Serikali imesisitiza umuhimu wa kupanua ushirikiano wake na Japan katika nyanja mbalimbali ili kuleta tija kwa nchi zote mbili.
Hayo yalielezwa hivi karibuni na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipokutana na ujumbe kutoka Japan ulioongozwa na Rais wa Chama cha Uchumi na Maendeleo ya Afrika (AFRECO), Tetsuro Yano aliyeambatana na Balozi wa Japan nchini Tanzania, Masaharu Yoshida.
Ujumbe huo kutoka Japan ulimtembelea Waziri Muhongo ofisini kwake ili kujadiliana masuala mbalimbali ikiwemo uwepo wa fursa za uwekezaji na ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.
Waziri Muhongo alisema ushirikiano baina ya Tanzania na Japan ni wa kihistoria na ni wa muda mrefu ambao unapaswa kuendelezwa kwa manufaa ya nchi zote mbili.
Alisema Tanzania inaingia katika uchumi wa viwanda na hivyo unahitajika ushirikiano wa dhati kwenye nyanja mbalimbali ili kuifikia dhamira hiyo.
Aidha, Waziri Muhongo aliainisha baadhi ya maeneo ya ushirikiano kuwa ni uzalishaji na usambazaji wa nishati ya umeme; utafutaji wa mafuta na gesi; uchimbaji wa madini yaliyo katika kundi adimu (Rare Earth Elements) na kuwajengea uwezo vijana wa Kitanzania.
“Tanzania inaelekea katika uchumi wa viwanda na hivyo kuna uhitaji mkubwa wa nishati ya umeme; tunahitaji kushirikiana kuzalisha na kusambaza umeme; na tunahitaji ufadhili wa masomo ya elimu ya juu kwa vijana wetu,” alisema.
Kwa upande wake Yano alisema Japan ipo tayari kushirikiana na Tanzania na kwamba zipo kampuni nyingi za nchini Japan ambazo zimeonesha nia na zipo tayari kuwekeza nchini.
 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akijadiliana jambo na Rais wa Chama cha Uchumi na Maendeleo ya Afrika (AFRECO), Tetsuro Yano (kushoto). Katikati ni wakalimani wa ujumbe huo kutoka Japan.
 Wajumbe wa mkutano wakimsikiliza mkalimani wa ujumbe kutoka Japan, Tasmin Akbar (hayupo pichani). Upande wa kulia ni Maafisa kutoka Wizara ya Nishati na Madini na upande wa kushoto ni Ujumbe kutoka Japan.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa tatu kutoka kushoto) katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka Japan uliomtembelea ofisini kwake. Kulia kwake ni Rais wa Chama cha Uchumi na Maendeleo ya Afrika (AFRECO), Tetsuro Yano na kushoto kwake ni Balozi wa Japan nchini Tanzania, Masaharu Yoshida.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...