Na Teresia Mhagama, Manyara

Wakandarasi wote wanaofanya kazi ya wanaofunga nyaya za umeme ndani ya nyumba (wiring),  wametakiwa  kuhakikisha kuwa hawafanyi kazi hiyo mpaka wawe wamepata idhini kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri  wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani  wakati akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini katika wilaya ya Babati na Mbulu mkoani Manyara.

“Baadhi ya Wakandarasi hawa wanaofanya wiring, wamekuwa wakitoza gharama kubwa ya kutoa huduma hiyo na matokeo yake inapelekea wananchi kuchelewa kuunganishwa na huduma ya umeme,” alisema Dkt Kalemani.

Aliongeza kuwa,  baadhi ya wakandarasi wamekuwa wakifanya kazi hiyo chini ya viwango na kupelekea matatizo mbalimbali kwa wananchi ikiwemo nyumba kupata hitilafu za umeme na kusababisha majanga kama ya moto na kusisitiza kuwa yeyote atakayekiuka agizo hilo atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Wakati huohuo, Dkt. Kalemani aliwaagiza Watendaji wa TANESCO kutoa elimu kwa wananchi  kuhusu faida ya kutumia kifaa kijulikanacho kama UMETA (Umeme Tayari) ambacho huwasha umeme ndani ya  nyumba bila mteja kulazimika kuingia gharama za kufunga nyaya za umeme ndani ya nyumba. 

“Kifaa hiki gharama yake ni shilingi 36,000 tu  na kinaweza kutumika kwenye nyumba ya chumba kimoja hadi vitano hivyo TANESCO mnapaswa kutoa elimu kwa wananchi ili wakitumie kifaa hiki,”alisema Dkt.Kalemani.

Aidha Dkt Kalemani aliwaagiza Watendaji wa  TANESCO nchi nzima,  kupeleka wataalam wawili katika sehemu zenye uhitaji mkubwa wa umeme ambazo kuna shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii ili kusogeza huduma kwa wananchi badala ya wananchi hao kuwafuata TANESCO ofisini na kueleza kuwa hiyo itasaidia kuongeza idadi ya wateja wanaotumia huduma ya umeme na Shirika kuongeza mapato yake.

Aidha akizungumza na watendaji wa mkoa wa Manyara, Dkt Kalemani  alisema kuwa  matumizi ya umeme katika mkoa ni chini ya megawati 8 huku uwezo wa mitambo ukiwa ni megawati 40 hivyo kuwataka watendaji hao kuhamasisha wawekezaji mbalimbali kwenda kuwekeza kwenye mkoa ili kuongeza matumizi ya umeme huo.

“Hamasisheni Wawekezaji ili kiwango cha matumizi ya umeme kiongezeke na TANESCO hamasisheni wananchi kutumia umeme kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu gharama za umeme kwani wengi wanasuasua kuunganisha umeme kwa kuhofia kuwa gharama ni kubwa .

Akizungumza kuhusu hali ya umeme katika mkoa huo, Kaimu Mkuu wa mkoa wa Manyara, Mhandisi Raymond Mushi alisema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba 2016, TANESCO imeunganisha umeme kwa wateja wapya 1919, huku lengo likiwa ni kuunganisha wateja 825 na hivyo kuvuka lengo kwa lililowekwa.

Kuhusu miradi ya usambazaji umeme vijijini Awamu ya Pili inayokamilika Oktoba 15, 2016, Mhandisi Mushi alisema kuwa miradi hiyo itanufaisha vijiji 96 ambapo wilaya ya Babati  itakuwa na vijiji 56 vitakavyounganishwa na huduma ya umeme, wilaya ya Mbulu itakuwa na vijiji 7, Hanang Vijiji 8 na Simanjiro ni vijiji 15.

Kuhusu vijiji ambavyo havijapata umeme katika Awamu hiyo ya Pili, Dkt Kalemani alisema kuwa vijiji vyote ambavyo havina umeme  nchini vitaunganishiwa umeme kupitia miradi ya REA ya Awamu ya Tatu ambayo utekelezaji wake utaanza mwishoni mwa mwaka huu.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (mwenye suti ya Bluu) akiwahutubia wananchi wa kijiji cha Magala wilayani Babati, wakati alipofika katika kijiji hicho ili kukagua utekelezaji wa miradi ya usambazaji umeme vijijini ya Awamu ya Pili.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani akiwaonyesha wananchi wa kijiji cha Mutuka wilayani Babati, kifaa cha umeme kijulikanacho kama UMETA ambacho kinaweza kuwasha umeme ndani ya nyumba bila kufunga nyaya za umeme. Naibu Waziri alifika katika kijiji hicho kukagua utekelezaji wa miradi ya usambazaji umeme vijijini ya Awamu ya Pili.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (katikati) akivalishwa mgololo na wananchi wa kijiji cha Magala wilayani Babati, wakati alipofika katika kijiji hicho ili kukagua utekelezaji wa miradi ya usambazaji umeme vijijini ya Awamu ya Pili. Wananchi walimvalisha mgololo huo kuonyesha shukrani zao kwa Serikali baada ya kijiji hicho kupata umeme kupitia miradi ya usambazaji umeme vijijini ya Awamu ya Pili.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...