WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itahakikisha inalinda amani ya nchi kwa gharama zozote na kamwe haitoruhusu mwanasiasa yeyote kusababisha vurugu zitakazochochea uvunjifu wa amani.

“Hatuzuii kuwa na vyama vya siasa ila haturuhusu vurugu kupitia vyama vya siasa na hakuna jambo lisilokuwa na mipaka. Mambo ya kuhamasishana kufanya vurugu hatutayaruhusu, tunataka watu wafanye kazi,” alisisitiza.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumanne, Agosti 23, 2016) wakati akizungumza na viongozi wa dini pamoja na wazee wa mkoa wa Rukwa mara baada ya kuwasili mkoani hapa kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Sabasaba mjini Nkansi akiwa katika ziara ya mkoa wa Rukwa, Agosti 23, 2016.

Alisema Serikali inataka Watanzania wawe na uhakika wa kuendelea kufanya kazi zao za kuwaingizia kipato na kuwaletea tija, hivyo suala la kudumisha amani ni muhimu kwani vurugu zikitokea hawatakuwa na mahali pa kukimbilia na hakuna shughuli ya maendeleo itakayofanyika.

“Suala la uhamasishaji wananchi juu ya utunzaji wa amani ni la lazima hivyo viongozi wa dini na wazee kwa pamoja tushirikiane katika kukemea vitendo vya uchochezi kwasababu vurugu zikitokea Watanzania hatuna mahali pa kukimbilia,” alisema.

Aidha, Waziri Mkuu aliwaomba viongozi wa dini kuendelea kuliombea taifa pamoja na viongozi wake kwa sababu kazi ya uongozi ni ngumu na inachangamoto nyingi.Pia aliwaagiza viongozi wa dini wa mkoa wa Rukwa kuharakisha uundwaji wa Kamati ya Amani ya mkoa huo.

Awali, Sheikh wa mkoa wa Rukwa, Sheikh Rashid Akilimali amesema madhehebu ya dini hayawezi kuvuruga amani ya nchi ila anahofu na viongozi wa vyama vya siasa kutokana na vitendo vyao vya kuhamasisha vurugu.
Baadhi ya watumishi wa Halmashauri na mkoa wa Rukwa wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao kwenye ukumbi wa St Maurus mjini Sumbawanga Agosti 23, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Kufuatia hali hiyo Sheikh Akilimali aliwaomba wanasiasa nchini kutovuruga amani kwani machafuko yakitokea watashindwa kufanya ibada mbalimbali ikiwemo kufunga mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Sheikh Akilimali alisema kwa sasa wananchi wako huru kwenda kufanya ibada misikiti na makanisani kutokana na uwepo wa amani, hivyo aliwasisitiza wanasiasa kutothubutu kuichezea amani.

“Tafadhalini wanasiasa msituharibie amani ya nchi yetu. Amani haichezewi tunaona kwa wenzetu wanavyohangaika, wanaishi kwa tabu sisi hatujazoea  kukimbia. Sisi Watanzania ni moja na tunaishi kwenye nyumba moja hivyo hatuna budi kushirikiana kuilinda amani yetu,” alisema.

Kwa upande Katibu wa Wazee mkoani Rukwa, Kanali Mstaafu, John Mzurikwao alimuomba kiongozi huyo kuwasaidia  kutatua kero mbalimbali zinazoukabili mkoa huo zikiwemo za malipo ya pembejeo kwa mawakala wa kilimo pamoja na mgogoro wa ardhi katika shamba ya Efatha.

Waziri Mkuu alisema suala la malipo kwa mawakala wa pembejeo za kilimo linafanyiwa kazi na watalipwa baada ya Serikali kukamisha zoezi la uhakiki wa madeni hayo ili kujiridhisha kama kweli wakulima wapatiwa pembejeo na kwa kiwango gani.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Hatuzuii kuwa na vyama vya siasa ila haturuhusu vurugu kupitia vyama vya siasa na hakuna jambo lisilokuwa na mipaka. Mambo ya kuhamasishana kufanya vurugu hatutayaruhusu, tunataka watu wafanye kazi,”


    I COULD NOT HAVE SAID IT BETTER. THANKS PM. HAPA KAZI. HAKUNA SERIKALI SERIOUS INAYOWEZA KURUHUSU VURUGU KUPITIA VYAMA VYA SIASA. TUSIRUHUSU WAJARIBU KUTUHARIBIA NCHI

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...