Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) akiwa kazini akipitia taarifa za Mtumishi wa Umma mkoani Kagera .

Kuondoa Watumishi wasiostahili katika orodha ya malipo ya mshahara Serikalini ni kazi endelevu na inafanyika kwa kushirikiana na waajiri nchini. Katika makala hii Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) anaongea kuhusu hatua mbalimbali na kazi zilizofanywa na Ofisi yake.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) alisema hayo hivi karibuni katika kipindi cha mahojiano ya moja kwa moja katika Runinga ya Taifa (TBC) na kusisitiza waajiri wanawajibu wa kuondoa mtumishi yeyote asiyestahili mara moja.

“ Tumefanya zoezi mahsusi kuwaondoa kwenye orodha ya malipo ya mishahara watumishi wasiostahili.  Watumishi wanaoondolewa ni wale walioacha kazi, kufukuzwa kazi, kumalizika kwa muda wa ajira ya mkataba na kugombea nafasi za kisiasa. Kuanzia tarehe 01 Machi, 2016 hadi tarehe 20 Agosti, 2016 jumla ya watumishi 16,127 wameondolewa na   wasingeondolewa kwa wakati  wangeisababishia Serikali hasara ya Shilingi 16,014,697,390 kwa mwezi mmoja” Mhe. Kairuki aliainisha.

Alisema hatua zinachukuliwa kwa wote waliobainika kuhusika katika suala hilo ambapo hadi  tarehe 20 Agosti, 2016 jumla ya watumishi 839 walifikishwa Polisi na TAKUKURU ili kutoa maelezo; na  uchunguzi unaendelea hatimaye hatua za kisheria zichukuliwe kulingana  wa ushahidi utakaopatikana.
Waziri Kairuki alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba fedha zote zilizolipwa kwa watumishi wasiostahili zinarejeshwa Serikalini akibainisha kuwa toka mwezi Machi, 2016 hadi mwezi Julai, 2016 jumla fedha zilizorejeshwa ni Shilingi 14,403,046,089.27 na zoezi ni endelevu.

Waziri Kairuki alisema Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCIMS) unaimarishwa kulingana na mahitaji na kutaja maeneo yaliyoimarishwa ikiwamo; Uwezo wa kutambua na kuzuia kuajiriwa watu wenye majina yanayofanana; Kuongeza moduli ambayo inamwezesha mwajiri kufanya uhakiki wa watumishi kwa kutumia taarifa mbalimbali zikiwemo za Kitambulisho cha Taifa; Uwezo wa kuwaondoa kwenye orodha ya malipo ya mishahara watumishi waliofikisha umri wa kustaafu na ambao hawana mikataba; Kuongeza Moduli ya Utambuzi wa Kituo cha Kazi cha mtumishi (Service Delivery Point) na hilo limeanza kwa Idara za Afya, Elimu, Kilimo na Mifugo; na Wigo wa matumizi ya mfumo umepanuliwa ili kuwawezesha Wakuu wa Idara za Afya, Elimu (Sekondari/Msingi), Kilimo na Mifugo kutumia na kuona taarifa za watumishi walio chini yao.

Akiongea kuhusu mkakati wa kuboresha Maadili katika Utumishi wa Umma alisema pamoja na mambo mengine Serikali  inasimamia kukuza uelewa wa Maadili kwa Watumishi wa Umma kupitia mafunzo na kuendeleza ushiriki wa Asasi za Kiraia (AZAKI) katika kuhamasisha wananchi kuzingatia maadili na kuacha kutoa vishawishi kwa watoa huduma. Pia, kuhakikisha kila Taasisi ya Umma ina Mkataba wa Huduma kwa Mteja na dawati la kupokea, kushughulikia malalamiko na kutoa mrejesho kwa wananchi.

Waziri Kariuki aliongeza pamoja na ofisi yake kuhakikisha Watumishi  wa Umma wanatoa Kiapo cha Ahadi ya Uadilifu na kusimamia viapo hivyo, pia inaandaa Mfumo wa Kielektroniki unaojulikana kama “Watumishi Portal” ambao utakuwa na moduli ya kupokea malalamiko, maoni na kero mbalimbali kutoka kwa Watumishi wa Umma na kuhamasisha Taasisi za Umma kuwa na kituo mahususi cha utoaji huduma (One Stop Service Centre) ili kupunguza kero kwa wananchi wanaofuata huduma.

Eneo la Uwajibikaje hali ikoje?
Waziri Kariuki alisema Serikali imekuwa na utaratibu wa kupima utendaji wa Mtumishi Mmoja mmoja kwa kutumia Mfumo wa Wazi wa Mapitio na Tathmini ya Utendaji Kazi (OPRAS).

Hata hivyo, alisema “Serikali inalenga kuimarisha mfumo wa uwajibikaji katika ngazi ya Taasisi ili kuhakikisha Taasisi za Umma zinatekeleza majukumu yake ipasavyo kwa kuanzisha Mfumo wa Mikataba ya Utendaji Kazi katika Taasisi zote za Umma kuanzia mwaka wa fedha 2017/18”.
Alifafanua kuwa Mkataba huo ni makubaliano ya kimaandishi kati ya Taasisi za Umma na Serikali ambayo yatatekelezwa na Taasisi husika katika kipindi cha mwaka mmoja na Mkataba utajikita katika kupanga na kupima utendaji wa Taasisi na utakuwa na malengo, shabaha, vigezo na viashiria vya utendaji ambavyo vitatekelezwa na Taasisi katika mwaka  husika.
Waziri Kairuki alianisha kuwa Mkataba huo utaainisha wajibu wa Serikali katika kuwezesha Taasisi kufikia malengo na shabaha na utekelezaji wake utafanyiwa tathmini kila mwisho wa mwaka na matokeo yake kutangazwa kwa umma.

Miongoni mwa faida za mfumo huo ni kuziwezesha Taasisi za Umma kuimarisha uchaguzi wa vipaumbele katika ngazi ya Taasisi na upangaji mipango ya utekelezaji kila mwaka; kuimarisha ufuatiliaji na upimaji utendaji kazi; na kuimarisha uwajibikaji na uwazi.

 Usimamizi wa Maadili kwa viongozi wa Umma ukoje?
Itaendelea...

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...