Mzee Said Maohamed Mannoro, Mkazi wa wilaya ya Kilwa - Kivinje akitoa ufafanuzi kuhusu nafasi ya wazee na mchango wao katika maendeleo ya Taifa.

Na. Aron Msigwa – Dar es salaam.
Watanzania hususan vijana wametakiwa kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa vitendo kwa kufanya kazi kwa bidi, kulinda na kudumisha amani iliyopo na kufanya matendo yenye tija na manufaa kwa Taifa.

Wito huo umetolewa leo jijini Dar es salaam na Mzee Said Maohamed Mannoro, Mkazi wa wilaya ya Kilwa - Kivinje wakati akizungumza katika mahojiano maalum na mwandishi wa habari hii kuhusu nafasi ya wazee na mchango wao katika maendeleo ya Taifa.

Amesema yeye kama mzee anao wajibu wa kuwaeleza na kuwashauri vijana  kuepuka kutumika kama chanzo cha kufanya vitendo vinavyochochea vurugu na kusababisha uvunjifu wa amani iliyopo. 

“Mahali ambapo panahatarisha amani hakuna mjadala, suala la amani linapewa nafasi ya kwanza mambo mengine yanafuata, hata kama kungekuwa na jambo zuri namna gani linalotaka kufanyika linapohatarisha amani kwa upande mmoja au mwingine ni afadhali kuliacha” Amesisitiza mzee Monnoro.

Amesema kuwa maandamano yaliyopangwa kufanywa na baadhi ya vyama vya Siasa Septemba mosi hayana sababu ya kufanyika kwa kuwa yana ajenda ya kukosa uvumilivu kuhusu usahihi wa uongozi wa nchi hivyo ni vyema wananchi wakayaepuka kwa kuendelea na shughuli zao za kujiingizia kipato kwa kuwa amani haina mjadala.

Amesisitiza kuwa ni vyema viongozi wa vyama vya hivyo wakatumia njia zinazostahili kutafuta ufumbuzi wa kero zao kupitia mazungumzo ili kupata haki kuliko kuwahamasisha wananchi kuandamana na kupambana na vyombo vya dola na jambo ambalo mwisho wake ni kuleta vurugu zisizo na maana.

Aidha, amewaomba viongozi hao wawe na busara na waheshimu maisha ya watu wanaowaongoza pia waepuke kuwa na kiburi cha kujiona wao ni bora kuliko wanachama wao.

“Mimi nayezungumza hapa niko upande wa upinzani, yanapokuja mambo ya kitaifa hayanizuii kuzungumza kwa kuwa yana manufaa kwa taifa, nasema kiongozi yeyote anayewashawishi wafuasi wake waandamane bila sababu za msingi ni kosa na jambo hili ni kupungukiwa na busara” Amesema mzee Mannoro.

Amebainisha kuwa kiongozi asiyeheshimu wala kujali maisha ya wananchi wake na kujiona anajua kuliko wao hafai, anapoteza sifa za kuwa kiongozi akisisitiza kuwa watanzania wanayo fursa nzuri ya kuchagua mustakabali mwema wa Taifa lao kwa kuwa amani ya Tanzania haina mbadala.

Akifafanua kuhusu utendaji wa viongozi wa Serikali katika ngazi mbalimbali za Serikali kuanzia kijiji hadi Taifa amesema kuwa katika nafasi zao wanao wajibu wa kulisaidia Taifa kwa kuwa wasimamizi wa utekelezaji wa malengo yaliyopangwa.

 “Sote tunafahamu Serikali imekuwa ikitekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo ikiwemo suala la utoaji wa elimu bure haya ndiyo mambo ya msingi ya kufuatilia na kusimamia kwa kila kiongozi katika nafasi yake, tunapaswa kumsaidia Rais wetu kutekeleza malengo yake” Amesisitiza.

Kuhusu maboresho ya sekta ya elimu ameishauri Serikali na wadau mbalimbali kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya elimu hasa ujenzi wa madarasa na mabweni ili kuwawezesha wanafunzi wanaokaa mbali na shule hususani eneo analotoka la wilaya ya Kilwa Kivinje ili waweze kuondokana na tatizo la kutembea umbali mrefu.

 Ametoa wito kwa watanzania hususan vijana kujikita katika shughuli za kilimo na shughuli nyingine zinazoweza kuwaongezea kipato badala ya kupoteza muda mwingi katika masuala yasiyo na tija kwa maendeleo yao binafsi na taifa.

Amesisitiza kuwa Kilimo sio adhabu kwa kuwa yeye mwenyewe pamoja na uzee wake shughuli za kilimo zimemsaidia kujenga familia imara na kuendesha maisha yake akiamini kuwa utajiri wa kweli uko kwenye ardhi.

 “Kinachonigusa mimi ni maisha ya watu, nawaomba watumishi wa Serikali waliosomea mambo ya kilimo wafanye kazi kwa bidi, wawasimamie vijana wetu wanaolalamika mitaani kuwa hawana cha kufanya, tukiwajenga na kuwasimamia vijana wetu katika misingi ya uwajibikaji na kufanya kazi kwa bidii umasikini utaondoka” 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...