Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman
Na Lydia Churi- Mwanza.

Mahakama ya Tanzania inakusudia kuongeza idadi ya Majaji katika kanda yake ya Mwanza ili kuongeza msukumo wa kumaliza kesi za mauaji kutokana na kanda hiyo kuongoza kwa kuwa na kesi nyingi za mauaji nchi nzima.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za kimahakama katika kanda ya Mwanza, Jaji Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Mohamed Chande Othman amesema ataongeza idadi ya majaji katika kanda hiyo ili kesi hizo za mauaji zimalizike kwa wakati.

Jaji Mkuu pia ameiagiza Mahakama Kuu kanda ya Mwanza kuzipa msukumo maalum kesi za mauaji ili kuhakikisha zinamalizika mapema na kupunguza mlundikano wa kesi katika mahakama za Tanzania.
Awali akisoma taaarifa ya hali halisi ya kesi katika Mahakama Kuu kanda ya Mwanza, Jaji Mfawidhi wa kanda hiyo Mheshimiwa Robert Makaramba alisema kanda ya Mwanza ndiyo inayoongoza kwa kuwa na kesi nyingi za mauaji nchini ambapo hadi kufikia Aprili mwaka huu kuna jumla ya kesi 512 za mauaji.

Pamoja na mkakati wa Jaji Mkuu kuongeza idadi ya Majaji ili kumaliza kesi hizo, Jaji Mfawidhi wa kanda ya Mwanza alisema wameshachambua kesi hizo za mauaji ambapo Jaji Kiongozi pia aliahidi kuwaongezea jumla ya Majaji 11 ili waweze kusaidia kusukuma kesi hizo.

Jaji Makaramba alisema kati ya mwezi Juni na Julai jumla ya vikao 11 vinatarajiwa kukaa ili kusikiliza kesi 123 zilizopangwa kusikilizwa. Alisema kati ya kesi hizo, 35 ni zile zitakazosikilizwa kwa mara ya kwanza na kesi 88 ni zile zitakazosikilizwa mpaka mwisho.

Alisema endapo vikao hivyo vitafanyika kama ilivyokusudiwa vitasaidia kupunguza kesi zilizopo mahakamani kwa miaka mingi.

Hadi kufikia mwezi April mwaka huu, Mahakama Kuu kanda ya Mwanza ina jumla ya kesi 2771 za aina zote zikiwemo zile za Madai ya kawaida, Madai ya Ardhi na za jinai. Ili kuongeza kasi ya usikilizwaji wa kesi hizo, kila Jaji amepangiwa kusikiliza kesi 346. Kanda hiyo ina Majaji nane (8).

Jaji Mkuu wa Tanzania ameanza ziara katika kanda ya Mwanza inayohusisha mikoa ya Geita, Mwanza na Mara ambapo atakagua shughuli mbalimbali za kimahakama katika kanda hiyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...