Nyumbu ni Wanyama wanaopenda kusafiri kwa makundi makubwa kila mwaka, ni 'raia' halali wa Tanzania kwa kuzaliwa na kwa nasaba.

HAWANA vyeti vya kuzaliwa, wala hawajulikani hata mahali gani wanapotupa makondo yao ingawa ukifuatilia unaweza kuyaona, lakini Nyumbu (Wildebeest) wanaopatikana katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ni raia halali wa Tanzania.

Kwamba wanapatikana pia katika hifadhi ya Maasai Mara katika nchi jirani ya Kenya, katu hiyo haiwezi kuhalalisha uraia wao kwamba wanatokea huko. Ni bahati mbaya tu kwamba wanyama hawana pasipoti kama ambavyo hawana vyeti vya kuzaliwa, vinginevyo ushoroba (corridor) wanaoutumia ungewekwa kizuizi (Border Point) kama kile cha Sirari, Namanga, Tarakea, Holili na kwingineko hakika hati hizo zingethibitisha kwamba wanyama hawa huwa wanakwenda Kenya kutalii tu na kurejea tena nchini mwao Tanzania.

Kuweka mambo sawa ni kwamba, wanyama hawa wanapokwenda kwenye Hifadhi ya Maasai Mara, huwa wanakwenda kwenye 'fungate' kwa muda usiozidi miezi miwili na kisha kurejea kwao Tanzania kuendelea na maisha yao ya kawaida.
Maelezo haya yanathibitishwa na Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Serengeti, William Mwakilema, ambaye anasisitiza kwamba kauli zinazotolewa na wenzao wa Kenya kwamba wanyama hao wanapatikana nchini mwao na ni mali yao ni za upotoshaji mkubwa kimataifa

Hakuna mahali popote duniani ambako kuna uhamaji wa Nyumbu kama wa Serengeti kuelekea Maasai Mara ambao umekuwa miongoni mwa Maajabu Saba ya Dunia na hakika ndio umeifanya Serengeti kushika nafasi ya kwanza katika Maajabu Saba ya Asili ya Afrika mwezi Januari 2013; Kifupi tu ni kwamba moja ya sababu zinazofanya watalii wengi kuja nchini ni kushuhudia maajabu haya ingawa nabii hakubaliki kwao (si aghalabu kwa Watanzania).

Zaidi ya nyumbu milioni 2 uhama kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti nchini Tanzania kuelekea Hifadhi ya Maasai Mara nchini Kenya kutafuta malisho kati ya kipindi cha Julai na Oktoba.
Wanapohama ni lazima wakatize kwenye Mto Mara ambako hukumbana na mamba ingawa wengi hunusurika NA HAPA WAZEE HUTANGULIZWA KAMA CHAMBO......
Mwakilema anasema, wanyama hao wanapatikana katika Mfumo-asili wa Serengeti (The Serengeti Ecosystem), unaochukua eneo la kilometa za mraba 40,000 huku wengi wa nyumbu hao wakiwa wale wenye manyoya meupe (Connochaetes tuarinus mearnsi) ambao wanapatikana pia katika sehemu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa upande wa kusini; Hifadhi ya Serengeti na Maswa Game Reserve pamoja na Hifadhi za Jamii zinazopakana.

Kwanini wanazalia Tanzania? Mbali ya kuwa Serengeti ndiyo makazi yao ya asili, lakini wanyama hao, na wengine wengi, hupenda kuzalia huko kwa kuwa ardhi ina madini ya kutosha ya fosforasi ambayo ni virutubisho muhimu kwa majani, hivyo kuwafanya ndama wanaozaliwa kupata nguvu muda mfupi baada ya kula majani hayo. Katika kipindi cha uzazi, Nyumbu wanaweza kuzaa ndama 8,000 kila siku, hivyo kuonyesha ni kwa nini hifadhi hiyo inao wanyama hao wengi zaidi.

Kutokana na tabia yao ya uhamaji, nyumbu huwa hawana uhusiano wa kudumu. Majira ya nyumbu kupandana ni wakati nyumbu madume wanapotengeneza himaya na kuwavutia majike. Himaya hizi ndogo huwa zinaanzia meta za mraba 3,000, ambapo ndani ya kilometa moja ya mraba kunaweza kuwepo himaya 300. Madume yanalinda himaya zao zisiingiliwe na wengine na kuwaita/tongoza majike.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Mbona sisi kila siku walalamikaji tu kuhusu upotoshwaji wa watani wetu? Hatujiulizi kwanini? Kuna kitu hatufanyi wenyewe. Hili halihitaji sayansi ya nuklia kutambua. Sisi kazi yetu imekuwa kunungunika tu wakati wenzetu wanajitangaza vizuri ndani na nje ya Nchi yao. Dunia ya leo huwezi kutegemea rehema za Myenzi Mungu pekee. Vinginevo hatutekelezi azma yetu, Hapa Kazi Tu. Tuamke tufanye kazi.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...