Mwenyekiti wa Kampeni ya Okoa Tembo Bw. Shubert Mwarabu (katikati) akielezea kuhus Kampeni yao ya kuokoa Tembo wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika leo katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mjumbe wa Kampeni hiyo Bw. Lameck Mkuburo pamoja na Bw. Arafat Mtui (wa kwanza kulia).(PICHA NA BENEDICT LIWENGA-MAELEZO).

Na Anitha Jonas – MAELEZO

Taasisi isiyo ya kiserikali ya Okoa Tembo Tanzania imemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli kuteketeza ghala la meno ya tembo liliopo nchini kufuatia Tanzania kusaini mpango wa kuwalinda Tembo mwaka 2014 unaozuia uuzaji wa meno ya Tembo kwa muda wa miaka 10.
Ombi hilo limetolewa leo jijini Dar s Salaam na Mwenyekiti wa Kampeni ya Okoa Tembo Tanzania Bw.Shubert Mwarabu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Barua ya Wazi waliyomwandikia Mheshimiwa Rais.
Amesema Tanzania inafungwa na mkataba wa kimataifa wa biashara juu ya viumbe vilivyo hatarini kutoweka (Convetion on International Trade in Endangered Species-CITES) ambao unabainisha kuwa Tanzania kwa sasa haiwezi kuuza ghala lake la meno ya Tembo.

Amesema uhifadhi wa meno hayo unaigharimu serikali fedha nyingi na kufafanua kuwa kwa sasa Tanzania ina hifadhi kubwa ya meno ya Tembo yaliyokamamwa kutokana na ujangili.
“Tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa kasi yake ya utendaji tangu kuchaguliwa kwake,tunamuomba atekeleze lengo la tatu la kampeni yetu ya Okoa Tembo wa Tanzania kwa kuliteketeza hadharani ghala la meno ya tembo,tunaona hakuna haja ya kuendelea kuwa na ghala hili” amesema Bw.Mwarabu.
Amesisitiza kuwa ombi lao kwa Rais kutaka ghala la meno ya Tembo liteketezwe kutasidia kutuma ujumbe mzito kwa majangili na wafanyabiashara kuwa meno ya Tembo hayana thamani ya pesa kiasi cha serikali kuona wepesi kuteketeza hazina hiyo.
“ Tunataka ieleweke kwamba kuharibu ghala la meno ya Tembo kunatuma ujumbe mzito kwa majangili na wafanyabiashara kuwa meno ya Tembo hayana thamani ya pesa na kuwa ujangili ni kosa la jinai lisilokubalika” Amesisitiza.
Amesema ipo haya ya Tanzania kuunga mkono mpango wao wa kuteketeza ghala la meno ya Tembo kama inavyotarajiwa katika nchi ya Kenya ambayo inatarajia kuteketeza ghala lake la meno ya Tembo hadharani Aprili 30 mwaka huu.Amezitaja nchi ambazo zina mpango wa kuchukua hatua kama ya Kenya kuwa ni Ethiopia,Chad,Gabon, Mozambique na Congo.
Naye mmoja wa wajumbe wa Kampeni ya Okoa Tembo wa Tanzania Bw.Arafat Mtui akizungumza katika mkutano huo amesisitiza kuwa kuendelea kuwepo kwa ghala hilo nchini Tanzania kunawapa moyo wafanyabiashara haramu wa meno hayo kuona kuwa ipo siku biashara hiyo itaendelea tena.
Amesema Kampeni yao ya Okoa Tembo wa Tanzania inaendelea kusisitiza kuwa kuwa hatma ya Tembo wa Tanzania iko mikononi mwa watanzania, hivyo ni vema Serikali ikashirikiana na wadau mbalimbali kuchukua hatua madhubuti kuokoa viumbe hao walio hatarini kutoweka kwa ajili ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Maoni ya Okoa Tembo ni mazuri, lakini tunaweza kuyatumia maghara ya meno ya tembo kama chanzo cha fedha za kuwalinda tembo wetu kwa kuyafanya kuwa maeneo ya watu maarufu kutembelea kwa kiingilio na kusaidia kuchangia fedha kusaidia jitihada za uhifadhi ndani ya nchi.

    Naitwa Jonathan L. Kwiyega

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...