Na
Veronica Simba
Serikali imetoa
ridhaa kwa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) kufanya uchimbaji wa madini hayo kwa
njia ya chini kwa chini (underground mining), sambamba na njia waliyokuwa
wakitumia awali ya uchimbaji wa wazi (Open Pit).
Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesaini Kibali kinachoruhusu Mgodi wa GGM
kufanya uchimbaji huo wa chini kwa chini, leo Machi 15 katika Ofisi za Makao
Makuu ya Wizara jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Uongozi
wa GGM kabla ya kusaini Kibali husika, Waziri Muhongo alimwambia Mkurugenzi
Mtendaji wa Mgodi huo, Terry MulPeter kuhakikisha wanatumia utaratibu wa wazi
katika kulipa ushuru wa huduma (service levy).
Alisema, wananchi,
hususan wanavijiji wanaoishi jirani na Mgodi huo wanayo haki kujua ni kiasi
gani kinalipwa na GGM kama ushuru wa huduma kwa ajili ya utekelezaji wa
shughuli za maendeleo katika vijiji vyao.
“Mtapaswa kuwasilisha
Mfano wa Hundi ya malipo, yenye kiasi cha fedha mlichotoa kwa jamii kila
mnapolipa ushuru wa huduma ili wananchi wajue ni kiasi gani mmelipa,”
alisisitiza.
Vilevile, Profesa
Muhongo aliongeza kuwa, wakati wa kukabidhi Hundi hiyo ya mfano, Naibu Waziri
wa Nishati na Madini ni lazima awepo kushuhudia zoezi hilo na kama sio yeye basi
atawakilishwa na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Madini.
Alisema, kiongozi
mwingine anayepaswa kushuhudia zoezi hilo la kukabidhi hundi ya mfano ya malipo
ya ushuru wa huduma kutoka kwenye Mgodi kwenda kwa jamii ni mmoja wa viongozi
waandamizi kutoka Serikali ya Mtaa husika.
Kabla ya kusaini
Kibali hicho, Profesa Muhongo aliwauliza Kaimu Kamishna wa Madini, Julius
Sarota na Kamishna Msaidizi wa Madini, Kanda ya Ziwa Viktoria Mashariki, David
Mulabwa kama Mgodi huo umekamilisha taratibu zote zinazopaswa ikiwa ni pamoja
na kulipa kodi na tozo mbalimbali za madini kwa wakati, ambapo viongozi hao
waliafiki.
“Taratibu zote za
kisheria ikiwa ni pamoja na masuala ya uhifadhi wa mazingira zimefuatwa
kikamilifu,” alisema Sarota. Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi Mulabwa
alimhakikishia Waziri kuwa amejiridhisha na sababu zilizotolewa na Mgodi huo
kuomba kibali cha kuchimba chini kwa chini na hivyo hana pingamizi kuhusu
ridhaa hiyo kutolewa kwao.
Naye Mkurugenzi
Mtendaji wa GGM, MulPeter, akijibu swali la Waziri kuhusu ulipaji wao wa kodi
na tozo mbalimbali kwa Serikali, alisema kuwa Mgodi huo umekuwa ukilipa kodi
zote stahiki kwa wakati.
“Kwa mwaka huu wa
2016 kwa mfano, tumelipa Dola za Kimarekani Milioni 21.6 kama mrabaha, tumelipa
Dola za Kimarekani Milioni 1.6 kama ushuru wa huduma na makadirio ya malipo ya
kodi ya mapato kwa mwaka huu ni Dola za Kimarekani Milioni 37,” alisisitiza.
Aidha, Waziri Muhongo
alitumia fursa hiyo kuutaka Uongozi wa Mgodi huo kufanya zoezi la utafiti wa
madini (exploration) na kubainisha maeneo ambayo yako ndani ya leseni yao
lakini hawatayatumia kwa shughuli za uchimbaji ili wapewe wananchi wenye
uhitaji kwa ajili ya kufanyia shughuli mbalimbali za kimaendeleo.
Waziri Muhongo
alisaini Kibali kinachotoa ridhaa kwa Mgodi wa GGM kufanya shughuli za
uchimbaji wa chini kwa chini kupitia Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, kifungu
cha 48 (3) kinachompa mamlaka hayo Waziri mwenye dhamana na Wizara husika.
Kibali hicho cha
kuchimba chini kwa chini kwa Mgodi wa Geita kitatumika katika Mashimo (Pit) ya
Star na Comet.
Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo (Kulia), akisaini Kibali cha kuuruhusu Mgodi
wa Dhahabu wa Geita (Geita Gold Mine – GGM) kufanya uchimbaji wa madini wa
chini kwa chini (underground mining) badala ya uchimbaji wa wazi (Open pit)
uliokuwa ukifanywa awali. Anayeshuhudia ni Mkurugenzi Mtendaji wa GGM, Terry
MulPeter. Kwa kibali hicho, sasa GGM watafanya uchimbaji kwa njia zote mbili.
Waziri Muhongo amesaini Kibali hicho Machi 15, 2016 Makao Makuu ya Wizara,
jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo (Kulia) akimkabidhi Mkurugenzi Mtendaji wa
Mgodi wa Dhahabu wa Geita (Geita Gold Mine – GGM) Terry MulPeter, Kibali cha
Mgodi huo kufanya uchimbaji wa madini wa chini kwa chini (underground mining).
Awali, GGM walikuwa wakifanya uchimbaji wa wazi pekee. Kibali hicho kimetolewa, Machi 15, 2016 Makao Makuu ya Wizara jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji
wa Mgodi wa Dhahabu wa GGM, Terry MulPeter (Kulia), akimsikiliza Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (Kushoto) wakati wa kikao baina
yake na Uongozi wa GGM, kabla ya kusaini Kibali kinachouruhusu Mgodi huo
kufanya uchimbaji wa chini kwa chini (Underground mining). Tukio hilo
limefanyika Machi 15, 2016 Makao Makuu ya Wizara, jijini Dar es Salaam.
Wengine pichani ni baadhi ya Viongozi na Maofisa Waandamizi wa Wizara.
Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati), akizungumza na Uongozi wa Mgodi wa
Dhahabu wa Geita (Geita Gold Mine – GGM) (Kushoto), kabla ya kusaini Kibali
kinachouruhusu Mgodi huo kufanya uchimbaji wa chini kwa chini (Underground mining).
Kulia ni baadhi ya Viongozi na Maofisa Waandamizi wa Wizara. Waziri amesaini
Kibali hicho Machi 15, 2016 Makao Makuu ya Wizara jijini Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...