Na Benedict Liwenga-WHUSM, Bukoba.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais,
Muungano na Mazingira, Mhe. January Makamba amewatoa wasiwasi waathirika
wa tetemeko la ardhi lilitokea Wilayani Bukoba Mkoani wa Kagera.
Mhe. Makamba ameyasema hayo leo mkoani
Kagera wakati wa ziara yake ya kutembelea maeneo mbalimbali yaliyokumbwa
na tetemeko hilo kwa lengo la kuwapa pole waathirika na kuwap ujumbe wa
Serikali kuhusu namna inavyojitahidi kuwasaidia waathirika hao.
Amesema kwamba, wananchi wasiwe na wasi wasi
kuhusu suala la kupatiwa misaada ya dharura kwani Serikali imejipanga
na bado inaendelea na zoezi la kufanya tathmini ya uharibifu uliotokea
ingawa zoezi la kuwapatia baadhi ya huduma za msingi linaendele.
“Tumekuja kutoa msaada kwa mji kwa ujumla
wakati tunapanga namna ya kusaidia katika masuala ya mazingira na
tambueni kuwa Serikali inawajali ndiyo maana kuna viongozi wakubwa wako
hapa na wengine wanazidi kuja”, alisema Mhe. Makamba.
Aliongeza kuwa, suala la kuwasaidia
waathirika wa tetemeko hilo limepewa uzito mkubwa na Serikali na suala
la kuchelewa kwa kutolewa kwa misaada kunatokana na umakini unaoendelea
kufanywa sasa hivi na Serikali ili kuwatendea haki waathirika pekee.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Misenyi Luteni Kanali
Denice Filangali Mwila amesema kuwa katika Wilaya yake sehemu
iliyoathirika zaidi ni Kata ya Minziro ambapo jumla ya nyumba 512
haziwezi watu kuishi,pia nyumba 1,524 zenye nyufa mbalimbali
zinazohitaji ukarabati, Taasisi za serikali 91 na taaisis 71 za watu
binafsi ikiwemo makanisa na misikiti imeathirika na tetemeko hilo.
Ameongeza kuwa tayari amepata msaada wa
Serikali katika tukio hilo kupitia Kamati ya Maafa ambapo jumla ya
maturubai 520 amepewa kwa ajili ya maeneo mbalimbali, chakula, blanketi
240 ambazo pia zimegaiwa kwa waathirika hao.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Bugandika
Bw. Amudi Migeyo amewataka wananchi wake kutobeza juhudi za Serikali
zinazofanywa sasa na amewataka kuridhika na chochote wakipatacho katika
kipindi hiki kigumu.
Hivi karibuni siku ya tarehe 10 Septemba,
2016 mkoa wa Kagera ulikumbwa na ukubwa wa nguvu za mtetemo wa ardhi wa
tetemeko la 5.7 kwa kutumia skeli ya ‘Ritcher’ ambapo jumla ya watu 17
walipoteza maisha na majeruhi kadhaa ambapo wengi wao wameshapatiwa
matibabu na wanaendelea vizuri.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. January Makamba (kushoto) akiwapa pole waathirika wa tetemeko la ardhi waliolazwa Hospitali ya Rufaa ya Bukoba leo 22/9/2016.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. January Makamba (kulia) akimpa pole Mwalimu Mkuu Shule ya Sekondari Ihunga Bw.Thomas Bonevanture mara alipowasili shuleni hapo kuwapa pole waathirika leo 22/9/2016.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. January Makamba (katikati) akiwa ameongozana na Mkuu wa Wilaya ya Misenyi Luteni Kanali Denice Filangali Mwila (kushoto) pamoja na Diwani wa Kata ya Bugandika Bw. Amudi Migeyo kwenda kuangalia maeneo yaliyoathirika na tetemeko la ardhi leo 22/9/2016 Wilayani Misenyi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. January Makamba (wa pili kushoto) pamoja na viongozi wengine wakiwapa pole baadhi ya waathirika wa tetemeko la ardhi Wilayani Misenyi leo 22/9/2016.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...