Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akitoa maelekezo kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Bw. Bernard Konga alipotembelea banda la upimaji afya katika Uwanja wa Taifa wakati wa Mechi ya Wabunge wa Simba na Yanga. 

Na Grace Michael
WAZIRI Mkuu Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa ameupongeza Mfuko wa Taifa wa Bima kwa kazi kubwa inayofanya ya kuwahudumia wanachama wake lakini pia kuendesha shughuli za upimaji wa afya bure katika maeneo mbalimbali.
Pamoja na pongezi hizo, ameutaka Mfuko huo kuangalia namna ya kuwafikia Watanzania wengi zaidi katika suala la upimaji wa afya ili kila mmoja ajue hali ya afya yake.
“Kwanza niwapongeze tu kwa kazi kubwa mnayoifanya hapa ya kutupima afya zetu...hakikisheni shughuli hizi zinafanyika mahali pengi zaidi kwani kwa sasa kuna mwamko mkubwa sana wa wananchi kupima afya zao, hata pale bungeni leteni huduma hizi wakati wa bunge ili waheshimiwa wabunge nao wapate fursa hii,” alisema Waziri Mkuu.
Alisema kuwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umekuwa msaada mkubwa katika usimamizi na utoaji wa huduma za matibabu kwa wanachama wake pamoja na uboreshaji wa huduma za matibabu.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi kujiunga na huduma za Mfuko ili kuwa na uhakika wa kupata matibabu wakati wowote wanapohitaji lakini pia kuhakikisha wanatumia fursa za upimaji wa afya zinapokuwa katika maeneo yao.
Naye Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Nape Nnauye akizungumzia zoezi la upimaji lililofanywa na NHIF uwanjani hapo, alisema kuwa ni jambo zuri kwa kuwa mbali na watu kujua hali ya afya zao lakini watapata elimu ya namna ya kujiunga na huduma za Mfuko.
Alitoa wito kwa vijana kuhakikisha wanajenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara ili kujua hali zao kwa kuwa ndio nguvu kazi inayotegemewa katika uzalishaji wa Taifa hili.
Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard Konga alisema kuwa, Mfuko umeendesha zoezi hilo uwanjani hapo kwa lengo la kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali hususan katika kushughulikia tatizo la janga la tetemeko lililotokea mkoani Kagera.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Nape Nnauye akipima uzito kabla ya mechi kuanza.
Katibu Mkuu wa Wizara y Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Gabriel akipima kiwango cha sukari katika banda la NHIF.
Mbunge wa Sengerema Bw. William Ngeleja akipima uzito kabla ya mtanange kati ya wabunge wa Yanga na Simba. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...