Msaragambo Neno msaragambo linamaanisha mfumo uliokubaliwa na jamii katika kitongoji, kijiji au kata wa kushirikiana katika kufanya kazi zenye faida kwa watu wote, maarufu kwa kazi za ujenzi wa taifa. Kwa kazi hizi ni za ridhaa zilipaswa kwanza zikubaliwe na wengi vinginevyo haikuwa rahisi mtu mmoja kuitisha wito wa kazi fulani na watu wengine kuja kuifanya.

Kazi hizi ambazo hata serikali ya awamu ya kwanza ilizikazania sana mara baada ya Tanganyika kupata uhuru, ni pamoja na ujenzi wa mashule, kuchimba visima vya maji, kuchimba barabara na kadhalika.
Upo ushahidi wa kutosha kuhusu Wapare walivyotumia mfumo huu na kupata maendeleo makubwa Wilayani mwao. Zipo barabara za Mwanga hadi Ugweno na Usangi; Ndungu hadi Mamba na Vunta; Hedaru hadi Mwala; Makanya hadi Chome,Mpirani hadi Bombo Song’ana,Gonja Maore hadi Vuje naVudee hadi Mbaga.
Hata hivyo, si barabara tu lakini zahanati, na shule nyingi zimejengwa na wapare wa wilaya za Same na Mwanga na kuinua kiwango cha maendeleo yao. Nakumbuka watu hawa si watu wapenda misaada ya mteremko ndiyo maana pamoja na kukabiliana na hali mbaya ya uhaba wa mvua mara kwa mara wamekuwa si watu wa kupiga yowe haraka. Kazi zilizofanywa kupitia utaratibu huu wa msaragambo ziliufanya Mkoa huu wa Kilimanjaro uongoze kwa maendeleo ya barabara nzuri, ujenzi wa shule nyingi hadi katika vitongoji.
Hivyo basi nashauri, ili kukabiliana vyema na maandamano yasiyo na tija kwa taifa ni heri kwa Serikali kuitisha Msaragambo tarehe ambazo wale wasiopenda maendeleo watakuwa wakiandamana. Serikali ibuni shughuli za maendeleo ambazo siku hiyo viongozi na wananchi watashirikiana kuzitimiza.
Watakaotaka kwenda kwenye maandamano waachwe waende na wapenda maendeleo wakachape kazi. Wakitoka kwenye maandamano watakuta maendeleo. Tena ingefaa kwa wale Wabunge wa Chama Tawala siku hiyo kila mmoja awe jimboni mwake na kufanya msaragambo. Kwa yale majimbo ya upinzani, mwenyekiti wa chama tawala na wale wagombea wanaolitaka jimbo wawe mstari wa mbele ili kuwaonyesha wananchi kwamba hapa ni kazi tu.

Mdau,
Theophani Celestine Ishika

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Tuachane na mambo ya kutengana ktk jamii.

    Kama ni kufanya msaragambo tufanye kwasababu tunataka kuleta maendeleo na siyo kwasababu tunataka kuwakomoa wale wanaotaka kuandamana.

    ReplyDelete
  2. Itisha msaragambo siku isiyo ya maandamano ili kuwapa wananchi wengi fursa ya kushiriki ili kuongeza tija na sio kuwagawa kwa misingi ya itikadi za kisiasa

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...