Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini Mhe. Salva Kiir Mayardit amemtumia ujumbe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki akimuarifu kuwa hali ya usalama katika nchi hiyo imeanza kutengemaa.
Rais Salva Kiir Mayardit amewasilisha ujumbe huo kupitia kwa Mjumbe wake Maalum Mhe. Aggrey Tisa Sabuni ambaye pamoja na kuwasilisha ujumbe huo amesema Sudani Kusini imekamilisha nyaraka za azimio la kuridia mkataba wa kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao umewasilishwa  tarehe 05 Septemba, 2016 katika makao makuu ya Jumuiya Jijini Arusha. 

Mhe. Aggrey Tisa Sabuni amesema Sudan Kusini ipo tayari kushirikiana na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika masuala mbalimbali yenye manufaa kwa wananchi ikiwemo biashara na uwekezaji na kwamba ni matumaini yake kuwa itapata ushirikiano mzuri.

Kwa upande wake Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na taarifa za kutengemaa kwa hali ya amani nchini humo na kwamba ni matarajio yake kuwa Sudan Kusini itajikita katika maendeleo ya wananchi wananchi wake.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amepokea ujumbe kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Pierre Nkurunziza ulioletwa na Mjumbe Maalum wa Rais huyo Mhe. Aime Laurentine Kanyana.

Katika ujumbe huo Rais Nkurunziza amesema hali ya Burundi ni shwari na kwamba wananchi wa Burundi wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.
Kwa upande wake Rais Magufuli amesema Tanzania yenye wakimbizi takribani 200,000 wa kutoka Burundi inafurahishwa na taarifa za kuwepo hali ya amani nchini humo.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
06 Septemba, 2016.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...