Naibu Katibu Mtendaji kutoka Tume ya Mipango, Mhandisi Happiness Mgalula akitoa hotuba wakati akifungua mafunzo ya Usimamizi na Utayarishaji wa Miradi ya Uwekezaji katika Sekta ya Umma mjini Dodoma, Kulia ni mkufunzi wa mafunzo hayo, dkt. John Mduma kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kushoto ni Kaimu Naibu Katibu Mtendaji, Klasta ya Uchumi Jumla kutoka Tume ya Mipango dkt. Lorah Madete.
 Picha ya pamoja ya washiriki wa mafunzo ya Usimamizi na Utayarishaji wa Miradi ya Uwekezaji katika Sekta ya Umma kanda ya kati inayojumuisha mikoa ya Manyara, Singida na Dodoma.

Na Adili Mhina, Dodoma.
Tume ya Mipango imewashauri maofisa wa serikali wenye dhamana ya kusimamia miradi ya umma kuhakikisha wanatumia mbinu za kisasa katika kuchambua, kuchagua, kutekeleza na kusimamia miradi ya serikali ili kuhakikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo yanafikiwa kwa wakati.

Ushauri huo umetolewa jana mjini Dodoma na Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango anayesimamia Klasta ya Miundombinu na Huduma, Mhandisi Happiness Mgalula alipokutana na maofisa mipango wa Ofisi za  Mikoa na Halmashauri za kanda ya kati iliyojumuisha Mikoa ya Dodoma, Singida na Manyara kwa lengo la kutoa elimu katika kuandaa, kusimamia, na kutekeleza miradi ya Umma.

Alisema kuwa Serikali ilifanya tathmini na kugundua kuwa hakuna vigezo vinavyofanana katika kuandaa na kuchagua miradi ya umma katika taasisi mbalimbali za Serikali kitu kinachorudisha nyuma juhudi za kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.

“Dira ya Taifa ya Maendeleo inaelekeza kuwa hadi kufikia mwaka 2025 Tanzania inatakiwa iwe inchi ya uchumi wa kati na kwa vile tumedhamiria kwa dhati kifikia hapo ni lazima tujipange upya na kutumia utaalamu wa kisasa na vigezo vinavyofanana katika kuchagua miradi yenye uwezo wa kulifikisha taifa huko,” alisema Mgalula.

Kukosekana kwa vigezo vinavyofanana kumesababisha upungufu mkubwa katika  miradi ya umma huku  ikipelekea miradi mingine kukosa mikopo katika soko la mitaji la ndani au la kimataifa kutokana na kuwa na maandiko yasiyokidhi vigezo vinavyohitajika.
Mgalula aliongeza kuwa ili kuwekeza katika miradi yenye tija itakayoharakisha Tanzania kuingia katika nchi za uchumi wa kati, Tume ya Mipango imedhamiria kuendelea na utaratibu wa kutoa mafunzo kwa walengwa nchi nzima ili kuongeza utaalam katika kuweka vipaumbele vichache vyenye ufanisi kwa kila mwaka wa bajeti kuliko kuwa na miradi mingi isiyokamilika.

Na kwa upande wa maafisa wanaopata elimu hiyo wanakiri kuwepo kwa changamoto nyingi katika maandalizi ya miradi ya umma kutokana kukosekana kwa mfumo unaofanana katika uwekezaji wa miradi ya umma.

“Tayari tumeanza kuelekezwa namna ya kuandaa miradi kwa kuzingatia vigezo vya kisasa viliyoainishwa katika mwongozo wa usimamizi wa uwekezaji wa miradi ya serikali, hii itatusaidia kuwa na utaratibu mmoja na unaoeleweka  tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo kila mradi mpya ulikuwa na mfumo wake” Alisema Bwana Mkama kutoka Dodoma.

Naye Afisa Mipango kutoka Halmashauri ya Babati Bw. Godlisten Geofray alieleza kuwa kuwepo kwa mfumo wa kisasa kutasaidia kuweka kumbukumbu sahihi za miradi hata ile ambayo haitafanikiwa kupata fedha kwa mwaka husika pale mfumo wa kanzidata utakapoanzishwa ambao utahifadhi kubukumbu za miradi yote nchini.

Washiriki wa mafunzo hayo wameonesha kuridhishwa na juhudi zinazofanywa na Tume ya Mipango katika kutoa elimu hiyo katika ngazi mbalimbali huku wakieleza kuwa utaratibu huo utasaidia kuimarisha mawasiliano kwenye bajeti ya miradi kati ya serikali kuu na serikali za mitaa.

Wataalamu hao wamesisitiziwa kuwa miradi yote itakayohitaji fedha za Serikali katika Bajeti italazimu kufuata utaratibu uliobainishwa katika Mwongozo wa Usimamizi na Utayarishaji wa Miradi ya Uwekezaji katika sekta ya Umma ili kuweza kuimarisha ufanisi na kupata thamani ya fedha.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...