Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na mke wa tajiri namba moja duniani na mwenyekiti mwenza wa Bill and Melinda Gates Foundation, Melinda Gates kwa pamoja wamelipongeza Shirika la Oxfam kupitia kampeni yake ya Grow kwa kufanya Shindano la Mama Shujaa wa Chakula kama moja ya mbinu za kumkomboa mwanamke mnyonge kiuchumi.

Wawili hao waliyasema hayo kwenye mdahalo uliofanyika Juni 29 mwaka huu katika bustani ya Hoteli ya Serena jijini Dar ambapo walikuwa wageni waalikwa waliopata fursa ya kuzungumzia jinsi ya kumuwezesha kiuchumi mwanamke mzalishaji na namna ya kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Akizungumza kwenye mdahalo huo, Melinda Gates alisema kuwa yeye kupitia Bill and Melinda Gates Foundation wamelenga kusaidia nchi nyingi hasa za ukanda wa Afrika Mashariki kama Tanzania katika kubadilisha maisha yao kwa kutengeneza fursa za ajira na kuwasaidia vitendea kazi.

Aliongeza kuwa kwa nchi kama ya Tanzania ambayo asilimia 25 ya mapato yake yanatokana na kilimo, taasisi yao imejikita katika kuwawezesha wakulima wadogowadogo ambao hata hivyo huwezi kuwaacha wakina mama kwa kuwa ndiyo wanaotoa mchango mkubwa kwenye sekta hiyo.

Akizungumzia kuhusu Shindano la Mama Shujaa wa Chakula, Melinda Gates alitoa pongezi zake za dhati kwa shirika la Oxfam na kuongeza kuwa, ikiwa nchi za Kiafrika hususan Tanzania itataka kupiga hatua lazima iwawezeshe kiuchumi wanawake kwa kuwa wao ndiyo wenye uwezo wa kubadilisha maisha yao na hilo ndiyo jambo muhimu zaidi. 


Naye Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ambaye alikuwa ni mgeni rasmi kwenye mdahalo huo alisema kuwa; kwa kipindi kirefu amekuwa mfuatiliaji wa mashindano hayo na kuahidi kuwa sera ya serikali ya awamu ya tano ni kuongeza vipaumbele kwa mwanamke kwa kutoa mianya kwa taasisi zinazomsaidia mwanamke ikiwemo shirika la Oxfam kupitia shughuli zake hasas shindano la mama shujaa wa chakula. “Nikiri tu kuwa nimekuwa mfuatiliaji mzuri sana wa shindano hili tangu zamani, naahidi kuwapa ushirikiano mkubwa kwenu kwa kila jambo kwa kuwa mnaisaidia sana serikali,” alisema Ummy.

Aidha mdahalo huo pia ulioongozwa na mwanaharakati, Maria Sarungi Tsehai ulihudhuriwa na wanaharakati wengine wa masuala ya jinsia akiwemo Mkurugenzi wa Msichana Initative, Rebecca Gyumi, Mwanaharakati wa Mtandao wa Masuala ya Kijinsia, Marjorie Mbilinyi, Mwezeshaji kutoka Forum CC, Faizal Issa na Mshindi wa Shindano la Mama Shujaa wa Chakula 2011, Anna Oloishuro.

Mwenyekiti mwenza wa taasisi ya Bill and Melinda Gates ya Marekani Bi. Melinda Gates akiongea na wadau mbalimbali na kulipongeza shirika la Kimataifa la Oxfam Tanzania kwa kuendesha Shindano la Mama Shujaa wa Chakula ambalo lengo kubwa ni kuwawezesha wakulima wadogo wadogo wanawake kufanikiwa katika Kilimo cha chakula na umiliki wa ardhi.
Mkurugenzi Mkazi wa Oxfam Tanzania Jane Foster akitoa neno la utangulizi wakati wa sherehe hiyo.
Waziri wa Afya,Jinsia,Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu akilipongeza Shirika la Kimataifa la Oxfam Tanzania kwa kuendesha Shindano la Mama Shujaa wa Chakula ambalo linaonesha changamoto za wazalishaji wa chakula wadogo ikiwemo umiliki wa ardhi.
Mshereheshaji katika Hafla hiyo Maria Sarungi Tsehai akiendelea kutoa muongozo.PICHA ZAIDI BOFYA HAPA 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...