Na Abushehe Nondo na Sheila Simba - MAELEZO.

Serikali imesema kuwa iliamua kununua ndege mbili za abiria aina ya Bombadier Q400 kutoka nchini Canada kutokana na uhitaji wa huduma ya usafiri wa anga kwa safari za ndani ya nchi na mazingira halisi ya viwanja vya ndege vilivyopo nchini. 
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wakufunzi wa marubani katika chuo cha Taifa cha usafirishaji(NIT) 
Mbarawa alisema kuwa Serikali haikukurupuka katika kufanya maamuzi ya aina ya ndege za kununua badala yake imezingatia vigezo na malengo mahsusi ya kuhudumia usafiri wa ndani na kuboresha usafiri wa anga kupitia Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
“Serikali imeamua kununua aina hii ya ndege za Bombadier Q400 kutokana na hali halisi ya Viwanja vya ndege nchini kuwa vya Changarawe na lami kwa baadhi, huku lengo ni kutoa huduma za usafiri wa ndani” Alisema Profesa Mbarawa.
Mbarawa aliwataka Watanzania kuelewa nia ya Serikali yao ni kuhudumia wananchi hivyo watu wasipotoshe ukweli kuhusu ndege hizo kwani zimezingatia mambo mbalimbali ikiwemo suala la usalama na ufanisi katika uendeshaji wake.
Aliongeza kuwa ndege hizo zina uwezo wa kutua katika viwanja vingi hapa nchini kwani zinaweza kutua katika viwanja vyenye urefu wa kilomita 1.5 ambavyo ndio vingi nchini tofauti na aina nyingine ambazo hutua kwenye viwanja vyenye urefu zaidi ya kilomita mbili.
Prof. Mbarawa alibainisha sababu nyingine kuwa ni aliongeza uwezo mdogo wa ndege hizo katika kutumia mafuta ukilinganisha na aina zingine ambapo kwa safari ya kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza zitakuwa zikitumia Tani 1.7 za mafuta tofauti na aina nyingine zinazotumia hadi Tani 2.8 kwa safari moja.
Waziri Mbarawa pia alitumia fursa hiyo kukanusha uvumi ulionezwa kuwa ndege hizo zimenunuliwa katika kampuni ndogo isiyokuwa na sifa na kubainisha kuwa suala hilo siyo la kweli kwani kampuni hiyo imefanya biashara na nchini nyingi ikiwemo Ethiopia yenye ndege t19 aina ya Bombadier Q400 zilizotengezwa na  Kampuni hiyo.
Mpaka sasa tayari Serikali imeshafanya malipo ya ununuzi wa ndege hizo kwa asilimia 40 ambapo ndege hizo zinatarajiwa kuwasili nchi tarehe 19 septemba mwaka huu ambapo zitaanza safari ya kutoka nchini Canada tarehe 15 septemba mwaka huu kupitia nchini Uingereza.
Akizindua mafunzo hayo ya wakufunzi wa  marubani, Waziri Mbarawa aliwaasa Marubani ambao watahitimu mafunzo hayo  kuhakikisha wanazingatia suala na nidhamu na uadilifu katika sekta hiyo ya usafiri wa anga.
“Hatutaki kuwa na marubani ambao wana uwezo wa kazi lakini sio waadilifu,hakikisheni mnawafundisha marubani wanafunzi kuzingatia nidhamu na uadilifu katika sekta hiyo ya anga ambapo wakati mwingine Rubani anajijua anakasoro lakini bado anang’ang’ania kurusha ndege” alisema Prof.Mbarawa.

Aidha amesema kuwa Serikali itashirikiana na chuo hicho katika kutoa kozi za urubani ili kuakabiliana na changamoto ya ukosefu wa marubani nchini. 





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 7 mpaka sasa

  1. Ni wazo zuri la kufufua Air Tanzania. lakini muhimu ili ishindane na mashirika mengine ya ndani inahitajika kuwa na ndege zenye engine ya jet,na kubwa kidogo kushindana na fastjet ambao wanandege kubwa za uwezo wa kubeba abiria 150 na hii inakwenda Mwanza kwa saa moja wakati hizi za propeller engine ni masaa 2,mimi nafikiri inatakiwa kuwa na CRJ 200 ambazo watengenezaji ni hao hao na zinachukua abiria 50 lakini jet engine.lakini naunga mkono kwa asilimia mia bora kuwa na chetu lakini tatizo watendaji je watatunyanyua???

    ReplyDelete
  2. kupanda panga hilo, aah

    ReplyDelete
  3. The mdudu, safi sana awamu ya 5 chini ya Rais wetu mpendwa John Pombe Magufuli na serikali yake yote kwa ujumla mdogo mdogo tutafika mpaka kwenye ma hayo ma Boeing ila minaona zingekuwa chini ya management ya mashilika kama NSSF au PPF kwa sababu haya mashilika tunaziona kazi wanazo zifanya kwakua wapo makini sana

    ReplyDelete
  4. Mtoa maoni wa kwanza, kukujibu ushauri wako. Umwshamsikia Mh. Magufuli kasema mwakani 2017 Airbus mbili zitanunuliwa, hizo sio za "pangaboy"

    Jamaa anakwenda na hesabu zake. Sasa huko Newala utapeleka Jet engine???

    Kuweni na subira kidogo, miaka 30 imekwenda ATC inasota tu, jamaa anataka kufufua mnaaza kulaumu aina za ndege.

    Ahsanteni.

    Mdau MD

    ReplyDelete
  5. Safi sana, hivyo ndivyo tusonge mbele TANZANIA OYEE!!!

    ReplyDelete
  6. Kweli kabisa wadau tunaanza humu humu mwetu kwanza. Tatizo letu watz hatusikilizi na kutunza maneno ya ahadi au SERA ili utekezaji ukianza tusiwe wa kushangaa. JPM anaanzia chini kwenda juu au anaanzia ndani kwenda nje ya nchi. Hivyo tuwe na subira ambayo ina heri. Amekuja bwana kupanga na kutekeleza kwa uwazi sasa lawama za nini? . TUSUBIRI KIDOGO, boeing tutanunuatu.

    ReplyDelete
  7. Maelezo ya professa - waziri husuka aliyoyatoa juzi yapo wazi na yanajitosheleza (kasema kwa kuanzia tunanaza na ndege zenye uwezo wa kutua viwanja vingi na ambazo ni lahisi keudeshwa na shirika linalofufuka, break even inafikiwa na abilia 26 sasa ndege kubwa ukaipeleka kwa watani zangu Kigoma break even abilia 65 utawapata kila siku? hivyo ni sawa kabisa kuanza na hizo,wanaangalia capacity na soko lililopo vilevile miundo mbinu...tembeleane tovuti za mashirika makubwa kwenye fleet zao utaona hizo unazosema panga wanazitumia pia eg Ethiopian airline

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...