Baada ya kufanya uhakiki wa Wanafunzi Uongozi wa Mkoa wa Simiyu umebaini uwepo wa wanafunzi hewa 2331  katika shule za Sekondari za Mkoa huo.

Taarifa hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka wakati alipozungumza na Walimu Wakuu na Waratibu Elimu Kata mara  baada ya kuwakabidhi Vishikwambi (Tablets) vilivyotolewa na Shirika lisilokuwa la Kiserikali la EQUIP Tanzania kwa ajili ya utunzaji wa Takwimu muhimu za Sekta ya Elimu,.

Mtaka amesema kati ya Halmashauri sita za Mkoa huo, Ni Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi  tu ambayo haina wanafunzi hewa wakati Halmashauri ya Wilaya ya Busega ikiwa na wanafunzi hewa  110, Itilima  2137, Maswa 14, Meatu 125 na Halmashauri ya Mji wa Bariadi 439.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka akizungmza na Walimu wakuu na Waratibu wa Elimu wa Kata baada ya kuwakabidhi Vishikwambi vilivyotolewa na Shirika lisilo la Kiserikali la EQUIP Tanzania, kwa ajili ya kutunza kumbukumbu na tawimu sahihi za masuala ya elimu.

Kufuatia kuwepo kwa wanafunzi hewa Mkuu wa Mkoa huo amesema, Serikali Mkoani humo imepanga kufanya mabadiliko ya Wakuu wa Shule za Sekondari katika Mkoa mzima, wakati taratibu za kinidhamu zikiendelea kwa wakuu wa shule  waliotoa takwimu za uongo za wanafunzi katika shule zao, wakati kwa upande wa shule za Msingi, mabadiliko yatafanyika baada ya kumaliza mtihani wa darasa la saba.

Mtaka amesema kabla ya uteuzi wa wakuu wa shule na walimu wakuu utafanyika upekuzi (vetting) kwa wale watakaopendekezwa ili kujiridhisha kama wahusika wana sifa na uwezo wa kuendesha shule na kusimamia fedha za Serikali zinazopelekwa shuleni kwa ajili ya kugharama elimu ya bila malipo. 
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini (kushoto) akizungumza na Walimu wakuu na Waratibu wa Elimu wa Kata baada ya kukabidhiwa Vishikwambi na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka (katikati)vilivyotolewa na Shirika lisilo la Kiserikali la EQUIP Tanzania, kwa ajili ya kutunza kumbukumbu na tawimu sahihi za masuala ya elimu(kulia)ni Afisa Elimu Mkoa, Julius Nestory.

“ Serikali inaendelea kupelekea fedha moja kwa moja katika akaunti za shule, kwa hiyo mkuu wa shule au mwalimu mkuu ni afisa masuuli katika shule yake. Ipo haja kwa sisi kujiridhisha kama Serikali kuwa anayeteuliwa kushika nafasi ya kuongoza shule ana uwezo na sifa  ya uadilifu. Sitakuwa tayari kuona katika mkoa huu kuna walimu wakuu wazoefu wa kula fedha za Serikali na wakaendelea kuongoza shule” alisema Mtaka.

Akitoa shukrani kwa Shirika la EQUIP Tanzania, Mkuu wa Mkoa amesema Shirika hilo limekuwa msaada katika kutatua baadhi ya changamoto za Watendaji katika Sekta ya Elimu mkoani Simiyu ikwa ni pamoja na  kuwawezesha Waratibu Elimu Kata kwa kuwapa pikipiki na kuwapa fedha za mafuta shilingi 206,000 kwa kila mwezi pamoja na kutoa mafunzo kwa walimu wakuu na walimu wakuu wasaidizi.
Afisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa (kushoto) akipokea Vishikwambi kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka(kulia) kwa ajili ya Walimu Wakuu na Waratibu Elimu Kata wa Halmashauri hiyo.

Aidha, Mtaka amesema analishukuru shirika hilo kuona umuhimu wa kutoa vishikwambi kwa Walimu wakuu na Waratibu Elimu Kata ambavyo ameelekeza vitumike kutunza takwimu sahihi za kieleimu ikiwemo idadi ya walimu na wanafunzi.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini amewataka Walimu Wakuu na Waratibu Elimu Kata kuvitunza vishikwambi hivyo na kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa.
Afisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima Nelasi Mulungu(kushoto) akipokea Vishikwambi kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka(kulia) kwa ajili ya Walimu Wakuu na Waratibu Elimu Kata wa Halmasahuri hiyo.

Naye Mkuu wa EQUIP Tanzania Mkoa wa Simiyu, Phoebe Okeyo amesema Vishikwambi hivyo  vitawasaidia Viongozi wa Elimu ngazi ya Mkoa, Wilaya na kata kupata taarifa za masuala mbalimbali yanayofanyika shuleni.

“Sasa hivi mtegemee kupata taarifa sahihi katika sekta ya Elimu kwa sababu ya hivi vifaa tulivyovitoa leo, tumeanza kama pilot study kwa Mikoa ya  Simiyu, Shinyanga, Mara, Tabora, Dodoma,Lindi na Kigoma. Tunatarajia kuongeza mikoa ya Katavi na Singida Januari, 2017” alisema Okeyo.

Jumla ya Vishikwambi(tablets) 637 vimetolewa  kwa Walimu wakuu 516  na Waratibu Elimu Kata 121 kutoka Halmashauri zote sita za Mkoa wa Simiyu, ambapo  kila kimoja kina thamani ya shilingi 315,000/=.
Baadhi ya Walimu wakuu na Waratibu Elimu Kata wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka (hayupo pichani) mara baada ya kukabidhiwa Vishikwambi vilivyotolewa na Shirika lisilo la Kiserikali la EQUIP Tanzania, kwa ajili ya kutunza kumbukumbu na tawimu sahihi za masuala ya elimu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Huu ulaghai na ulaji wa hewa katika sekta mbalimbali unatisha

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...