miradi ya umeme lazima mjadiliane
naye kwa pamoja badala ya mwekezaji husika kwenda TANESCO baadaye anaenda EWURA
au TPDC hivyo mwekezaji anapokuja jadilini naye kwa pamoja ili msitumie muda
mrefu katika utekelezaji wa suala moja
na hivyo kuchelewesha utekelezaji wa miradi mbalimbali,” alisema Profesa
Muhongo.
Vilevile Profesa Muhongo aliwaagiza watendaji wa TANESCO katika vitengo vya ukaguzi kufanya
kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa ikiwemo usimamizi madhubuti wa nguzo za umeme
ambazo baadhi huanguka kila inapofika msimu wa mvua na kusema kuwa suala hilo
halikubaliki.
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (aliyesimama) akizungumza na
watendaji mbalimbali wa Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi zilizo chini ya
Wizara wakati wa kikao chake na Watendaji hao kilichofanyika katika Kituo cha kuzalishia
umeme cha Mtera.Kulia ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard
Kalemani na kutoka kushoto (mstari wa mbele)
ni Kaimu Kamishna wa Nishati na Maendeleo ya Petroli, Mhandisi Norbert
Kahyoza, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Mhandisi Juliana
Pallangyo na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa.
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (aliyesimama) akizungumza na
watendaji mbalimbali wa Taasisi zilizo chini ya Wizara wakati wa kikao chake na
Watendaji hao
kilichofanyika katika Kituo cha kuzalishia umeme cha Mtera. Kushoto kwa Waziri
ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani Kutoka kulia ni Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Zena Kongoi, Dkt.Wellington
Hudson, Mkurugenzi wa Mkondo wa Chini kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli
(TPDC), Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio, Mkurugenzi
wa Umeme, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA),
Mhandisi Anastas Mbawala na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Felix Ngamlagosi.
Watendaji
mbalimbali wa Taasisi zilizo chini ya Wizara wakiwa kwenye kikao na Waziri wa
Nishati na Madini Profesa Sospeter
Muhongo (hayupo pichani) kilichofanyika
katika Kituo cha kuzalishia umeme cha Mtera. Kutoka kulia ni Dkt.Wellington
Hudson, Mkurugenzi wa Mkondo wa Chini kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli
(TPDC), Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio, Mkurugenzi
wa Umeme, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA),
Mhandisi Anastas Mbawala na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Felix Ngamlagosi.
Katibu
Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa (aliyesimama) akizungumza
katika kikao
cha Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani) na
Watendaji wa Taasisi zilizo chini ya Wizara kilichofanyika katika
Kituo cha kuzalishia umeme cha Mtera.Wengine kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mkuu
wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Dkt. Lutengano Mwakahesya, Naibu Mkurugenzi
Kitengo cha Usambazaji na Huduma kwa Wateja Shirika la Umeme nchini (TANESCO),
Sophia Mgonja, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Felchesmi Mramba, na
Kaimu Kamishna wa Nishati na Maendeleo ya Petroli, Mhandisi Norbert Kahyoza.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...