Na: Lilian Lundo - MAELEZO
SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imewapangia vyuo wanafunzi   wa programu maalum ya ualimu chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) ambao hawakupata nafasi ya vyuo katika awamu ya kwanza, walioagizwa kuomba mafunzo kulingana na sifa zao kupitia Baraza la Taifa la Mafunzo ya Ufundi (NACTE).

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Leonard Akwilapo leo, jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa taarifa kuhusu wanafunzi wanaosoma stashahada maalum ya ualimu wa sayansi chuo kikuu cha Dodoma.

“Mtakumbuka tuliagiza kwamba wanafunzi ambao walikosa sifa za kujiunga na ualimu wa sayansi waliombwa kuomba mafunzo yanayolingana na ufaulu wao kupitia NACTE,  Lakini baada ya taarifa hiyo tulipokea maombi mengi kutoka kwa vijana hawa wakiomba kupangiwa vyuo moja kwa moja na Wizara, wizara imetafakari na kuamua nao wapangiwe vyuo vya Serikali,” alifafanua Dkt. Akwilapo.

Aliendelea kusema kuwa, wanafunzi ambao waliachwa awamu ya kwanza na kupangiwa katika awamu ya pili ni wanafunzi 290 ambao walikuwa wakisomea programu ya stashahada ya ualimu wa sekondari na wanafunzi 1,181 ambao walikuwa wakisomea stashahada ya ualimu wa msingi.

Dkt. Akwilapo amesema kuwa Wizara imeamua kuwapangia wanafunzi hao vyuo kutokana na kuonyesha nia ya dhati ya kusomea ualimu ambapo wanafunzi hao wamepangiwa vyuo vya ualimu vya Marangu na Tabora.

Aidha, Dkt. Akwilapo ameeleza kuwa wanafunzi hao watajigharamia masomo yao kulingana na viwango vya ada vilivyowekwa na Serikali. Pia amewataka kutembelea tovuti ya wizara ya hiyo ambayo ni www.moe.go.tz ili kuona vyuo walivyopangiwa.

Mnamo tarehe Mei 28, 2016 Serikali iliwarejesha nyumbani wanafunzi 7,805 waliokuwa wanasoma Stashahada Maalum ya Ualimu wa Sayansi na Hisabati katika Chuo Kikuu cha Dodoma. Katika mchujo wa awamu ya kwanza wanafunzi 382 ndio waliokuwa na sifa ya kuendelea na masomo chuo kikuu cha UDOM na wengine 4,586 walipangiwa vyuo vya ualimu vya Serikali.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...