Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt John Pombe Magufuli akiwahutubia mamia ya wakazi wa mji wa Dodoma mapema leo asubuhi waliojitokeza kushuhudia maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa iliyofanyika kwenye uwanja wa Mashujaa, mjini Dodoma.PICHA NA MICHUZI JR-DODOMA






Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewasihi watanzania kuwaenzi Mashujaa kwa kudumisha Amani, Umoja na Utulivu uliojengwa na mashujaa hao.Rais Magufuli ametoa rai hiyo leo tarehe 25 Julai, 2016 wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya siku ya Mashujaa, yaliyofanyika katika uwanja wa Mashujaa Mjini Dodoma.

Pamoja na kutoa rai hiyo Rais Magufuli ameahidi kuwa atahakikisha azma ya Serikali kuhamia Dodoma inatekelezwa kabla ya kuisha kwa kipindi chake cha uongozi wa miaka mitano.

"Tunapoadhimisha siku ya Mashujaa hatuwezi kumsahau Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa alisema makao makuu yawe Dodoma, haiwezekani sisi watoto wake, sisi wajukuu wake tupinge kauli ya Mzee huyu.

"Kwa hiyo nilikwishazungumza na leo narudia hili katika siku ya Mashujaa, mlinichagua ndugu zangu wa Dodoma kwa kipindi cha miaka mitano, hadi sasa miezi minane imepita, nimebakiza miaka minne na miezi minne, nataka kuwathibitishia kuwa katika kipindi cha miaka minne na miezi minne iliyobaki nitahakikisha serikali yangu pamoja na mimi tunahamia Dodoma bila kukosa" Amesema Rais Magufuli.

Kufuatia maelekezo hayo ya Mhe. Rais, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ameagiza Mawaziri wote waanze mara moja kuhamia Dodoma na kwamba yeye mwenyewe atakuwa amehamia Dodoma ifikapo mwezi Septemba mwaka huu.

Viongozi wengine waliohudhuria maadhimisho hayo ni Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais Mstaafu wa awamu ya Pili Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson, Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Zubeir Ali Maulid, Mawaziri Wakuu wastaafu Mhe. John Samwel Malecela na Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda, Mabalozi na wanadiplomasia kutoka nchi mbalimbali, Viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama, Viongozi wa vyama vya siasa na dini, maafisa na askari waliopigana vita mbalimbali.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dodoma



25 Julai, 2016

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...