Wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu ambao hawajaanza kurejesha mikopo yao wamekumbushwa kutimiza wajibu wao kwa kurejesha mikopo hiyo ili iwanufaishe watanzania wengine ambao ni wahitaji.

Wito huo umetolewa na baadhi ya wabunge walionufaika na mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) katika hafla fupi ya kuwakabidhi vyeti baada ya kumaliza kurejesha mikopo yao iliyofanyika katika ofisi za HESLB mjini Dodoma jana (Septemba 1, 2016).

Akizungumza katika hafla hiyo, Mbunge wa Vwawa na Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma (PAC) Mhe. Japhet Hasunga alisema mahitaji ya kifedha ya Bodi ni makubwa hivyo kila mnufaika wa mikopo ana wajibu wa kurejesha ili iwanufaishe watanzania wengi wanaohitaji mikopo.

“Mimi nilinufaika katika mwaka wangu wa mwisho wa 1995 nikiwa chuoni Mzumbe na nimeamua kulipa kwa mkupuo nikijua kuna watanzania wengi wanahitaji kusaidiwa,” alisema Hasunga katika hafla hiyo fupi na kuwaomba wabunge wenzake walionufaika na mikopo kurejesha mikopo yao.

Kwa upande wake, Mbunge wa Biharamulo Magharibi Mhe. Oscar Mukasa aliishukuru Serikali kwa mkopo uliomuwezesha kupata elimu ya juu na kuhitimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1996 na kushauri vigezo vya utoaji mikopo vitoe kipaumbele kwa watanzania waliopo katika maeneo ya pembezoni mwa nchini.

“Na mimi nimemaliza kurejesha mkopo wote niliopewa na ninaishukuru Serikali ... lakini ninashauri vigezo vya utoaji wa mikopo vitoe kipaumbele kwa watanzania waliopo pembezoni kama Biharamulo,” alisema baada ya kukabidhiwa cheti chake na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru.

Katika hafla hiyo, mtumishi wa Mamlaka ya Ufundi Stadi (VETA) Bw. Richard Jafu naye alikabidhi wa cheti baada ya kurejesha kwa mkupuo mmoja kiasi cha Tshs 14.5 milioni alichokuwa anadaiwa baada ya kukopeshwa akiwa Chuo Kikuu cha Mtakatifu John cha Dodoma ambako alihitimu mwaka 2013.

Akizungumza katika hafla hiyo kwa niaba ya Bw. Jafu ambaye yupo mkoani Shinyanga kikazi, mfanyakazi mwenzake Bw. Gabriel Sikoi alisema uamuzi wa Bw. Jafu kumaliza deni lake ulisukumwa na uzalendo ili fedha hizo zitumike kuwakopesha wengine.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Bw. Badru aliwashukuru wadau hao kwa kutimiza wajibu wao na kuwasihi wanufaika wengine kujitokeza na kurejesha mikopo waliyopewa.

“Wito wangu kwa wanufaika wote ni kujitokeza na kurejesha mikopo, ikiwezekana kwa mkupuo mmoja au miwili au mitatu kulingana na uwezo,” alisema Bw. Badru aliyeteuliwa mwezi uliopita kushika wadhifa huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo Bw. Abdul-Razaq Badru akimkabidhi cheti cha kumaliza kurejesha mkopo wa elimu ya juu Mbunge wa Biharamulo Magharibi Mhe. Oscar Mukasa (kushoto) mjini Dodoma jana (Septemba 1, 2016). Kulia ni Mbunge wa Vwawa Mhe. Japhet Hasunga ambaye naye alikabidhiwa cheti baada ya kumaliza kurejesha mkopo wa elimu ya juu.
Mbunge wa Biharamulo Magharibi Mhe. Oscar Mukasa akizungumza katika mkutano na wanahabari mjini Dodoma jana (Septemba 1, 2016) baada ya kukabidhiwa cheti cha kumaliza kurejesha mkopo wa elimu ya juu. Wengine ni Mbunge wa Vwawa Mhe. Japhet Hasunga (kulia) ambaye naye alikabidhiwa cheti baada ya kumaliza kurejesha mkopo wa elimu ya juu na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo Bw. Abdul-Razaq Badru aliyekabidhi vyeti hivyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...