Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Nicodemas Mushi (kushoto) akimkabidhi tuzo kwa niamba ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa shirika hilo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye (kulia) iliyotolewa na TTCL kwa mwanariadha, Alphonce Simbu aliyefanya vizuri katika mashindano ya Olimpiki 2016 yaliofanyika jijini Rio De Jeneiro nchini Brazil hivi karibuni. Wengine wanaoshuhudia ni baadhi ya viongozi wa vyama vya riadha Tanzania.
Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Nicodemas Mushi (kulia) akimkabidhi tuzo mwanariadha, Alphonce Simbu aliyefanya vizuri katika mashindano ya Olimpiki 2016 yaliofanyika jijini Rio De Jeneiro nchini Brazil kwa niamba ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL. Wanaoshuhudia katikati ni baadhi ya wanariadha waliyoiwakilisha Tanzania katika mashindano hayo. 
Kushoto ni wachezaji wa timu ya Taifa Tanzania walioshiriki katika mashindano ya Olimpiki ya mwaka 2016 yaliofanyika hivi karibuni jijini Rio De Jeneiro nchini Brazil wakirejesha bendera ya taifa kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye (wa tatu kulia) kwenye hafla ya chakula cha jioni kuwapongeza wachezaji iliyofanyika jijini Dar es Salaam. 
Baadhi ya maofisa wawakilishi wa TTCL wakipiga picha ya pamoja na timu ya riadha iliyoiwakilisha Tanzania mashindano ya Olimpiki 2016 Rio, nchini Brazil.

KAMPUNI ya Simu Tanzania (TTCL) inafanya mazungumzo na vyama vya mchezo wa riadhaa nchini pamoja na wachezaji wa mchezo huo ili kuandaa mpango utakaowawezesha wanaridha kufanya mazoezi ya kutosha na hatimaye kufanya vizuri katika mashindano yao mbalimbali. Kauli hiyo imetolewa jana na Meneja Uhusiano wa TTCL, Nicodemas Mushi kwa niamba ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa shirika hilo alipokuwa akitoa tuzo kwa mmoja wa wanariadha, Alphonce Simbu aliyefanya vizuri katika mashindano ya Olimpiki 2016 yaliofanyika jijini Rio De Jeneiro nchini Brazil hivi karibuni. Mwanariadha Simbu alishika nafasi ya tano katika mbio za marathoni na kuvunja rekodi kwa wanariadha wa Tanzania. 


Kampuni ya TTCL mbali ya kutoa tuzo na fedha zitakazomsaidia mchezaji huyo akiwa mazoezini kwa sasa, imetoa fedha kidogo kwa washiriki wote wa mchezo huo ikiwa ni ishara ya kuwapongeza na kuwatia moyo kutokata tamaa ili waweze kufanya vizuri zaidi katika mashindano mengine yajayo. "...Kwa niaba ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dk. Kamugisha Kazaura TTCL tumejiunga na wadau wengine wa michezo katika kuwapongeza wanamichezo wa timu ya Taifa ya Tanzania walioshiriki mashindano ya Olimpiki 2016 yaliofanyika jijini Rio De Jeneiro nchini Brazil, TTCL kwa nafasi yetu tumejiweka mstari wa mbele katika kuwasaidia wanamichezo wa riadha, tumejitolea kufanikisha timu ya riadha katika kukaa vizuri kimichezo..," alisema Mushi. 

"...Katika kipindi hiki cha michezo 2016 tumejitolea kuifanikisha timu ya riadha kuweza kushiriki vizuri katika programu za mazoezi, leo wakati wanarejea tumewaunga mkono kwa kutoa tuzo na fedha kwa msindi aliyefanya vizuri mwaka huu na pia kutoa fedha kwa wanamichezo wetu zitakazo wawezesha kufanya vizuri katika mazoezi yao, huu ni mwanzo lengo letu ni kwamba tutaweka utaratibu mzuri wa kuzungumza na vyama pamoja na taasisi zinazosimamia michezo hii ili kuona tunatengeneza utaratibu mzuri zaidi ambao ni endelevu utakaosaidia kukua kwa mchezo huu," 

alisisitiza meneja uhusiano huyo. Tuzo ya TTCL kwa Alphonce Simbu na fedha kwa wanariadha hao zilikabidhiwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ambapo aliwapongeza wanamichezo wote wa timu ya tanzania iliyokwenda nchini Brazil kwenye mashindano ya Olimpiki 2016 kwa uzalendo waliouonesha kwa taifa licha ya changamoto anuai. Waziri Nnauye aliwaomba Watanzania kutowakejeli wanamichezo hao kwa maneno ya kuwakatisha tamaa na badala yake kuungana kuwapongeza na pia kutoa ushauri kwa wadau wa michezo ili Tanzania iweze kufanya vizuri katika mashindano yajayo, ikiwa ni pamoja na vyama vya michezo kusaidia kyuongeza idadi ya wachezaji wa timu ya Tanzania. 

Kampuni ya Multichoice Tanzania pia iliungana na TTCL na kuwazawadia ving'amuzi vya DSTV vilivyolipiwa kwa muda wa miezi sita wanamichezo wote wa timu ya Tanzania iliyoshiriki katika mashindano ya Olimpiki mwaka 2016, pamoja na kumsaidia kumuwezesha mwanariadhaa Simbu programu za mazoezi kwa muda wa mwaka mmoja akiwa kama balozi wa kampuni hiyo. Timu ya Taifa ya Tanzania iliyoshiriki katika mashindano ya Olimpiki mwaka 2016 ilikuwa na wanamichezo saba, ambapo wanamichezo wanne walishiriki riadha, wawili waogeleaji na mmoja alishiriki mchezo wa judo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...