Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Madini, Profesa James Mdoe (kushoto kwa Waziri), wakifuatilia majadiliano yaliyokuwa yakiendelea wakati wa Mkutano baina ya Wizara na wachimbaji pamoja na watumiaji wa makaa ya mawe, uliofanyika Agosti 24 wizarani, jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akifafanua jambo katika mkutano na wachimbaji pamoja na watumiaji wa makaa ya mawe (hawapo pichani) uliojadili changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo. Mkutano huo ulifanyika Agosti 24, mwaka huu, Makao Makuu ya Wizara, jijini Dar es Salaam. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Madini, Profesa James Mdoe.
Wajumbe mbalimbali walioshiriki Mkutano baina ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Wachimbaji pamoja na Watumiaji wa Makaa ya Mawe, wakifuatilia mijadala mbalimbali katika Mkutano huo uliofanyika Agosti 24 mwaka huu Makao Makuu ya Wizara jijini Dar es Salaam.

Veronica Simba na Devota Myombe.
SERIKALI imeziteua maabara za Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) na Shirika la Umma linalojishughulisha na tafiti mbalimbali pamoja na kutoa ushauri wa kitaalam kuhusu Viwanda (Tanzania Industrial Research and Development Organization – TIRDO), kupima na kuthibitisha ubora wa makaa ya mawe yanayozalishwa nchini.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema Maabara hizo za GST na TIRDO zitatumika kupima na kuthibitisha ubora wa makaa hayo pale inapotokea mgogoro wa kutokukubaliana kuhusu ubora wake baina ya wazalishaji na watumiaji wake.

Aliyasema hayo hivi karibuni jijini Dar es Salaam alipokutana na kuzungumza na wazalishaji na wamiliki wa Viwanda vinavyotumia makaa ya mawe nchini kuhusu changamoto wanazokabiliana nazo.

Maelekezo hayo ya Waziri Muhongo yalitokana na wasiwasi walioonesha baadhi ya wajumbe wa kikao hicho, hususan watumiaji wa makaa ya mawe, ambao wamekuwa wakilalamika kuwa madini hayo yanayozalishwa nchini hayana ubora unaotakiwa na hivyo kuagiza kutoka nje ya nchi, kabla ya hivi karibuni kuzuiwa na Serikali na kuwataka wanunue yanayozalishwa hapa nchini. 

Akitoa maelekezo kuhusu utaratibu utakaotumika, Profesa Muhongo alisema kuwa, pande zote mbili, yaani wazalishaji na watumiaji wanapaswa kuwa na maabara zao ambazo zitatumika kupima ubora wa makaa husika.

Alielekeza kuwa, kabla ya kupeleka mzigo wa makaa ya mawe kwa watumiaji, wazalishaji wanapaswa kupima ubora wake katika maabara zao na kuweka alama inayoonesha ubora husika juu ya mzigo.

Aidha, kwa upande wa watumiaji, Waziri Muhongo alielekeza kuwa, wanapopokea mzigo husika, wanapaswa kuupima katika maabara zao, kabla ya kuutumia ili kujiridhisha kuhusu ubora wake kama ambavyo utakuwa umeainishwa katika alama iliyofungwa juu ya mzigo.

“Mkijiridhisha kuwa makaa ya mawe mliyopokea yana ubora unaotakiwa, mtapaswa kusaini kuthibitisha hilo na endapo mkigundua kuna tofauti, mna haki ya kutokusaini na kutokuyatumia makaa hayo,” alifafanua.

Waziri Muhongo aliongeza kuwa, endapo itatokea mgogoro wa kutokuelewana kuhusu ubora wa makaa yaliyowasilishwa na mzalishaji kwa mtumiaji, pande hizo mbili zitapaswa kutoa taarifa serikalini kupitia kwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, anayeshughulikia Madini, Profesa James Mdoe, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati iliyoundwa kushughulikia migogoro katika sekta husika.

Alisema kuwa, suala husika likifikishwa serikalini, Mwenyekiti atasimamia zoezi la upimwaji wa makaa husika katika moja ya maabara zilizoteuliwa, ambazo ni GST na TIRDO ili kuthibitisha ubora wake na hivyo kufikia muafaka.

Waziri Muhongo aliwataka wazalishaji na watumiaji wa makaa ya mawe kuacha manung’uniko yasiyo na tija na kila upande utimize makubaliano yaliyofikiwa katika vikao vyote vya awali na kwamba, Serikali kwa upande wake, itatimiza wajibu wake ipasavyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...