Hifadhi asili ya Mkingu ipo wilaya ya Muvemero Mkoani Morogoro. Hifadhi hii ni eneo muhimu sana kiutalii kutokana na upekee wake wa maisha ya viumbe, mimea pamoja na maisha ya binadamu kiujumla.

Hifadhi hii ina ukubwa wa hekta 26, 334 na imezungukwa na vijiji vitano ambavyo vipo ndani ya kata sita na tarafa mbili. Tangu kuanzishwa kwake Hifadhi hii mwaka 2016, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii chini ya Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania ( TFS) imekuwa ikihudumia hifadhi hii kutokana na kuwa na mimea na viumbe ambavyo ni vivutio pekee vya Utalii nchini ambavyo havipatikani mahali popote duniani.

Mhifadhi Mkuu wa Mazingira asili ya Mkingu, Bw. Abeid Kindo anasema kutokana na sifa hizo za kipekee zinazopatikana katika Hifadhi hiyo imekuwa na umuhimu wa aina mbili ambao ni umuhimu wa kidunia na umuhimu wa kitaifa, Katika umuhimu wa kidunia upo katika viumbe, mimea na wanyama.

Anasema hifadhi hii ina wanyama wenye uti wa mgongo 392 kati ya hao 32 hawapatikana mahali popote duniani isipokuwa ni Mkingu tu yaani ni endemic species. Aidha , alisema kuna vyura na ndege wanaopatikana katika hifadhi hiyo tu. Bw. Kindo anasema kuwa hifadhi hiyo imejaliwa kuwa na wanyama wanaotambaa 42 kati ya hao 14 hawapatikanimahali popote duniani isipokuwa Mkingu tu pamoja na aina ya ndege 214 kati ya hao ni aina nne ndio wanaopatikana katika hifadhi hiyo. Mbali na hiyo, Anasema kuwa ndani ya hifadhi kuna msitu unaotumika kwa masuala ya mila za Waluguru kuwa eneo hilo ni zuri sana amabalo nalo ni kivutio cha utalii ndani ya msitu huo

Mbali ya kupatikana kwa wanyama na mimea katika Hifadhi hiyo Bw, Kindo anaeleza kuwa kuna pango la Malolo ambalo wenyeji wa Mkindo wana historia kubwa ya pango hilo ambalo wenyeji hawataweza kusahau kwani kuna mwanaume mmoja aliiba mke wa Mtu akaishi naye ndani ya pango hilo kwa muda wa miaka 3 bila kujulikana kijini. Pango hilo lina vyumba mithili ya nyumba iliyojengwa.

Pia anasema kuwa nadni ya hifadhi hiyo kuna pango ambalo ukikaa nje kuna upepo unaotoka ndani unapuliza hiyo ni ishara tosha kuwa humo ndani ndani kuna uhai. Anabainisha kuwa hifadhi hiyo ina jiwe lenye alama za nyayo za binadamu, kwato za mifugo ikiwa hiyo ni ishara tosha kuwa maisha ya kale ya binadamu yalianzia ndani ya hifadhi hiyo. .

Aliongeza kuwa mbali ya mapango ndani ya hifadhi hiyo , kuna maporomoko Lusingizo yenye mita zaidi ya 50 , hadi hivi sasa kuna wawekezaji wamejitokeza ili waweze kuzalisha umeme katika kivuto hicho cha utalii. Pia kuna magofu ya kale ya Wajerumani ambayo waliishi ndani ya hifadhi kabla vita vya pili vya dunia na baada ya kuondoka kwa Wajerumani ilikuwa shule ya msingi ya kijiji cha Mafuta, na baada ya eneo hilo likatangazwa kuwa hifadhi , Shule ile ilitolewa na kujengwa kijijini.

Bw. Kindo anasema licha ya hifadhi hiyo kuwa na vivutio lukuki bado imekuwa ikitembelewa na idadi ya watalii isiyoridhisha licha kwa mwaka jana wameweza kupata watalii 75 kutoka Ujerumani, ‘’Tokea mwaka jana hadi hivi sasa tumeweza kuibua vivutio saba vya utalii na tunaendelea kufanya jitihada za makusudi ili kuhakikisha tunakuwa na vivutio vingi vya utalii ili tuweze kuwavutia watalii wa ndani na nje ya nchi ‘’.alisema Bw. Kindo

Aidha,Alisema Hifadhi hiyo ndio chanzo cha mto Wami, mto Ruvu na Mto Mkingu ambapo maji hayo yamekuwa yakitumika katika shughuli za kiuchumi kama vile kilimo,uvuvi,mazalia na makazi ya mimea na wanyama bila kusahau maji hayo ndiyo hutumika kuwanyesha wakazi wa Dare s Salaam na mikoa ya jirani

Amewataka wanafunzi wa vyuo mbalimbali wasisubili watafiti kutoka nje ya nchi kwenda kufanya tafiti katika Hifadhi hiyo badala yake wao wawe mstari wa mbele katika kuvumbua vitu vingi ambavyo vinapatikana katika hifadhi hiyo.

Huyu ni aina mojawapo ya chura ambaye hapatikani mahali popote duniani isipokuwa katika Hifadhi ya Mazingira asili ya Mkingu ambaye ni mojawapo ya kivutio cha utalii katika hifadhi hiyo. ( Picha na Lusungu Helela- Wizara ya Maliasili na Utalii)
Baadhi ya sehemu za kuvutia katika Hifadhi ya Mazingira Asili ya Mkingu ambayo ni njia mojawapo inayotumiwa na watalii kwenda kijiji cha Maskati kuangalia vivutio vya Utalii vinavyopatikana katika Hifadhi hiyo. ( Picha na Lusungu Helela- Wizara ya Maliasili na Utalii).
 Maporomoko Lusingizo yenye mita zaidi ya 50 yaliyoko katika Hifadhi ya Mazingira Asili ya Mkingu ambayo ni mojawapo ya kivutio cha Utalii katika Hifadhi hiyo, Hadi hivi sasa kuna wawekezaji wamejitokeza ili waweze kuzalisha umeme katika kivutio hicho cha utalii. ( Picha na Lusungu Helela- Wizara ya Maliasili na Utalii).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...