Baraza la Taifa la Uwezeshaji wananchi Kiuchumi (NEEC) limetoa onyo kali kwa taasisi au watu binafsi wanaowatoza wananchi fedha kama ada ya usajili wa vikundi vyao vya kijasiriamali kwa madai ya kuwawezesha kuwa na sifa ya kupata Tshs milioni 50 kwa kila kijiji zilizoahidiwa na serikali ya awamu ya tano.
Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Bi. Beng’i Issa alitoa onyo hilo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya taasisi au watu binafsi ambao wanafanya udanganyifu huo.
“Serikali haijatoa fedha hizi na zitakapo toka mpango huu utatekelezwa na serikali na siyo taasisi wala watu binafsi,” alisema jana jijini Dar es Salaam na kusema wanaofanya hivyo waache mara moja tabia hiyo.
Hadi sasa pamekuwa na taarifa za udanganyifu huo katika mikoa ya Lindi, Ruvuma, Mbeya, Tanga na Njombe.
Taasisi hizo na watu binafsi hao huvitoza vikundi hivyo vya wananchi kati ya Tshs 10,000 na Tshs 100,000.
“Taasisi au watu binafsi hawa wanadanganya wananchi kuwa wametumwa na baraza, jambo hili si kweli,” alifafanua.
Aliwataka wananchi kutoa taarifa kwa vyombo vya dola mara wanapobaini taasisi au mtu binafsi anayewashawishi kutoa fedha hizo kama ada ili vikundi vyao viweze kusajiliwa na kufaidika na fedha za kila kijiji.
Kwa mujibu wa Bi. Issa, fedha kwa kila kijiji zitatolewa kwa kukopesha vikundi vya wajasiriamali kupitia vyama vya ushirika vya akiba na mikopo (SACCOS), Vikundi vya Kifedha vya Jamii (VICOBA) na vikundi vingine ili viweze kuanzisha au kuendeleza shughuli za kiuchumi.
“Ni vyema sheria na taratibu za nchi zikafuatwa,” alisema na kuongeza kuwa serikali ipo mbioni kukamilisha utaratibu wa utekelezaji wa mpango wa fedha hizo kwa kila kijiji na kwamba ukiwa tayari taarifa itatolewa rasmi kwa umma.
Katibu Mtendaji Baraza la Taifa la Uwezeshaji wananchi Kiuchumi (NEEC), Bi. Beng’i Issa akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuhusu taarifa za kuwepo kwa taasisi na watu binafsi wanaowatoza wananchi fedha kama ada ya kujisajili katika vikundi vya kijasiriamali ili wawe na sifa ya kupata Tshs milioni 50 kwa kila kijiji zilizoahidiwa na serikali ya awamu ya tano.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...