Na Neema Mwangomo (MNH)
Hospitali ya Taifa Muhimbili inaendelea kutekeleza azma ya Serikali ya kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje ambao mara nyingi walikuwa wakifuata matibabu yasiyopatikana hapa nchini ama kutokana na kutokuwepo wataalamu au ukosefu wa vifaa vya kutolea huduma husika. 
Akizungumza na wanahabari leo Jijini Dar Es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru amesema katika kutekeleza hilo, Septemba 25, 2016, Hospitali itapeleka watalaamu saba nchini India katika Hospitali ya Apollo iliyopo New Delhi ili wakajifunze kwa njia ya vitendo jinsi ya kufanya upasuaji na upandikizaji wa kifaa cha usikivu kwa watu wazima na watoto. 
“Wataalamu hao ni pamoja na madaktari bingwa wawili wa upasuaji wa pua, koo na masikio, wauguzi wawili wa chumba cha upasuaji, mtalaam mmoja wa kupima usikivu pamoja na watalaam wawili wa kufundisha jinsi ya kuongea hususani kwa watoto waliozaliwa na tatizo hilo” amesema. 
Prof. Museru amesema kuwa takwimu za Hospitali ya Taifa Muhimbili zinaonyesha kuwa asilimia 95 ya wagonjwa ambao wanahitaji kufanyiwa upasuaji wa kuwekewa kifaa cha usikivu ni watoto wadogo na kusisitiza kuwa  huduma hii itasaidia watoto wengi hapa nchini na pia kujenga uwezo kwa wataalamu wa ndani ya nchi.   
“Gharama za kupandikiza kifaa cha usikivu kwa mtoto mmoja ni kati ya shilingi milioni 80 hadi 100 anapopelekwa nje ya nchi wakati mgonjwa mmoja anayepandikizwa figo nje ya nchi pia hugharimu kiasi cha shilingi milioni 40 hadi 60. Uwepo wa huduma hizi hapa nchini utawezesha watanzania wengi kupata huduma hii na kwa gharama nafuu zaidi na kupunguza mzigo kwa Serikali wa kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwani gharama za matibabu zitapungua kwa zaidi ya asilimia 50” amesisitiza.
 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Lawrence Museru akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusu wataalamu saba wakiwamo madaktari wanakwenda India Septemba 25, mwaka huu kwa ajili ya kujifunza upandikizaji wa kifaa cha usikivu ( COCHLEA IMPLANT).
 Waandishi wa habari wakimsikiliza Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Pua, Koo na Sikio, Dk Edwain Liyombo wakati akizungumza leo kuhusu watoto wenye matatizo ya usikivu na kuzungumza.
 Baadhi ya wataalamu wanaokwenda India Septemba 25, mwaka  huu kujifunza upandikizaji wa kifaa cha usikivu wakimsikiliza mkurugenzi.
Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Pua, Koo na Sikio, Dk Edwain Liyombo akizungumza na waandishi wa habari leo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...