Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba 

Na Beatrice Lyimo-
MAELEZO, Dodoma.

Serikali imetoa kauli kuhusu hali ya chakula nchini na kusema kuna chakula cha kutosha pamoja na ziada ya asilimia 123. Ziada hiyo ya chakula inatokana na uzalishaji wa msimu wa mazao mwaka 2015/2016 ambao unapelekea upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2016/2017.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba leo mjini Dodoma alipokuwa akitoa kauli ya Serikali kuhusu hali ya chakula nchini.“Takwimu zinaonesha upatikanaji na mahitaji ya chakula nchini ni wa kuridhisha kwa kiwango cha utoshelevu wa ziada kwa asilimia 123” Dkt. Tizeba.
Katika kufafanua hali hiyo, Dkt. Tizeba amesema kuwa kulingana na takwimu zilizopo hali ya upatikanaji na mahitaji ya chakula nchini inautoshelevu wa ziada kwa asilimia 123 ambapo nafaka ni asilimia 113 na mazao yasio ya nafaka ni asilimia 140 ambapo viwango vya ziada kwa mazao yote ya chakula ni tani 3,013,515.
Dkt. Tizeba ameongeza kuwa Wakala wa Hifadhi ya Chakula ya Taifa (NFRA) inauwezo wa kuhifadhi jumla ya tani 246,000 ambapo kufikia Septemba 6, ilikuwa na akiba ya tani 67,506.920 za chakula kinachojumuisha mahindi, mpunga na mtama.
Pia amesema kuwa Serikali inaendelea na mpango wake wa kuiongezea NFRA uwezo wa kuhifadhi chakula katika kanda sita baada ya kupata mkopo wa dola za Kimarekani million 55 kutoka Serikali ya Poland ambazo zitatumika kujenga vihenge vyenye uwezo wa kihifadhi tani 190,00 na maghala yenye uwezo wa kuhifadhi tani 60,000.
Kuhusu muda wa Serikali wa kutoa vibali vya kuuza chakula nje ya nchi, Dkt Tizeba amesema kuwa lengo ni kutoa nafasi kwa Serikali kukamilisha taarifa ya tathimini ya awali ya uzalishaji wa mazao ya chakula kwa mwaka 2015/2016 na hali ya upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2016/2017. 

Mbali na hayo, Dkt Tizeba amesema kuwa katika kuboresha hali ya usalama wa chakula nchini, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi inapitia upya mfumo wa utoaji wa vibali vya kusafirisha chakula nje ya nchi ili kuwezesha ufuatiliaji wa karibu kuliko ilivyo sasa.
Aidha, Dkt. Tizeba amesema kuwa utoaji wa vibali vya kusafirisha mazao nje umejitokeza baada ya kuona chakula kinasafirishwa nje bila kufuata utaratibu maalumu ambapo wafanyabiashara wa nchi jirani walijihusisha kununua vyakula vikiwa bado mashambani kabla ya kuvunwa.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuhifadhi chakula cha kutosha kwa matumizi katika kaya ambapo ameitaka sekta binafsi kuendelea kushiriki katika kutoa masoko ya kununua na kuuza mazao katika maeneo yenye uhaba.
Kuhusu hali ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi inayoikabili dunia ikiwamo upungufu wa mvua , Dkt Tizeba amesema kuwa Serikali itaendelea na juhudi za kuhimiza na kupanua kilimo cha umwagiliaji mashambani kwa kuimarisha miundombinu iliyopo na uvunaji wa maji ya mvua ili kuongeza uzalishaji wa mazao wenye tija. 
Hata hivyo, Serikali inaendelea kuhamasisha na kuelimisha wafanya biashara kuuza unga nje ya nchi badala ya mahindi au mchele badala ya mpunga ili kuendana na Sera ya kuendeleza Viwanda nchini na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Taarifa hii ni muhimu sana kuzingatiwa.
    Tayari Mamlaka ya hali ya hewa imetoa matarajio mvua za vuli 2016, ikionesha kutokuwepo kwa mvua za kutosha. Hivyo hiyo akiba iliyopo inastahili kusimamiwa vizuri matumizi yake. Nakumbuka kilichotokea mwaka 1983/84 ambapo ninakumbuka shule za sekondari tulikula unga wa njano a.k.a unga wa njano na dagaa. na mahala pengine kama shinyanga watu walishindi maembe mabichi, n.k.

    Hongera sana waziri. Pata uhakiki zaidi na simamia.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...