KAMPUNI ya mafuta ya Puma Energies Tanzania imejitosa kudhamini mashindano ya Rock City Marathon ambayo kilele chake kinatarajiwa kuwa Septemba 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Akikabidhi hundi yenye thamani ya sh milioni 15 (15,000,000/-) kwa msemaji wa kampuni ya Capital Plus International, Bw Mathew Kasonta ambae kampuni yake kwa kushirikiana na mkoa wa Mwanza ndio wanaandaa mbio hizo, Meneja Mkuu wa kampuni ya Puma Energies Bw Phillipe Corsaletti alisema udhamini huo unalenga kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu tano katika kuendeleza na kuhamasisha michezo hapa nchini.

“Lakini pia tumeguswa na malengo ya mbio hizi ambazo pamoja na mambo mengine zinalenga kupambana na ujangili pamoja na kutangaza utalii katika katika kanda ya Ziwa,’’ aliongeza. Aliahidi kuwa kampuni yake itaendelea kushirikiana na waandaaji wa mbio hizo katika kuboresha zaidi mbio hizo kwa miaka ijayo huku akitoa wito kwa vijana wengi zaidi kutoka mikoa mbalimbali kujiandaa na mbio hizo.

Akizungumzia zawadi za washindi wa mbio hizo Bw Mathew Kasonta alisema washindi wa kwanza wa mbio za kilometa 21 kwa wanaume na wanawake watajinyakulia sh. Mil 1.5/- kila mmoja, sh. 900,000/- kwa washindi wa pili na sh. 700,000/- kwa washindi wa tatu.

Kwa upande wa mbio za Kilometa tano ambazo zitaongowa na wakuu wa mikoa ya Mwanza na Simiyu ambazo pia zitahusisha wafanyakazi kutoka makampuni mbalimbali (Corporate) pamoja na watu wenye ulemavu wa ngozi yaani Albino, Mathew alisema washindi watapatiwa zawadi za heshima kwa makampuni huku pesa zilielekwa washiriki wenye ulemavu wa ngozi.

“Kubwa zaidi pia ni kuwashukuru sana wadhamini wa mbio hizi kwa kuendelea kutuunga mkono kwenye maandalizi haya yaani kampuni za Freidkin Conservation Fund na African Wildlife Trust, Benki ya NMB, New Mwanza Hotel, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Real PR Solutions, kampuni ya Fabec, Tiper, Puma Energies, Clouds Fm, Jembe Fm, Barmedas Tv na EF Out Door alitaja. Alitoa wito kwa washiriki zaidi kuendelea kujisajili ili kuthibitisha ushiriki wao kwenye mbio hizi.

“Kwa wakazi wa jiji la Mwanza na mikoa jirani wanaweza kujisajili kwa kuchukua fomu katika vituo kadhaa vikiwemo ofisi za michezo wilaya zote za mkoa wa Mwanza, Ofisi zote za riadha mikoa ya Geita, Simiyu na Shinyanga, Uwanja wa Nyamagana, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Mwanza, Kituo cha michezo Malya, Shule ya Kimataifa ya Isamilo, Mwanza Hotel.

“Kwa upande wa Dar es Salaam Fomu za ushiriki pia zinapatikana katika ofisi za Kampuni ya Capital Plus International zilizopo ghorofa ya tatu jengo la ATC, jijini Dar es, Salaam,” alihitimisha.

Meneja Mkuu wa kampuni ya Puma Energies Bw Phillipe Corsaletti (kushoto) akikabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya sh milioni 15 (15,000,000/-) kwa msemaji wa Rock City Marathon zinazoratibiwa na kampuni ya Capital Plus International (CPI) na Mkoa wa Mwanza, Bw Mathew Kasonta ikiwa ni udhamini wa mbio hizo wakati wa hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana.
Msemaji wa Rock City Marathon Bw Mathew Kasonta akizungumza mbele ya  waandishi wa habari kuhusu udhamini wa kampuni ya Puma Energy kwenye  Rock City Marathon ambapo waandaaji wa mbio hizo kampuni ya Capital Plus International (CPI) ilikabidhiwa kiasi cha sh milioni 15/- na kampuni hiyo . Wengine ni Meneja Mauzo reja reja kampuni ya Puma Energy Bw Machumani Shebe (Kushoto) na Meneja Mkuu wa kampuni ya Puma Energies  Bw Phillipe Corsaletti (katikati).
Meneja Mauzo reja reja kampuni ya Puma Energy Bw Machumani Shebe (Kushoto) akizungumza mbele ya waandishi wa habari kuhusu udhamini wa kampuni hiyo kwenye Rock City Marathon ambapo kampuni hiyo ilikabidhi kiasi cha sh milioni 15/- kwa waandaaji wa mbio hizo kampuni ya Capital Plus International (CPI). Wengine ni Meneja Mkuu wa kampuni ya Puma Energies Bw Phillipe Corsaletti (katikati) na msemaji wa Rock City Marathon   Bw Mathew Kasonta.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...