Baadhi ya mitambo ya umeme katika kituo cha kupooza na kusambaza umeme kilichopo mkoani Singida. Hiki ni moja ya kituo kilichoboreshwa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji mradi wa ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha umeme ya msongo wa kV 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga (BackBone).

Na Teresia Mhagama / Henry Kilasila

Imeelezwa kuwa takriban vijiji 121vilivyo kandokando ya njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovolti 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga (BackBone), vitaunganishwa na huduma ya umeme.

Hayo yalielezwa mkoani Singida na Meneja anayeshughulikia Umeme Vijijini katika mradi wa BackBone, Mhandisi Lewanga Tesha wakati Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipofanya ziara katika mikoa ya Dodoma, Singida na Shinyanga ili kukagua mradi huo.

Mhandisi Tesha alisema kuwa Mradi huo wa umeme vijijini unafadhiliwa na Serikali za Sweden, Norway na Tanzania ambapo utatekelezwa na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kwa kushirikiana na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhandisi Mathew Mtigumwe wakati alipofika katika Ofisi za Mkuu wa mkoa wa Singida, akiwa katika ziara ya kukagua mradi wa ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha umeme ya msongo wa kV 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga (BackBone).

Alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo utaanza mwanzoni mwa mwaka 2017 na kutarajiwa kukamilika ndani ya miezi 18 baada ya kuanza kazi rasmi.

Mhandisi Tesha aliongeza kuwa mikoa itakayofaidika na mradi huo ni Iringa, Dodoma, Singida, Tabora na Shinyanga.

“ Kwa mkoa wa Iringa vijiji vitakavyofaidika na mradi huu nii 25, Dodoma vijiji 31, Singida vijiji 40 na mikoa ya Tabora na Shinyanga vijiji 25,” alisema Mhandisi Tesha.
Meneja anayeshughulikia Umeme Vijijini katika mradi wa ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha umeme ya msongo wa kV 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga (BackBone), Mhandisi Lewanga Tesha (wa kwanza kulia) akimsikiliza mmoja wa wananchi mkoani Singida akitoa maoni yake wakati wa Ziara ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa pili kushoto)ya kukagua mradi huo.

Aliongeza kuwa jumla ya gharama zitakazotumika katika mradi huo wa kupelekeka umeme katika vijiji kandokando ya BackBone ni Dola za Kimarekani milioni 39.6.

Vilevile alisema kuwa tayari Mshauri Mwelekezi ameshateuliwa na mchakato wa kuwapata wakandarasi wa kazi za ujenzi unaendelea ambapo zoezi hilo linafanyika kwa ushirikiano kati ya TANESCO na REA.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema kuwa mradi huo wa kupeleka umeme vijijini hauhusiani na miradi ya REA ya upelekaji umeme vijijini na kwamba vijiji vingi zaidi katika mikoa hiyo vitapata umeme kupitia miradi ya REA, Awamu ya Tatu.
Kushoto ni baadhi ya nguzo kubwa (Towers) za msongo wa kV 400 zilizojengwa ikiwa ni utekelezaji mradi wa ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha umeme ya msongo wa kV 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga (BackBone). Kulia ni nguzo za awali za msongo wa kV 220.

Alitumia fursa hiyo pia kuwaeleza wananchi kuwa gharama za kuunganisha umeme vijijini katika miradi ya REA, Awamu ya Tatu inayotarajia kuanza mwezi Agosti mwaka huu, imebaki kuwa shilingi 27,000 kama ilivyokuwa katika miradi ya REA, Awamu ya Pili.

Aidha alisema kuwa katika mwaka huu wa Fedha (2016/2017), bajeti ya usambazaji umeme vijijini imekuwa ni ya kihistoria kwani zaidi ya shilingi Trilioni moja, imetengwa kwa ajili ya zoezi husika.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...